Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Elimu

Umoja na mshikamano ni vinasaba na utambulisho wa watanzania!

Umoja, upendo na mshikamano ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa watanzania mahali popote pale walipo! - RV

15/05/2018 12:03

Chuo kikuu kinapaswa kuwa ni mahali muafaka pa kukuza na kudumisha mchakato wa mabadiliko unaofumbatwa katika majadiliano yanayojenga utamaduni wa watu kukutana. Ikumbukwe kwamba, hekima ya kweli ni tafakari, majadiliano na mkutano kati ya watu. Mshikamano wa kitaifa ni jambo linalowezekana, kwa kukazia zaidi mfumo wa elimu unaopaswa kuwa ni chachu ya maendeleo kwa kuzingatia tunu msingi za elimu zinazotolewa kwenye Chuo Kikuu: kwa kufundisha, kufikiri na kutenda kama sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu. Hii ni tafakari ya kina iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Chile.

Baba Mtakatifu anasema, haya ndiyo majiundo ya akili “forma mentis”. Ili kuweza kufikia hatua hii ya maendeleo endelevu ya binadamu kuna haja ya kushirikisha lugha mbali mbali zinazowatambulisha kama watu; elimu inayoweka uwiano mzuri kati ya: akili, moyo na matendo; mambo msingi yanayoweza kuwasaidia wanafunzi kukua na kukomaa kama mtu binafsi na kama jamii. Elimu iwasaidie wanafunzi: kufikiri na kutekeleza kile wanachofikiri kama sehemu muhimu sana ya huduma kwa binadamu na jamii katika ujumla wake. Mchakato wa elimu uwawezeshe wanafunzi kushirikishwa zaidi katika masuala ya elimu ili kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza huko mbeleni.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, mawazo hayana budi kumwilishwa katika lugha, ili kuwaunganisha watu. Changamoto kubwa kwa wakati huu ni watu kufikri na kutenda katika ombwe bila ya kuwa na msingi thabiti na matokeo yake, maisha ya hadhara hayana nafasi tena na hivyo ubinafsi kushika kasi ya ajabu. Maisha ya kijumuiya yapewe msukumo wa pekee zaidi, ili kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa. Watu wawe na utambuzi wa kumbu kumbu endelevu zinazowatambulisha kama: familia, jamii na taifa! Bila umoja na mshikamano, watoto hawana matumaini ya kesho iliyo bora zaidi na kwamba, ubinafsi utaota mizizi na matokeo yake ni kinzani na mipasuko ya kijamii.

Kutokana na changamoto hizi, Chuo kikuu hakina budi kuhakikisha kwamba, kinatoa mwelekeo sahihi ili kujenga mshikamano na ukuaji wa jumuiya. Kumbe, Chuo kikuu cha Kikatoliki kinapaswa kuwa pia ni mahali pa uinjilishaji, chemchemi ya furaha  ya Injili inayolipyaisha Kanisa, tayari kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Jumuiya ya Chuo Kikuu itambue kwamba, ina dhamana na wajibu wa kimissionari kwani huko wanakutana na watu mbali mbali.

Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki Watanzania wanaosoma Roma pamoja na walezi wao, katika Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, tarehe 13 Mei 2018 wameadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa kumshukuru Mungu aliyewawezesha baadhi yao kuhitimu masomo katika viwango mbali mbali, kupiga hatua katika wito wao wa kipadre na maisha ya kitawa. Padre Felix Mushobozi, C.PP.S, Afisa mwandamizi kutoka Umoja wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Italia baada ya kukabidhi vyeti kwa wale waliokuwa wanahitimu, amekazia umoja na mshikamano wa watanzania kwa kutambua kwamba, mshikamano ni fadhila ya hali ya juu ya Kikristo inayotekelezeka kwa kugawana zaidi mema ya kiroho hata kuliko ya kimwili.

Amewashukuru na kuwapongeza viongozi wa Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki Watanzania kwa sadaka na majitoleo yao kwa kutambua kwamba, ndani ya Kanisa uongozi ni huduma. Umoja huu ni kiungo muhimu sana cha wanafunzi pamoja na walezi wao na kwamba, unapaswa kukuzwa, kudumishwa na kuendelezwa zaidi katika matukio mbali mbali ya maisha yao na hasa wanapokuwa ughaibuni, mahali penye changamoto kibao!

Watanzania wasaidiane, wapendane, kuheshimiana na kuthaminiana ili kukuza na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa! Padre Mushobozi amesema, wahitimu wanao wajibu na dhamana nyeti ya kutumia vyema elimu, ujuzi na maarifa waliochota kutoka katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu vya kipapa hapa mjini Roma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Tanzania. Wao ni matunda ya sadaka kubwa na majitoleo ya Kanisa la Tanzania, wanaporejea sasa nyumbani watumie vyema elimu yao na kamwe wasiwe “mzigo kwa Kanisa la Tanzania” bali chachu muhimu ya ukuaji wa familia ya Mungu katika ari na moyo wa kimisionari, kitamaduni, kiliturujia pamoja na kuhakikisha kwamba, wanafanya tafiti ili kuboresha maisha na utume wa Kanisa la Tanzania. Huu si wakati wa kubweteka!

Padre Mushobozi amesema kwamba, umoja na mshikamano ni vinasaba na utambulisho wa watanzania. Kwa wale ambao wametindikiwa na sifa hizi, wanakosa utambulisho wao kama watanzania. Kumbe kuna haja kwa wakleri, watawa na waamini walei kujenga tena umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kutambua na kuthamini mipaka ya maisha na utume wao, ili kuweza kutembea kwa pamoja kama familia ya Mungu inayowajibikiana na kusaidiana, dhana ya sinodi katika maisha na utume wa Kanisa!

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara linahimiza roho na sadaka ya umisionari na kwamba, sasa ni zamu ya Wakristo Barani Afrika kuwa wamisionari kwa kuwasaidia wengine kukua kiroho, kuamsha imani, kutangaza na kushuhudia Injili. Padre Joseph Shiyo kutoka Shirika la Roho Mtakatifu (Holy Ghost Fathers) ambaye ni kati ya walezi wanaoishi na kufanya utume wao mjini Roma amesema, Shirika lake mwaka huu, 2018 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu lilipoingia Tanzania Bara na kwa sasa limeenea katika nchi 62 duniani. Padre Shiyo amewakuimbusha wakleri na watawa waliohitimu kwamba, wao ni viongozi ambao wamefundwa barabara na wanayo dhamana ya kuonesha dira na njia kwani uongozi ni huduma. Ni wajibu wao kuwasaidia watu wa Mungu kutambua na kuambata mambo msingi katika maisha yao. Katika kipindi hiki cha Novena kwa Roho Mtakatifu, wamwombe aweze kuwakirimia mapaji yake, ili waweze kumshuhudia Kristo Yesu katika maisha na utume wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

15/05/2018 12:03