2018-05-14 10:50:00

Ninyi ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka, vyombo vya huruma na upendo!


Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki Watanzania wanaosoma Roma pamoja na walezi wao, katika Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, tarehe 13 Mei 2018 wameadhimisha Mafumbo ya Kanisa kwa kumshukuru Mungu aliyewawezesha baadhi yao kuhitimu masomo katika viwango mbali mbali, kupiga hatua katika wito wao wa kipadre na kitawa pamoja na kumwomba Roho Mtakatifu aweze kusaidia kujiandaa kufanya vyema mitihani yao, ili nguvu ya Roho Mtakatifu ikishakuwajilia juu yao, waweze kuwa ni mashuhuda, vyombo vya huruma na mapendo kwa familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania.

Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kikanisa cha Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma. Umoja wa Wanafunzi pia umemchangua Padre Florence Kamugisha Ngaiza kuwa Katibu wa Umoja huo kuanzia sasa. Ibada ya Misa Takatifu imeongozwa na Padre Felix Mushobozi, C.PP.S, Afisa mwandamizi kutoka Umoja wa Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Italia. Padre Mushobozi katika tafakari yake amefafanua mambo makuu mawili yanayofumbatwa katika Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni.

Mosi, ni ukuu, nguvu na utukufu wa Kristo Mfufuka anayepaa mbinguni kwa sauti ya baragumu na kelele za shangwe na hivyo kufunga ngwe ya kwanza ya ujio wake uliotekelezwa kwa njia ya Fumbo la Umwilisho ambalo limepata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufuufuko wake. Kwa muda wa siku 40 aliwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo na kuwaimarisha katika imani kwamba, kwa hakika Yeye alikuwa ni Kristo na Bwana wa wazima na wafu.

Pili, Wafuasi wa Kristo wanapewa dhamana na utume wanaopaswa kuuendeleza hapa dunia kwa kuwa ni vyombo vya wokovu kwa watu wa Mataifa. Wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa, dhamana wanayoitekeleza kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayewasimika rasmi kuwa nguzo za Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji; wanapewa silaha za kupambana na nguvu za giza zinazopingana na Ufalme wa Mungu pamoja na kuhakikishiwa uwepo endelevu wa Kristo kati yao. Kumbe, wanatumwa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka. Padre Mushobozi anakaza kusema, Kanisa limepewa dhamana na jukumu kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kati ya watu! Kusoma alama za nyakati; ili kutafsiri yanayotokea katika maisha ya watu, kutafuta majibu ili kukabiliana na changamoto mamboleo zinazowakabili watu wa nyakati hizi; kuonesha uhusiano uliopo kati ya matukio na uwepo wa Kristo Yesu.

Padre Mushobozi pia amegusia kuhusu maadhimisho ya Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni ambayo kwa mwaka 2018 yanaongozwa na kauli mbiu “…Kweli itawaweka huru: Habari za kughushi na uandishi wa habari wa amani”. Kama sehemu ya uinjilishaji wa kina, wakristo wawe ni watangazaji hodari wa Habari Njema ya Wokovu kwa kutumia lugha mpya, yaani lugha inayofahamika na kueleweka na watu, ili kujenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano, ili kubomoa kuta za utengeno kati ya watu wa Mataifa. Lugha ya upendo, ndiyo lugha mpya inayovaliwa njuga na Mama Kanisa kwa watu wa nyakati hizi.

Baada ya kupaa Bwana Mbinguni, Kanisa linahamasishwa kusoma “Nyakati za Ishara”, kwa kuwa ni chombo cha huruma, upendo, msamaha na unabii! Hiki ni kitovu cha Mafundisho Jamii ya Kanisa. Padre Felix Mushobozi amehitimisha mahubiri yake kwa kusema, “Yesu amepaa na kuketi kuume kwa Mungu Baba pamoja na ubinadamu wetu, akituwezesha nasi, siku moja baada ya kumaliza safari yetu hapa duniani, nasi tutapaa na kuketi kuume kwa Baba  milele!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.