Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Vyombo vya mawasiliano vilinde na kudumisha utu na heshima ya binadamu

Vyombo vya mawasiliano ya jamii vinayo dhamana na wajibu wa kulinda, kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu sanjari na ujenzi wa udugu na utu wema.

12/05/2018 16:20

Chama cha Waandishi wa Habari Wakatoliki Ubelgiji, “Logia”, kilianzishwa katika mji wa Fiandre ili kukuza na kudumisha tunu msingi za Kikristo katika vyombo vya mawasiliano ya jamii, ili kuleta maboresho katika mijadala ya kiuchumi, maendeleo endelevu ya binadamu, siasa, maisha ya kiroho, sanaa, sayansi, elimu na majiundo makini ya binadamu; haki na michezo: Kimsingi ni chama kinachojikita katika mchakato wa kutaka kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya tunu msingi za Kiinjili. Chama hiki kinawajumuisha wanachama wataalam na mabingwa katika nyanja mbali mbali za maisha ya mwanadamu wapatao 150 wanaotaka kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili inayopendeza na kufariji; kwa kupyaisha imani na uaminifu katika mchakato mzima wa uinjilishaji, ili kuwatangazia watu kwamba, kweli Mungu ni upendo ambao umefunuliwa kwa namna ya pekee kabisa kwa njia ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Huu ni ndio utajiri wa hekima ya Mungu unaoendelea kuwastaajabisha walimwengu.

Kutokana na mwelekeo huu, dini kamwe haiwezi kuachwa kuwa ni jambo la faragha katika maisha ya mwamini, kwani athari zake zinaonekana katika medani mbali mbali za maisha ya watu, kwani hii ni chachu ya mabadiliko kutoka katika undani wa mtu, kwa kurithisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, ili kuacha dunia walau kwa kiasi fulaini ikiwa ni bora zaidi. Hii ndiyo dhamana na wajibu wa vyombo vya mawasiliano ya jamii, vinavyopaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi kwa wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Wakatoliki Ubelgiji na kukaza kwa kusema, vyombo vya habari vina wajibu wa kujenga jamii inayosimikwa katika haki, udugu na utu kadiri ya moyo wa Mwenyezi Mungu. Haya ni mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga na waandishi wa habari wakatoliki katika majadiliano kwani Injili ya Kristo ni njia inayomwilisha utu wa binadamu katika shule ya Yesu; Bwana na Mwalimu na wala si kama adui anayepaswa kushughulikiwa kama “Mbwa koko”, bali kuheshimiwa, kuthaminiwa na bila kuchoka kutenda mema!

Baba Mtakatifu anawahamasisha wajumbe hawa katika shughuli zao za kila siku kujitahidi kushuhudia ile kiu ya Kanisa ya kutaka kuwasindikiza watu kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kukuza na kudumisha sera na mikakati inayoheshimu utu, ustawi na mafao ya wengi kwa kuchota utajiri unaobubujika kutoka katika Mapokeo ya Kikristo na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Utajiri huu unapaswa kushuhudiwa kwa njia ya maneno na matendo yanayoonesha imani thabiti kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ni zawadi ya pendo la Baba wa milele inayotolewa kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, masikitiko, utupu wa maisha ya ndani na hali ya kutengwa ili kuiendea chemchemi ya furaha ya maisha ya uzima wa milele! Dhamana hii wanaweza kuitekeleza vyema zaidi ikiwa kama maisha yao yataendelea kuboreshwa kwa njia ya sala, ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa na karama za Roho Mtakatifu anayewakirimia utakatifu wa maisha katika huduma kama utambulisho wa mihimili ya uinjilishaji. Wanachama wajenge na kudumisha umoja na udugu katika tofauti zao msingi kadiri ya karama za Roho Mtakatifu. Lengo ni ushuhuda wa maisha unaojenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano na madaraja ya watu kukutana, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na watu wasiokuwa na sauti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

12/05/2018 16:20