Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko: Rutubisheni huduma ya upendo kwa sala na tafakari!

Chama cha Waamini Walei wa Mtakatifu Petro ni wamisionari jasiri a upendo wa Kristo na mashuhuda wa huruma na wema wa Mungu; chombo cha faraja kwa maskini na watu waliokata tamaa.

12/05/2018 16:58

Chama cha Waamini Walei wa Mtakatifu PetroCircolo San Pietro” kilianzishwa kunako mwaka 1869 na kikundi cha vijana kutoka Roma, ili kuonesha uaminifu wao kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na kusaidia kufadhili matendo ya huruma yanayotekelezwa na Mama Kanisa kwa ajili ya maskini ndani na nje ya Roma. Hiki ni kikundi kinachojitambulisha kwa maisha ya sala, utume na sadaka. Tangu wakati wote huo, chama hiki kimekuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo kwa maskini!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 12 Mei 2018 amekutana na kuzungumza na Chama cha Waamini Walei wa Mtakatifu Petro. Kwa niaba ya wanachama wote, amemskukuru Rais wake Bwana Duca Leopoldo Torlonia kwa ushuhuda wa huduma ya upendo wanayoitoa kwa maskini. Wao ni sawa na shamba la Kanisa la Roma. Ni kielelezo cha Kanisa linalotoka kimasomaso kwa kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye kiu na njaa ya kusikilizwa; watu wanaotamani kushirikiana na kushikamana na wengine; watu wanaotaka kujenga na kudumisha ujirani mwema kwa njia ya mshikamano.

Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo njia wanayopaswa kuifuata katika maisha na utume wao! Wasiwaonee aibu maskini ambao ni amana na utajiri wa Kanisa! Ndani ya kila mtu wajitahhidi kuiona sura ya Kristo anayeteseka. Wawe wamisionari jasiri wa upendo wa Kikristo na mashuhuda wa huruma na wema wa Mungu na chombo cha faraja kwa maskini na wale wote waliokata tamaa katika maisha!

Mbele yao kuna umati mkubwa wa waamini waliotangazwa kuwa wenyeheri na wengine ni watakatifu! Hawa ni watu waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani zao, kiasi hata cha kuwa ni chemchemi ya utakatifu wa maisha. Waamini walei wanashiriki unabii wa Kristo, kwa njia ya ushuhuda wa imani na mapendo Chama hiki ni chombo kinachowaelekeza wanachama wake kwenye chemchemi ya utakatifu wa maisha. Kwa njia ya matendo ya huruma, wanaiwezesha neema ya Sakramenti ya Ubatizo kuzaa matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru kwa uwepo na ushiriki wao mkamilifu katika huduma kwa maskini inayotekelezwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro mjini Roma. Huduma hii ya upendo iendelee kurutubishwa kwa njia ya sala na tafakari makini ya Neno la Mungu, mwanga katika njia na mapito yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

12/05/2018 16:58