Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Nyaraka

Papa Francisko anasema, amani ndiyo habari yenyewe! Idumisheni!

Papa Frabcisko anasema, amani ndiyo habari ya kweli inayomlenga mtu mzima ili kumjengea uwezo wa kusikilizana na kujadiliana katika ukweli na uwazi, kwa kuvutwa na wema na uzuri ili kuwajibika barabara. - REUTERS

12/05/2018 17:17

Ukweli utawaweka huru ndiyo changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake katika maadhimisho ya Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni inayoadhimishwa tarehe 13 Mei 2018. Watu wanapaswa kutambua, kusimamia na kuupenda ukweli, ili uwongo uweze kujitenga. Ukweli ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na Kristo Yesu anakaza kusema kwamba “Yeye ni ukweli, njia na uzima” na kwamba, mtu anayegundua na kuambata ukweli katika maisha yake, atakuwa huru kweli kweli. Watu wajifunze kupambanua ukweli ili kujenga umoja na mshikamano; utamaduni wa kusikilizana katika ukweli na uwazi. Kamwe watu wasichoke kutafuta na kuambata ukweli ilikujenga umoja na ukomavu katika tafakari, hatimaye kudumisha majadiliano yanayozaa matunda yanayokusudiwa yaani haki, amani, upendo na mshikamano.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, amani ndiyo habari ya kweli inayomlenga mtu mzima ili kumjengea uwezo wa kusikiliza, kujadiliana katika ukweli na uwazi, kwa kuvutwa na: ukweli, wema na uzuri ili hatimaye, kuwajibika barabara. Wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii wanao wajibu na utume mzito wa kulinda ukweli wa habari kwa kutambua kwamba, mlengwa mkuu ni binadamu. Habari inalenga kuwaunda watu wengine katika jamii, kugusa maisha yao ili kudumisha wema na uaminifu unaofungua njia ya umoja na amani. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawataka waandishi wa habari kujikita katika uandishi wa habari wa amani kwa kuondokana na habari za kughusi zinazochezea vionjo na hisia za watu kama alivyokuwa nyoka, Ibilisi katika Agano la Kale. Uwe ni uandishi wa habari kwa ajili pamoja na watu, yaani uandishi wa habari kwa ajili ya huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu; ili kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti.

Waandishi wa habari wasijikite tu kwa “Breaking News”, bali wawe na ujasiri, ari na moyo wa kupembua kwa kina na mapana sababu msingi zinazopelekea vita, kinzani na migogoro ya kijamii, ili kujenga uelewa mpana zaidi utakaosaidia mchakato wa suluhu na amani ya kudumu. Uandishi wa habari anaoutaka Baba Mtakatifu Francisko ni ule usiokuwa wa vita ya maneno na makelele kibao! Mwishoni, anataka waandishi wa Habari wawe ni vyombo na mashuhuda wa mchakato wa maridhiano, haki na amani duniani akiwataka kurejea katika Sala ya Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

12/05/2018 17:17