Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko anadadavua magonjwa ya maisha ya kiroho!

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume Furaha ya Injili anapembua kwa kina na mapana magonjwa ya maisha ya kiroho yanayoweza kukwamisha maisha na utume wa Kanisa.

12/05/2018 07:34

Baba Mtakatifu Francisko,  alifungua rasmi kongamano la kichungaji Jimbo kuu la Roma kunako mwaka 2017 alikazia zaidi: dhana ya Injili ya familia jijini Roma; umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu; kuandamana na vijana kwa kuwasikiliza kwa makini ili kujibu matamanio yao halali katika maisha; umuhimu wa kuendelea kujikita katika elimu endelevu; jinsi ya ambavyo Kanisa linaweza kukabiliana na changamoto za maisha na utume wa vijana wa kizazi kipya pamoja  na umuhimu wa kuboresha maisha ya kiroho kwa kupambana na Ukosefu wa kinga za kiroho mwili, yaani UKIROHO au kwa maneno mengine kutafuta tiba muafaka ya magonjwa ya kiroho ambayo yamebainishwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa kitume “Evangelium gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anasema, furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi ya wokovu wanawekwa huru na hivyo kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke hasi. Pamoja na Kristo daima, furaha inazaliwa upya! Baba Mtakatifu Francisko anasema, furaha ya Injili ndiyo chapa makini ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo! Baba Mtakatifu anakaza kusema, furaha ya Injili daima ni mpya na ni furaha inayoshirikishwa; ni furaha inayoinjilisha, inayopendeza na kufariji, ili kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo.

Pamoja na mambo mengine, Baba Mtakatifu anakazia mabadiliko ya umisionari wa Kanisa, upeo wa tatizo la kujiaminisha katika Jumuiya; utangazaji na ushuhuda wa Injili; mwelekeo wa kijamii katika mchakato wa uinjilishaji; umuhimu wa Kanisa kuwa na mihimili ya uinjilishaji iliyojazwa nguvu na karama za Roho Mtakatifu pamoja na kutambua kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Kanisa na Uinjilishaji! Askofu mkuu Angelo Donatis, Makamu Askofu mkuu Jimbo kuu la Roma, katika barua yake ya mwaliko kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma, anasema, hapo tarehe 14 Mei 2018, saa 1:00 za jioni, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana na kuzungumza na waamini wa Jimbo kuu la Roma, ili kuhitimisha hija ya maisha ya kiroho ambayo imejikita katika kutambua magonjwa ya maisha ya kiroho, ili yaweze kupatiwa tiba muafaka kwa wakati wake!

Askofu mkuu Angelo Donatis anasema, Nabii Isaya anazungumzia kuhusu saumu na Ibada anayoitaka Mwenyezi Mungu ni kuwagawia watu sehemu ya chakula chako, kuwahifadhi maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na kuwavika walio uchi. Kwa maneno machache, waamini wanahamasishwa kutelekeza matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama sehemu ya imani tendaji. Baadhi ya magonjwa ya kiroho yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo ni: “uchumi unaobagua na kuwatenga watu.” Hii inatokana na utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia; uchumi unaogubikwa katika fedha kwa kutafuta daima faida kubwa matokeo yake ni kukua na kuenea kwa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani.   Ugonjwa huu unaweza pia kuipekenya hata Jumuiya ya Wakristo kwa baadhi ya watu kutoa kipaumbele cha kwanza kwa masihali yao binafsi, kwa kubinafsisha na kutafisha rasilimali za dunia kwa matumizi binafsi. Kumbe, tiba ya ugonjwa huu ni toba na wongofu wa ndani kwa kuambata ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ugonjwa wa pili ni vita, malumbano na misigano miongoni mwa Wakristo wenyewe wanaotafuta nafasi za upendeleo na madaraka ndani ya Kanisa kwa ajili ya mafao yao binafsi na matokeo yake ni chuki na uhasama, kiasi cha kusahau Amri ya upendo kwa Mungu na jirani na kwamba, wanatumwa wa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Ugonjwa wa tatu ni: Ubinafsi na utepetevu wa maisha ya kiroho; sumu ya uchoyo na ubinafsi inayoendelea kuwapekenya wakristo kutoka katika undani wa maisha yao, kiasi cha kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa mazoea! Hawa ni watu ambao waamekosa ladha ya maisha kama chumvi isiyokuwa na ladha ambayo haifai kitu! Ni watu ambao mwanga wa maisha yao umefifia na unaendelea kuzimika pole pole kama mshumaa kwenye upepo mkali!

Ugonjwa wa nne ni kutopea katika maovu na kumezwa na malimwengu! Ni waamini ambao wamekosa amani na furaha ya ndani kwa kujengewa hofu na manabii wa maangamizi kuhusu mwisho wa dunia; hali ambayo hudumaza ujasiri, ari na mwamko wa maisha ya kiroho pamoja na kupoteza imani. Waamini watambue udhaifu na uwepo wa dhambi katika maisha yao, lakini, wanapaswa kusonga mbele bila ya kukata tamaa kwa kutambua kwamba, ushindi wa Kristo Yesu umetundikwa juu ya Msalaba, Bendera ya ushindi ili kupambana na utasa wa maisha ya kiroho!

Ugonjwa wa tano ni ubinafsi usiokuwa na mashiko wala mvuto, kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na maisha ya Kikristo kwa ari na moyo mkuu. Kwa njia hii, mwamini anapoteza dira, mwelekeo na utambulisho wa maisha ya Kikristo kiasi hata cha kushindwa kusali, kujenga na kudumisha umoja na udugu, kwani anajisikia amefika nyumbani katika ubinafsi wake! Ni mwamini ambaye amekauka kama “mti mkavu” hafai tena kushimbwa mzizi wa dawa! Katika ubinafsi wake anajiona kuwa kama mteule wa Bwana, kiasi cha kuchindwa kuchangamana na waamini wenzake. Hii inaonesha kwamba, waamini wamepoteza ile furaha ya kukaa pamoja kama ndugu wamoja na matokeo yake, wanataka kujifungia ndani na kuwa kama “Watoto wa geti kali”.

Ugonjwa wa sita ambao kwa sasa unachemshiwa dawa na Baba Mtakatifu ili aweze kuitoa wakati atakapokutana na familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma ni kutopea katika malimwengu ya maisha ya kiroho, kwa kisingizio cha kulipenda Kanisa na kuhudhuria Ibada kwa kutaka kuonekana mbele za watu kuwa hata wewe, wamo ingawa hawavumi! Ni waamini wanaotafuta utukufu mbele ya watu, lakini ni watupu kama debe tupu ambalo haliachi kutika katika maisha yao ya kiroho! Watu wenye kiburi ambacho kimegeuka kuwa ni kaburi la maisha yao ya kiroho; watu wanaojiamini kupita kiasi na kuhisi kwamba, wao ni bora zaidi kuliko watu wengine wote. Huu ni Ukristo wa kughushi usiokuwa na mvuto wala mashiko! Kanisa linakuwa ni mahali pa kuendeleza anasa binafsi badala ya kuwa ni uwanja wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani tendaji!

Hii ni tabia ya mtu kutaka kujifurahisha binafsi na matokeo yake anapoteza dira na mwelekeo sahihi wa maisha halisi ya Kikristo! Waamini kama hawa anasema Baba Mtakatifu Francisko wana upeo mfinyu sana wa maisha, hawako tayari kutubu na kumwongokea Mungu, kwa kujifunza kutokana na udhaifu na dhambi zinazowaandama! Kanisa halina budi kutoka katika ubinafsi wake, kwa kuendelea kua aminifu kwa Kristo na tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Kamwe waamini wasikubali kupokwa Injili kwa furaha za mpito! Askofu mkuu Angelo Donatis, Makamu Askofu mkuu Jimbo kuu la Roma anahitimisha kwa kusema, kwa hakika, ni Baba Mtakatifu Francisko mwenyewe atakayeweza kuwapatia dawa ya kuganga, kutibu na kuponya magonjwa haya maisha ya kiroho yanayoendelea kuwapekenya waamini kama alivyoyadadavua katika Wosia wake wake “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili.”

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

12/05/2018 07:34