2018-05-12 07:53:00

Baba Mtakatifu Francisko kukutana na vijana wa Italia, Agosti, 2018


Vijana wa Chama cha Huduma ya Uamsho wa Kikatoliki nchini Italia RnS, watakutana mjini Perugia, Kaskazini Mashariki mwa Italia, kuanzia tarehe 8-11 Agosti 2018, na vijana kutoka sehemu mbali mbali za Italia wanatarajia kukutana na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 11-12 Agosti 2018, kama sehemu ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba hapa mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa vijana wa kizazi kipya kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana anawaalika vijana kusikiliza sauti ya  Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wao, bila kuogopa kwani yupo pamoja nao ili kuwalinda na kuwategemeza!

Anasema ulimwengu bora unajengwa na kudumishwa kutokana na mchango wa vijana wa kizazi kipya, wanaoonesha ukarimu, kwa kutaka mabadiliko, changamoto kubwa iliyoko mbele yao ni kusikiliza kwa makini sauti ya Roho Mtakatifu na dhamiri nyofu, tayari kujisadaka kwa ajili ya kumfuasa Kristo, Bwana na Mwalimu. Kanisa linataka kuwasikiliza vijana, kuguswa na unyenyekevu, imani; mashaka na “madongo” yao!

Baba Mtakatifu anawataka vijana kupaaza sauti zao kwenye Jumuiya, kiasi hata cha kuwafikia viongozi wa Kanisa, ili kabla ya kufanya maamuzi muhimu ya maisha, vijana nao wapate nafasi ya kutoa maoni yao, kwani mara nyingi Mwenyezi Mungu anawapatia vijana suluhu bora zaidi. Baba Mtakatifu anahitimisha barua yake kwa vijana wa kizazi kipya kwa kuwaambia kwamba, Kanisa linataka kuwa chombo cha furaha ya vijana na anapenda kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili aweze kuwashika mkono na kuwaongoza kwenye chemchemi ya furaha timilifu na ukarimu!

Vijana kutoka sehemu mbali mbali za Italia, wanatarajia kukutana na Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 11-12 Agosti 2018 mjini Roma, wakiongozwa na kauli mbiu “Mwalimu unakaa wapi?”. Zote hizi ni juhudi za Mama Kanisa katika ujenzi wa utamaduni na sanaa ya kuwasikiliza na kuwathanmini vijana. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake  kwa Siku ya 55 ya Kuombea Miito Duniani, anawaalika waamini kutafakari kwa kina na mapana mambo makuu matatu: kwanza kabisa: ni kujenga utamaduni na sanaa ya kusikiliza; pili, kufanya mang’amuzi ya miito na tatu ni kuishi upya wa maisha kama unavyopata utimilifu wake katika ufunuo wa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anasema, ujumbe huu ni mwendelezo wa tafakari kwa ajili ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican, kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Hii itakuwa ni nafasi ya kutafakari kwa kina mwaliko wa furaha kama kiini cha maisha kwa watu wa marika mbali mbali. Maisha na uwepo wa watu hapa duniani ni kadiri ya mpango wa Mungu na wala si kwa nasibu tu! Mwenyezi Mungu daima anapenda kukutana, kutembea na kuambatana na waja wake ili kuzima kiu ya upendo inayowaka ndani mwao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.