2018-05-11 14:45:00

Papa Francisko mambo msingi: Utakatifu, Uinjilishaji na Utamadunisho


Kwa mara ya kwanza katika historia Askofu mkuu Rastislav wa Jimbo kuu Presov, Kiongozi mkuu wa Kanisa la Kiorthodox wa Nchi ya Czech na Slovakia, Ijumaa, tarehe 11 Mei 2018 amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu Francisko amekazia amani na mambo yanayowasaidia kujengana kama wafuasi wa Kristo, huku wakitiana shime kumshukuru Mungu kwa njia ya Liturujia Takatifu, kielelezo cha umoja na Kristo Mfufuka. Roma inahifadhi masalia ya Mtakatifu Cyril.

Kadiri ya Mapokeo, inasemekana kwamba, Watakatifu Cyril na Method waliosaidia kurejesha masalia ya Mtakatifu Clement kwa Papa Adriano II, changamoto na mwaliko wa kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha. Wafiadini wamekuwa ni mashuhuda waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake hasa nyakati za madhulumu, kama ilivyo hata kwa nyakati hizi, ambapo kuna umati mkubwa wa wakristo wanaoendelea kuteseka, kunyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Watakatifu Cyril na Method, wawasaidie waamini kutambua na kuthamini utakatifu wa maisha ya Kikristo!

Baba Mtakatifu anasema, uinjilishaji unakwenda sanjari na utamadunisho dhamana iliyovaliwa njuga na watakatifu Cyril na Method katika maisha na utume wao. Kutokana na mchango wao mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa, Mtakatifu Yohane Paulo II, aliwatangaza kuwa wasimamizi wenza wa Bara la Ulaya. Mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho ni mtindo unaopaswa kuigwa, kwa kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu anayeendelea kulihamasisha Kanisa kutoka kifua mbele ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu, sanjari na mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko hata katika zile nchi ambazo, tayari zilikwisha Injilishwa na kuwa na utamaduni wa Kikristo!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, watakatifu Cyril na Method wanaweza kuwasaidia Wakristo kuvuka kashfa ya utengano kutokana na tamaduni na Mapokeo mbali mbali. Lengo ni kujenga umoja katika utofauti kwa kujikita katika upatanisho unaobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu amerejea katika Waraka wa Chieti wa mwaka 2016 uliotolewa na Tume Mchanganyiko ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox unaokazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na ukuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika karne za mwanzo wa Kanisa. Ni matumaini yake kwamba, majadiliano haya yataendelezwa zaidi ili kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.