2018-05-11 09:13:00

Papa Francisko: Jengeni jamii inayopenda na kuthamini amani!


Familia ya Mungu nchini Ujerumani kuanzia tarehe 9-13 Mei 2018 inaadhimisha Siku ya 101 ya Waamini Wakatoliki nchini Ujerumani, “Katholikentag” ambayo kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu “Tafuteni amani”. Hii ni sehemu ya Zaburi ya 34 inayowataka waamini kuacha mabaya, kwa kutenda mema, watafute amani na kuifuatia, changamoto endelevu hata kwa watu wa nyakati hizi. Amani ni tema muhimu sana miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani kutokana na ukweli kwamba, leo hii, vitendo vya kigaidi na wongofu wa shuruti vinatishia amani duniani, kiasi hata cha kuzua vita, machafuko na mipasuko ya kijamii.

Ukosefu wa amani unajidhihirisha hata katika kuta za kifamilia, maeneo ya kazi, kwenye mashirika, vitongojini na hata katika ngazi ya kitaifa na kimataifa. Katika hali na mazingira kama haya, binadamu kamwe haonekani kuwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na matokeo yake, anakuwa ni sababu ya uhasama, chuki na hasira. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko alioiandikia familia ya Mungu nchini Ujerumani kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya 101 ya Waamini Wakatoliki nchini Ujerumani.

Baba Mtakatifu anasema, vitendo vyote hivi vinamjengea hofu kubwa hasa kwa watoto na vijana wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kwa sababu ya vita na ghasia ili: kuokoa maisha yao na kupata hifadhi. Hawa ni watu wanaobisha hodi katika malango ya wananchi wengi wa Bara la Ulaya na katika macho yao, mtu anaweza kuona ile kiu ya kutafuta amani. Miaka 370 iliyopita, mji wa Munster ulishuhudia tukio kubwa la amani, baada ya watu wengi kupigiswa magoti na athari za vita na huo ukawa ni mwisho wa mauaji ya kimbari kutokana na vita ya kidini.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, sherehe hizi mjini hapo, ni mwaliko wa kujifunza kutafuta na kudumisha amani kama njia ya kuendeleza historia kwa siku za usoni. Hii ni dhamana ya kikristo inayopaswa kuvaliwa njuga kuanzia kwenye familia, shule, taasisi na hasa katika medani za kisiasa. Wakristo wawe ni mashuhuda na vyombo vya amani, kwa kuendelea kujizatiti katika kutafuta na kudumisha amani kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni amani yao. Amani ya kweli inasimikwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru kamili, changamoto kwa watu wote ni kujenga jamii inayopenda amani.

Baba Mtakatifu Francisko anaitaka familia ya Mungu nchini Ujerumani kuwa ni chombo cha amani, kinachowajibika kwa kujikita katika huruma. Hii ni changamoto pevu kwa vijana wa kizazi kipya! Kila mtoto anayezaliwa duniani ni Kristo mwenyewe anayewaangalia, anayekuja duniani kama mtoto asiyeweza kujilinda peke yake. Watoto ni matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Ushiriki mkamilifu wa watu wote wa Mungu katika usawa ni kigezo muhimu sana katika mchakato wa kulinda na kudumisha amani duniani. Kanisa limeendelea kutoa mchango mkubwa katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani. Amani inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kawaida, kwa kuchagua maneno yanayotumika, kwani yanaweza kusaidia kujenga au kubomoa amani. Maneno yanayotumika yawe ni yale yanayopenda ukweli na kuhudumia amani katika medani mbali mbali za maisha ya watu. Haya ndiyo maneno yanayopaswa kuwa ni sehemu ya sala ya waamini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maadhimisho ya Siku ya 101 ya Waamini Wakatoliki nchini Ujerumani inakuwa ni sherehe ya imani na alama ya amani kwa watu walioko karibu na wale walioko mbali.

Kipindi kati ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni hadi Sherehe ya Pentekoste ni muda wa Novena kwa ajili ya kumwomba Roho Mtakatifu, ili aweze kuwakirimia waamini mapaji na karama zake. Bikira Maria Mama wa Kanisa alishikamana na Mitume wa Yesu kusubiri ujio wa Roho Mtakatifu, awasaidie na kuwasindikiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaotafuta amani. Waendelee kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.