Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Papa Francisko awataka wananchi wa Italia kupambana na mafia!

Papa Francisko anaitaka familia ya Mungu nchini Italia kutubu na kumwongokea Mungu kama njia ya kupambana na vitendo vya mafia. - ANSA

11/05/2018 09:34

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Jimbo kuu la Agrigento lililoko kusini mwa Italia na kutumia fursa hiyo, kuwataka wale wote wanaojihusisha na vikundi vya kigaidi vya Mafia kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anapenda kuwatia shime viongozi wa Kanisa na waamini katika ujumla wao, hasa Kusini mwa Italia, kutembea kwa pamoja huku wakiwa wameshikamana.

Wajitahidi kufuata dira na mwongozo wa maisha uliotolewa na Mwenyeheri Don Pino Puglisi aliyeuwawa kikatili na kikundi cha Mafia kutokana na msimamo wake thabiti wa kupinga vitendo vilivyokuwa vinafanywa na kikundi hiki kwa kudhalilisha utu na heshima ya binadamu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, matendo maovu yanashughulikiwa kikamilifu kwa kumwilisha kila siku tunu msingi za maisha ya Kikristo na kiutu zinazofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu, ujasiri na ushupavu wa Kiinjili, kwa kuendelea kujikita katika malezi na majiundo makini ya vijana wa kizazi kipya, ili wasitumbukie katika janga hili la maisha na hivyo kupokwa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi!

Wakati huo huo, Askofu mkuu Salvatore Gristina wa Jimbo kuu la Catania katika mahubiri yake kwa ajili ya kumbu kumbu ya miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Agrigento, ameitaka kwa mara nyingine tena, familia ya Mungu nchini Italia kuwa ni shuhuda na chombo cha kutangaza Fumbo la Pasaka linalopyaisha maisha yao, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Ilikuwa ni tarehe 9 Mei 1993, Mtakatifu Yohane Paulo II alipoadhimisha Ibada ya Misa Takatifu huko Agrigento na kuwataka wale wote waliokuwa wanajihusisha na vitendo vya kigaidi vinavyoendeshwa na Mafia, kutubu na kumwongokea Mungu.

Mtakatifu Yohane Paulo II aliwataka wasiwe na wasi wasi wala hofu ya kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, ili aweze kuwagusa na kuwapyaisha tena. Aliwataka kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka, unaobubujika kutoka kwa Kristo Mkombozi wa dunia. Mwamini anayemfungulia Kristo Yesu maisha yake, anaimarisha imani, anafukuza giza la ubinafsi na uchoyo; anakuza na kudumisha Injili ya upendo na mshikamano, ili kung’oa ndago za chuki, uhasama na hali ya kutaka kulipiza kisasi; imani inamwezesha mwamini kukuza umoja na udugu na hivyo kuondokana na sera za kibaguzi zinazotaka kuwagawa watu na hatimaye, kuwasambaratisha kwa ajili ya mafao ya watu wachache ndani ya jamii.

Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaambata kanuni maadili na utu wema; kwa kuendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Vitendo vya kigaidi vya mafia vinapandikiza utamaduni wa chuki, uhasama na kifo. Ndiyo maana Mtakatifu Yohane Paulo II akaitaka familia ya Mungu nchini Italia kujikita katika Injili ya amani, kwa kutubu na kumwongokea Mungu; ili kuachana na utamaduni wa kifo ili kuambata utawala wa sheria unaosimikwa katika haki, usawa na mshikamano.

Ni wajibu na dhamana ya familia ya Mungu nchini Italia kupyaisha maisha yao mintarafu tunu msingi za maisha ya Kikristo. Vitendo vyote vinavyofanywa na mafia ni dhambi dhidi ya Mungu na jirani na kwamba, ni kinyume kabisa cha Injili ya Kristo. Maaskofu wanawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha Injili ya amani na maridhiano; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kwamba, Maaskofu wapo kwa jili ya huduma kwa watu wa Mungu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika Barua yake kama Kumbu kumbu ya Miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II atembelee huko Agrigento inayoongozwa na kauli mbiu “Tubuni”, pamoja na mambo mengine msingi, Maaskofu wanawataka waamini kusimama kidete kupambana na vitendo vya mafia bila kuvifumbia macho. Kujishakamanisha na katekesi endelevu, kwa kushiriki pia katika vyama mbali mbali vya kitume ili kukita maisha yao katika tunu msingi za Kiinjili ili kudumisha haki, amani, huruma na mapendo.

Waamini wajisikie kuwa ni sehemu muhimu sana ya Kanisa na kwamba, waendelee kuboresha maisha yao kwa njia ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na Ibada mbali mbali. Watambue kwamba, vitendo vya mafia ni dhambi inayofumbata uchu wa mali na madaraka kwa ajili ya mafao ya watu wachache ndani ya jamii. Waamini katika hija ya maisha yao ya kila siku, waendelee kutubu na kumwongokea Mungu, ili waweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Kimsingi barua hii inajikita zaidi katika mwaliko wa Mtakatifu Yohane Paulo II wa kutubu na kumwongokea Mungu; ujumbe wa kinabii, unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu; waamini waendelee kutambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa; wawe mstari wa mbele kuwahudumia na kuwasaidia waathirika wa vitendo vya mafia na kwamba, maaskofu wanasali, ili kuomba huruma ya Mungu, msamaha, mwanga na ujasiri wa kuanza kuandika kurasa mpya za imani na matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

11/05/2018 09:34