2018-05-11 16:11:00

Leo mnatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!


Utangulizi: “Basi Bwana Yesu, baada ya kusema nao akachukuliwa mbinguni, akaketi mkono wa kuume wa Mungu” karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Neno la Mungu leo ikiwa ni Sherehe ya Kupaa Bwana. Siku arobaini baada ya kufufuka Yesu anapaa mbinguni kwenda kwa Baba yake ambaye ni Baba yetu. Anakwenda ili tukae tukiamini kwamba sisi tulio viungo vyake ametutangulia huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shina letu ili pale alipo sisi nasi tupate kuwepo. Tukiwa tunangojea kuungana naye anatuachia utume wa kuutekeleza na kuuendeleza, utume aliokuja kuufanya “kuutangazia ulimwengu mzima habari njema ya wokovu”.

Masomo kwa ufupi: Somo la Kwanza (Mdo. 1:1-11) linatoa kwa muhtasari mambo ambayo Yesu aliyafanya katika kipindi cha siku arobaini baada ya kufufuka kwake. Na kwa vile alikwisha waweka tayari mitume ili waendeleze kazi yake ya ukombozi hadi atakaporudi.  Kipindi hiki cha siku arobaini kinakuwa pia ni kipindi cha kuwapa maelekezo kabla ya kuanza rasmi utume wao. Anakazia mafundisho juu ya ufalme wa Mungu, anawaambia wasiondoke Yerusalemu bali wangojee ujio wa Roho Mtakatifu na kisha waanze utume wao wa kumshuhudia akisema “nanyi mtakuwa mashahidi wangu”. Na hapa tunaona mambo matatu: ufalme wa Mungu, kungojea ujio wa Roho Mtakatifu na kuwa mashahidi wa Kristo.

Ufalme wa Mungu ndio kitovu cha mafundisho ya Yesu kadiri ya Mwinjili Luka ambaye ndiye pia ndiye mwandishi wa kitabu cha Matendo ya Mitume. Kumbe Yesu kuzungumza na wanafunzi wake juu ya ufalme wa Mungu ni kuwapitisha tena katika mafundisho yake yote kwa maana tangu sasa ni wao wanakuwa waalimu. Kungojea ujio wa Roho Mtakatifu ni kungojea nguvu kutoka juu itakayowawezesha kutekeleza utume wao. Ndiye Roho Mtakatifu, Bwana na Mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana ndiye anayewezesha utume wote wa Kanisa kuendelea.  Kusubiri ujio wa Roho Mtakatifu ni pia kusubiri wakati wa Bwana. Na wakati wa Bwana husubiriwa si kwa kukaa tu bali kwa sala na tafakari, na ndivyo walivofanya mitume.

Ni hapa ilipozaliwa novena ya kwanza, Novena ya Roho Mtakatifu ambayo hadi leo Kanisa linasali kuelekea sherehe ya Pentekoste. Na mwisho tunaona Yesu anawaambia watakuwa mashahidi wake. Ni mashahidi kuwa hayo wanayofundisha kuhusu Kristo sio habari za kusadikika bali wao wenyewe wameshuhudia. Wameshuhudia mateso na kifo chake, wamemwona alipofufuka na sasa wamemwona akipaa kurudi kwa Baba.

Somo la pili (Ef. 4:1-13) Mtume Paulo anaiandikia jumuiya kuipa maonyo ya kimaadili na kuwaasa kulinda umoja kati yao. Anataja fadhila za unyenyekevu, upole, uvumilivu na kuchukuliana katika upendo. Na kuhusu umoja anaonesha kuwa jumuiya  inaalikwa kuutafuta na kuuishi umoja kwa kufuata fumbo la umoja katika Mungu mwenyewe. Yeye ni mmoja, amewapa Roho mmoja, amewaita katika tumaini moja kwa njia ya imani moja na ubatizo mmoja walioupokea. Kisha anataja huduma mbalimbali ambazo watu huitwa kutekeleza katika jumuiya: mitume, manabii, wainjilisti, wachungaji na waalimu. Paulo anazitaja hizo kwa sababu inaonekana zilikuwa mojawapo ya sababu za kuleta utengano katika jumuiya.

Wapo walioona nafasi zao zinawafanya kuwa bora zaidi kuliko wengine wakiwadharau ambao hawana nafasi hizo. Anawaasa kutambua kuwa nafasi zote hizo zinatoka kwa Kristo kwa lengo la kuujenga mwili wake ambao ni kanisa jumuiya ya waamini. Ni nafasi za huduma kwa ajili ya jumuiya na kila aliyepewa amepewa kwa ukamilifu wake. Anasema “kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo”. Hivyo hakuna sababu ya kujikweza wala kuwadharau wengine kwa sababu ya vipawa vitokavyo kwa Kristo.

Injili (Mk. 16:15-20) inarejea pia kama Somo la kwanza matokeo ya Yesu na wanafunzi wake baada ya ufufuko na kuelezea tukio la kupaa kwake kurudi kwa Baba. Hapa pia kabla ya kupaa, Yesu anawaachia wanafunzi wake agizo, kwenda ulimwenguni kote kuihubiri Injili kwa kila kiumbe. Anawaagiza pia kuwabatiza wote wanaoamini katika Injili na kwamba wanaoamini na kubatizwa wataokoka ilhali wale wasioamini watahukumiwa. Anawahakikishia pia kuwa utume wao utaambatana na ishara mbalimbali: watatoa pepo, watasema kwa lugha mpya, watashika nyoka, hawatadhuriwa na pia wataponya wagonjwa.

Tunaona katika somo hili kuwa agizo walilopewa mitume ndio agizo ambalo hata leo Kanisa linalichukua kama utume wake nambari moja, ndiyo misioni ya Kanisa “kwenda na kuhubiri Injili kwa kila kiumbe” mpaka hapo atakaporudi. Ishara Yesu anazozitaja, ambazo kwa kweli ni miujiza, zinadhihirika wazi pale Kanisa linapoadhimisha sakramenti. Kwa njia ya maadhimisho ya sakramenti Kanisa linatekeleza yale ambayo kibinadamu hayayamkiniki. Hata zinapokuwa nje ya sakramenti bado lengo lake ni kukuza imani na kuwaleta watu kwenye sakramenti na katu sio kuonesha umahiri wa mtendaji, umaarufu wake au kitu kingine chochote nje ya imani.

Tafakari fupi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika sherehe ya leo, sherehe ya kupaa Bwana tunatafakari fundisho ambalo ni mojawapo ya mafundisho makuu ya imani yetu. Ni mojawapo ya kiri ya imani iliyo kwenye Kanuni ya Imani Katoliki kwamba “(Yesu).. alipaa mbinguni na amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi”. Tendo la Yesu kupaa mbinguni ni tendo lililounganika na ufufuko wake na tena linaukamilisha ufufuko huo kama kilele chake kwa sababu Yesu alipofufuka hakufufuka kama walivyofufuliwa wengine, mfano Lazaro, ili waweze kufa tena. Yesu alifufuka na mwili usioweza kufa tena na hivi akapaa mbinguni kwenda kuushiriki utukufu ule wa Baba, ndio kwenda kukaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi.

Kumbe Kupaa mbinguni ni tendo pia linalomtukuza Yesu mwenyewe baada ya kujishusha, kujinyenyekeza na kutwaa mwili wa binadamu ili aweze kumkomboa mwanadamu na ulimwengu mzima, sasa kisha kumaliza utume huo anarejeshewa utukufu aliokuwa nao kabla hata ya kuwekwa misingi ya ulimwengu kama asemavyo Mtume Paulo. Ndivyo pia alivyokuwa akiwaambia wanafunzi wake “kila ajishushaye atakwezwa na kila ajikwezaye atashushwa” akiwahimiza kuchukua unyenyekevu katika kutekeleza huduma wanazokabidhiwa.

Pamoja na kiri hiyo ya imani, liturujia ya leo inaleta kwetu mambo mawili ya kutafakari katika sherehe hii. Jambo la kwanza ni lile ambalo limeonekana katika masomo ya leo, Kupaa Bwana kumeliachia Kanisa agizo na utume wa kufanya. Kuhubiri injili kwa kila kiumbe kote ulimwenguni. Liwe ushuhuda kwa Kristo. Hili ni agizo kwa wanakanisa wote tunaounganishwa na ubatizo mmoja, tunaoshiriki tumaini moja kwa njia ya karama na nafasi mbalimbali alizotujalia Mungu. Sote tumeachiwa wajibu wa kutekeleza.

Jambo la pili ni maneno anayosali kuhani katika sala ya utangulizi (Prefasio) siku ya leo kuwa “amepaa si kwa sababu ya kutuacha sisi wanyonge bali ili tukae tukiamini kwamba sisi tulio viungo vyake ametutangulia huko aliko Yeye aliye kichwa chetu na shina letu” Amekwenda kutuandalia makao ili pale alipo sisi nasi tupate kuwepo. Ni sala inayotupa tumaini la kushiriki naye heri ya uwinguni na hapo hapo ikitualika tuishi hapa duniani tukijua kuwa lengo letu ni uwinguni. Hivyo tuyaelekeze daima macho yetu huko, na kuishi maisha yetu hapa duniani tukijua kuwa maisha yetu halisi yako huko alikotutangulia Bwana Wetu Yesu Kristo.

Padre William Bahitwa

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.