Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Askofu mkuu Rastilav akutana na kuzungumza na Papa Francisko!

Askofu mkuu Rastislav akazia umuhimu wa Maandiko Matakatifu kama njia ya kumtambua Kristo Yesu, Mapokeo ya Kanisa na Utamadunisho.

11/05/2018 15:03

Askofu mkuu Rastislav wa Jimbo kuu Presov, Kiongozi mkuu wa Kanisa la Kiorthodox wa Nchi ya Czech na Slovakia katika hotuba yake kwa Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 11 Mei 2018 amekazia umuhimu wa kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu; hija inayowakutanisha wafuasi wa Kristo pamoja na ushuhuda unaofumbatwa katika Mapokeo ya Kanisa. Wanafunzi wa Emau waliweza kumtambua Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa njia ya kuumega mkate. Kumbe, tafakari ya Maandiko Matakatifu iwe ni chemchemi ya matumaini mapya, ujasiri na upya wa maisha kwa kuaminiana zaidi. Hii ni changamoto ya kuendeleza Jumuiya za waamini kadiri ya Mapokeo ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox.

Askofu mkuu Rastislav amekazia umuhimu wa wafuasi wa Kristo kuendelea kujikita katika hija inayofumbata upendo kwa kutembeleana kama mashuhuda wa Kristo Mfufuka na kama walivyofanya Watakatifu Cyril na Method, kukutana na hatimaye kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Umoja na mshikamano miongoni mwa Wakristo utawasaidia kukabiliana na changamoto mamboleo kama vile: mauaji, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia.

Kuna mamilioni ya Wakristo wanaolazimika kuzikimbia nchi zao, wanaoendelea kuteseka kutokana na umaskini, magonjwa na utapiamlo wa kutisha, kiasi kwamba, waamini hawa wamepoteza mizizi na imani yao ya Kikristo. Changamoto mamboleo ziwasaidie kuungana ili kuweza kumshuhudia Kristo katika umoja na mshikamano wao kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha. Wakristo washikamane kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, haki na amani duniani, wakianzia kwanza katika maisha yao wenyewe! Kwa njia hii wataweza kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu wakiwa na furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Wakristo waendelee kudumisha Mapokeo ya Kanisa yanayopyaishwa kwa kutumia lugha inayoeleweka na watu wa nyakati hizi. Kwa maneno mengine, wanapaswa kujikita katika mchakato wa utamadunisho, ili Injili ya Kristo iweze kufahamika kwa watu wengi zaidi na Kristo Mfufuka, Bwana na Mwalimu awasaidie kuondokana na woga wa kukutana na ulimwengu mpya pamoja na watu wake. Mwishoni, Askofu mkuu Rastislav amepongeza juhudi zinazofanywa na Tume Mchanganyiko ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa haya mawili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

11/05/2018 15:03