2018-05-10 13:42:00

Jumuiya ya Nomadelfia ni maabara ya imani yanayosimikwa katika Injili


Bwana Francesco Matterazzo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Nomadelfia katika salamu zake kwa Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, 10 Mei 2018, amemshukuru kwa kumtambua na kumuenzi Don Zeno Saltini ambaye, aliamua kuivalia njuga changamoto ya watoto maskini, yatima na wale waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Katika maisha yake, akabahatika kuwakusanya na kuwatunza watoto 5000, huku akisaidiwa na “Wanawake wenye wito”, wanandoa pamoja na mapadre kadhaa.

Don Zeno alijiaminisha kwa neema na tunza ya Mwenyezi Mungu katika maisha yake, akathubutu kutumia utajiri kidogo aliokuwa nao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na matumaini; kwa kutaka wote wawe wamoja kama anavyosisitizia Kristo Yesu katika Sala yake ya Kikuhani. Akavunjilia mbali kuta za utengano na kuwaunganisha watu ili wote waweze kujisikia kuwa ni ndugu na wamoja katika Kristo Yesu, huku wakijikita katika haki kama sheria msingi kwa wafuasi wote wa Kristo.

Don Zeno ni kiongozi aliyethubutu, kuvumbua tena amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa la mwanzo, kwa kutaka kumfuasa Kristo Yesu, katika Njia za Heri za Mlimani, muhtasari wa mafundisho yake makuu. Injili ya Kristo, ikawa ni dira na mwongozo wa Jumuiya ya Nomadelfia. Daima aliwakumbusha wanachama wake kwamba, wameteuliwa na Mwenyezi Mungu ili kuanzisha maabara ya imani inayomwilishwa katika maisha ya watu kwa kujenga utamaduni wa Injili unaowafumbata wananchi wote wa Nomadelfia.

Licha ya mapungufu na udhaifu wao, lakini wamekuwa ni ndugu na mashuhuda upendo wa Mungu kwa waja wake. Don Zeno ambaye hapo awali alikuwa ni mwamini mlei, aliamua kujisadaka zaidi kwa kujikita katika malezi na majiundo ya kipadre, kwa neema ya Mungu na msaada wa Padre Francesco D’Alfonso, SJ., akabahatika kupewa Daraja ya Upadre. Jumuiya ya Nomadelfia, imemwomba Baba Mtakatifu Francisko kuisindikiza Jumuiya hii inayojikita katika mageuzi makubwa, ili iweze kuendelea kuwa aminifu katika wito wake na hatimaye, iweze kupandikiza udugu kati ya familia sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.