2018-05-10 14:31:00

Jumuiya ya Loppiano ni shule ya majadiliano ya kidini na kiekumene!


Chama cha Kitume cha Wafokolari kunako mwaka 2014 kimeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake, aliwataka Wafokolari kuwa na imani, ujasiri na ufahamu, ndoto ambayo chama hiki kimekuwa kikiitekeleza katika maisha na utume wake kama kielelezo cha furaha ya Injili. Mji wa Loppiano unayo mifano yake mingine katika nchi 25 katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii na kitamaduni.

Mtumishi wa Mungu Chiara Lubich alitamani sana kujenga maabara ya watu kuishi kwa amani, umoja na ushuhuda wa jamii inayoshikamana na kusaidiana kwa hali na mali kwa kupata chimbuko lake kutoka katika tunu msingi za Kiinjili. Itakumbukwa kwamba, Makao makuu ya Chama cha Kitume cha Wafokolari yako Rocca di Papa ambako kuna watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaishi na kufanya kazi hapo. Leo hii, mji wa Loppiano una jumla ya watu 850 kutoka katika nchi 65, ambao wamempokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko alipowatembelea, Alhamisi, tarehe 10 Mei 2018.

Mama Maria Voce, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu kuwatembelea na kuzungumza pamoja nao, amesema, Jumuiya ya Loppiano inaundwa na familia zinazoishi kama katika “Shule ya Loreto” yaani maisha ya “Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu”; kuna wakleri, majandokasisi na watawa; wapo vijana wa kizazi kipya na wale wanaojitolea kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Kwa muda wa miaka 10 sasa, Loppiano ni Chuo Kikuu kilichoidhinishwa na Vatican kama msingi wa kutafuta ukweli ili kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kuunganisha mawazo na uhalisia wa maisha. Ni mahali pa kukuza na kudumisha uchumi shikamanishi, kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika haki na usawa.

Mama Maria Voce anakaza kusema, kuna Chama cha Ushirika cha Loppiano kilichoanzishwa kunako mwaka 1973 ili kukuza na kuboresha sekta ya kilimo; kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kuzijengea uchumi familia ambazo zimeacha yote kwa ajili ya upendo kwa Mungu na jirani. Luppiano pia ni mahali panaposhuhudia sana ana kwamba, watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamekuwa wakitembelea ili kujionea wenyewe matendo makuu ya Mungu kwa binadamu.

Loppiano ni mji ambao unamejengwa na kujiaminisha katika Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu, ndiyo maana unaitwa “Mariapoli”. Bikira Maria anawaonesha programu ya maisha na mambo wanayopaswa kutekeleza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wagonjwa; ili kuwashirikisha furaha ya Injili. Wafokolari wanataka kuhakikisha kwamba, Sheria ya Upendo, amani na utulivu inakuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wao kama njia ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, tayari kushiriki kikamilifu katika kuandika ukurasa mpya wa historia ya ulimwengu unaofumbatwa katika umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.