Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Katekesi siku ya Jumatano

Papa Francisko: Ubatizo ni kuzamishwa katika Fumbo la Pasaka!

Ubatizo unamaanisha na kudhihirisha mauti kwa dhambi na kuingia katika uzima wa Fumbo la Utatu Mtakatifu.

09/05/2018 14:32

Baada ya Ishara ya Msalaba, Tangazo la Neno la Mungu na Ibada ya Kupunguza pepo inayomwezesha mwamini kukiri imani ya Kanisa, ambamo ataaminishwa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na baada ya kubariki ya Maji ya Ubatizo kisha yanafuata madhehebu ya lazima ya Sakramenti ya Ubatizo. Mababa wa Kanisa wanasema Ubatizo unamaanisha na kudhihirisha mauti kwa dhambi na kuingia katika uzima wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, kwa kugeuzwa kwa njia ya Fumbo la Pasaka ya Kristo! Kubatizwa maana yake ni “kuzamishwa”.

Mtume Paulo anasema, wale wote waliobatizwa katika Kristo Yesu, wamebatizwa katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo Wakristo waenende katika upya wa uzima! Ubatizo unawafungulia waamini maisha ya Kristo mfufuka na wala si kwa ajili ya mambo ya kidunia! Kumbe, waamini wanapaswa kuishi na kutenda kadiri ya mapenzi ya Kristo, Bwana na Mwalimu! Hii ni sehemu ya Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoitoa, Jumatano, tarehe 9 Mei 2018 kama sehemu ya mwendelezo wa Katekesi zake kuhusu Maisha ya Kikristo, na kwa namna ya pekee, Sakramenti ya Ubatizo.

Kisima cha Ubatizo ni mahali ambapo waamini wanashiriki Pasaka pamoja na Kristo Yesu! Yaani, wanauvua utu wa kale, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya, ili kufanywa upya katika roho na nia njema. Mtakatifu Cyril wa Yerusalemu anafafanua sehemu hii ya Ibada ya Ubatizo kwa kusema kwamba, kwa njia ya Ubatizo watu wanakufa na kuzaliwa upya katika maji na Roho Mtakatifu. Kwa njia hii, utu wa zamani ambao umeharibiwa kutokana na dhambi unazikwa katika Kisima cha Ubatizo ambacho kinaweza kufananishwa na: “Kaburi” na “Tumbo la Mama mzazi”.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ndiyo mambo mazito yanayofumbatwa katika Ibada ya Ubatizo. Kwa njia ya Kisima cha Ubatizo, Mama Kanisa anabahatika kupata watoto wapya wanaopata pumzi ya Mungu na kwamba, wale waliobatizwa wanakuwa na tumaini la Ufalme wa Mungu. Kumbe, waamini wanazaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu ndani ya Kanisa ambalo linakuwa ni Mama na Mwalimu. Watoto waliozaliwa kwa Ubatizo wanakuwa ni Watoto wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu. Ndiyo maana mara baada ya Kristo Yesu kubatizwa Mtoni Yordani mara sauti kutoka mbinguni ikasema “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye” (Mt. 3:17).

Wale waliozaliwa katika Ubatizo, wanadumu katika neema hiyo kwani wakiwa wameingizwa katika Kristo kwa Ubatizo, mbatizwa amefananishwa na Kristo. Ubatizo unamtia mtu alama ya mhuri wa kiroho usiofutika wa kuwa ni mali ya Kristo. Mhuri huu hauwezi kufutwa na dhambi yoyote, ingawa dhambi huuzuia Ubatizo kuzaa matunda ya wokovu. Ubatizo hutolewa mara moja kwa daima, hauwezi kurudiwa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata katika dhambi zao, bado wabatizwa wanaendelea kuwa ni watoto wateule wa Mungu, anayewaita kutubu na kumwongokea. Kwa njia ya Ubatizo wanafananishwa na Mwana wa Mungu, mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu zake. Roho Mtakatifu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo: anatakasa, anatakatifuza na kumhesabia mtu haki, ili kwa pamoja waweze kujenga Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kwa kupakwa Krisma Takatifu, mwamini anakuwa Mkristo, yaani “Mpakwa” yaani anapewa: alama: kuhani, nabii na mfalme katika jumuiya ya watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wito wa Kikristo umezama katika kuishi huku wakiwa wameungana na Kristo katika Kanisa Takatifu, kwa kuwekwa wakfu wanatumwa kuyatakatifuza malimwengu. Kimsingi, familia ya Mungu inakuwa ni taifa la: Kikuhani, Kinabii na Kifalme, kwa kuwajibika katika utume na huduma, ili kumtolea Mwenyezi Mungu sadaka inayopendeza, kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayosimikwa katika imani na mapendo kama alivyofanya Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

09/05/2018 14:32