Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Nyaraka

Papa Francisko: Habari za kughushi na uandishi wa habari wa amani!

Papa Francisko anawataka waandishi wa habari kuachana na habari za kughushi na kuanza kujikita na uandishi wa habari wa amani ili kudumisha ukweli, haki na maridhiano kati ya watu! - ANSA

09/05/2018 08:57

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni, inayoadhimishwa katika Sherehe ya Kupaa Bwana mbinguni ambayo kwa mwaka huu ni hapo tarehe 13 Mei 2018 unaongozwa na kauli mbiu “... Ukweli utawaweka huru: Habari za kughushi na Uandishi wa Habari wa Amani.”  Baba Mtakatifu katika ujumbe huu, anawataka wadau mbali mbali katika tasnia ya mawasiliano ya jamii, kuwa ni vyombo vya huduma ya ukweli. Anafafanua maana ya habari za kughushi, jinsi ya kuzitambua, umuhimu wa kuambata na kudumisha ukweli unaowaweka huru na kwamba, amani ni habari ya kweli!

Baba Mtakatifu anasema, binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kiasi cha kuwa na uwezo wa kushirikisha kile kilicho: kweli, chema na kizuri ili kuweza kuunda kumbu kumbu ya kihistoria pamoja na kuelewa matukio mbali mbali yanayomzunguka mwanadamu. Lakini kutokana na ubinafsi, mwanadamu amejikuta akiharibu uwezo wake wa kuwasiliana na wengine, hali ambayo inapata chimbuko lake hata kutoka katika Maandiko Matakatifu. Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, leo hii mwanadamu anakumbana na bahari ya habari za kughushi, dhana ambayo imetendewa kazi hata na Mapapa waliotangulia ambao wamewataka wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kusimama kidete kupinga habari za kughushi, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na weledi wa uandishi wa habari kwa wanahabari wenyewe kuwajibika kikamilifu katika kutangaza na kushuhudia ukweli! Habari za kughushi anasema Baba Mtakatifu Francisko, ni habari tenge inayojikita katika takwimu zilizochakachuliwa au hata zile ambazo hazipo kabisa, ili kumwadaa msomaji.

Lengo ni kutoa ushawishi katika maamuzi ya kisiasa ili kulinda na kudumisha zaidi mafao ya kiuchumi. Kwa haraka haraka habari za kughushi zinaonekana kuvutia sana na kugusa hisia za watu wengi kwani zinajikita katika maamuzi mbele yanayotolewa na jamii kutokana na chuki, hasira na hali ya kuchanganyikiwa. Habari za kughushi husambaa kwa haraka sana kama moto wa mabua, kiasi hata uwezo wa vyombo husika kukanusha, vinakuwa haviwezi kufua dafu!

Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya watu hujikuta wakiwa kwenye mstari wa mbele kutaka kuunga mkono hoja inayotolewa bila hata kufahamu undani wake. Hizi ni habari potofu, zisizokuwa na chembe ya ukweli ndani yake, zisizoweza kutoa changamoto dhidi ya maamuzi mbele wala kujenga majadiliano katika ukweli na uwazi. Matokeo yake ni kuharibu sifa za watu wengine kwa kuwachora kama adui wanaopaswa kushughulikiwa kama “Mbwa koko” hali ambayo inakuza kinzani ndani ya jamii. Habari za kughushi ni dalili za kukosekana kwa maridhiano katika jamii, hali inayopelekea kusambaa kwa jeuri, chuki na uhasama kati ya watu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ili kuweza kutambua habari za kughushi kuna haja ya kujenga na kukuza mfumo wa elimu utakaowawezesha watu kutafsiri na kupata habari za uhakika zinazotolewa na vyombo vya habari pamoja na kuwajengea uwezo wa kufichua habari za kughushi. Pili, kuna haja ya kukuza na kudumisha utawala wa sheria ili kuhakikisha kwamba, wale wote wanaohusika na habari za kughushi wanashughulikiwa kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu zilizopo. Tatu, Makampuni ya mawasiliano ya jamii, yasaidie kuweka vyombo vitakavyofichua habari za kughusi, hali ambayo inahitaji mchakato wa mang’amuzi ya kina, ili ukweli uweze kung’ara katika maisha ya watu na hivyo kuondokana na dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu na jirani.

Ibilisi, shetani ni baba wa tamaa na watu wengi wameanguka katika mtego wake na huo ukawa ni mwanzo wa majanga katika maisha ya mwanadamu. Ibilisi anapenda kuung’arisha uwongo kwa kuwapaka watu “mafuta kwa mgongo wa chupa” na hivyo, uwongo unakuwa ni habari inayotamanika na kupendeza machoni pa watu, lakini ndani mwake kumefichama hatari na si rahisi sana kuweza kubomolewa kwani habari za kughushi zinakita mizizi yake katika tamaa ya binadamu inayofumbatwa katika mchakato wa kutafuta nguvu za kiuchumi na kuharibu uhuru wa ndani. Ndiyo maana kuna haja kupambanua, kutathimini na kufahamu matamanio halali ya mwanadamu ili kuambata ukweli wa mambo.

Ukweli utawaweka huru ndiyo changamoto kubwa inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake katika maadhimisho ya Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni. Watu wanapaswa kutambua, kusimamia na kuupenda ukweli, ili uwongo uweze kujitenga. Ukweli ni sehemu ya maisha ya mwanadamu na Kristo Yesu anakaza kusema kwamba “Yeye ni ukweli, njia na uzima” na kwamba, mtu anayegundua na kuambata ukweli katika maisha yake, atakuwa huru kweli kweli. Watu wajifunze kupambanua ukweli ili kujenga umoja na mshikamano; utamaduni wa kusikilizana katika ukweli na uwazi. Kamwe watu wasichoke kutafuta na kuambata ukweli ilikujenga umoja na ukomavu katika tafakari, hatimaye kudumisha majadiliano yanayozaa matunda yanayokusudiwa yaani haki, amani, upendo na mshikamano.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, amani ndiyo habari ya kweli inayomlenga mtu mzima ili kumjengea uwezo wa kusikiliza, kujadiliana katika ukweli na uwazi, kwa kuvutwa na: ukweli, wema na uzuri ili hatimaye, kuwajibika barabara. Wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii wanao wajibu na utume mzito wa kulinda ukweli wa habari kwa kutambua kwamba, mlengwa mkuu ni binadamu. Habari inalenga kuwaunda watu wengine katika jamii, kugusa maisha yao ili kudumisha wema na uaminifu unaofungua njia ya umoja na amani.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anawataka waandishi wa habari kujikita katika uandishi wa habari wa amani kwa kuondokana na habari za kughusi zinazochezea vionjo na hisia za watu kama alivyokuwa nyoka, Ibilisi katika Agano la Kale. Uwe ni uandishi wa habari kwa ajili pamoja na watu, yaani uandishi wa habari kwa ajili ya huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu; ili kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti. Waandishi wa habari wasijikite tu kwa “Breaking News”, bali wawe na ujasiri, ari na moyo wa kupembua kwa kina na mapana sababu msingi zinazopelekea vita, kinzani na migogoro ya kijamii, ili kujenga uelewa mpana zaidi utakaosaidia mchakato wa suluhu na amani ya kudumu. Uandishi wa habari anaoutaka Baba Mtakatifu Francisko ni ule usiokuwa wa vita ya maneno na makelele kibao! Mwishoni, anataka waandishi wa Habari wawe ni vyombo na mashuhuda wa mchakato wa maridhiano, haki na amani duniani akiwataka kurejea katika Sala ya Mtakatifu Francisko kwa Assisi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

09/05/2018 08:57