2018-05-09 09:30:00

Maisha ya kitawa ndani ya Kanisa: Udugu, Utume, Karama na Sinodi


Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kuanzia tarehe 3-6 Mei 2018 limeadhimisha kongamano la kimataifa kwa ajili ya maisha ya kitawa kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Antonianum kilichoko mjini Roma. Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na wajumbe hawa Ijumaa, tarehe 4 Mei 2018 amekazia umuhimu wa maisha ya sala, ufukara na uvumilivu unaopaswa kuwa ni dira na mwelekeo wa kupambana na changamoto, matatizo na fursa mbali mbali katika maisha ya kitawa na kazi za kitume.

Kongamano hili limekuwa likiongozwa na kauli mbiu “Consecratio et consecration per evangelica consiglia” yaani “Kuwekwa wakfu kwa ajili ya mashauri ya Kiinjili.” Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume linasema, kuna njia mbali mbali za kumfuasa Kristo Yesu; kuna mambo ambayo yanalandana na kuna mambo yanatofautisha mtindo wa maisha ya kuwekwa wakfu; yote haya yanategemeana na kukamilishana na wala hakuna mtindo wa maisha ya kitawa unaoweza kujidai kuwa ni wa maana kuliko mwingine, jambo la msingi ni kila mtawa kubaki katika mfumo wa maisha ya kitawa ambayo Mwenyezi Mungu amemwitia, ili kushiriki maisha na utume wa Kanisa.

Sr. Carmen Ros Nortes, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume anasema, maisha ya kuwekwa wakfu hayawezi kufafanuliwa tu kwa kuishi nadhiri, yaani: Ufukara, Utii na Useja au Usafi kamili. Kuna mambo msingi ambayo yanapaswa pia kuzingatiwa katika maisha ya kuwekwa wakfu. Mambo haya ni pamoja na: Maisha ya kidugu, Utume, Maisha ya kiroho, Unabii. Miito yote hii inapata chimbuko lake kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo inayowachangnamotisha waakristo wote kuchuchumilia na kuambata mchakato wa utakatifu wa maisha.

Kwa upande wake Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume amekazia dhana kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye anayemwita mja wake, anamweka wakfu na kumtuma kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Wakristo wote wanatumwa kushiriki maisha na utume wa Kanisa, lakini kuna baadhi ya watu ambao wamedhaminishwa utume maalum. Kitendo cha kuwekwa wakfu, tayari ni sehemu ya mchakato wa utume, changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, mambo msingi kama vile: udugu, utume na karama yanazingatiwa ili kutoa mwelekeo sahihi kwa kila mtawa katika maisha na utume wake ndani ya Kanisa.

Padre Josè Cristo Rey Garcìa Paredes, katika tafakari yake, amejikita zaidi katika karama ya maisha ya kitawa mintarafu mwelekeo sahihi wa ufahamu wa Kanisa na maisha ya Kisakramenti, ili kukuza na kudumisha uzuri wa upendo wa Mungu kwa waja wake. Mkazo zaidi ni uelewa sahihi wa Taalimungu ya Agano, Taalimungu ya Sakramenti za Kanisa, Taalimungu ya Roho Mtakatifu pamoja na mambo ya nyakati. Haya ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana katika maisha na utume wa kitawa.

Hili ni Agano katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linalomwilishwa katika maisha ya mtawa binafasi na hatimaye katika jumuiya na shirika zima, changamoto na mwaliko wa kuwa ni mashuhuda, wamisionari na manabii wanaotumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati zote. Maisha ya Kisakramenti kwa kila mtawa ni chachu ya utakatifu inayopaswa kuvaliwa njuga na wote kwa kutambua kwamba, kwa njia ya nadhiri, wanawekwa wakfu na Roho Mtakatifu ili kumshuhudia Kristo Yesu kwa namna ya pekee kabisa, tayari kujisadaka katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu bila ya kujibakiza sanjari na kujiandaa kwa maisha ya uzima wa milele!

Kama sehemu ya majumuisho ya kongamano hili ambalo limewashirikisha watawa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Kardinali Josè Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, amekazia kwa namna ya pekee kabisa mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na viongozi wakuu wa Kanisa ili kuwawezesha watawa kufanya hija ya pamoja kwa kujikita katika “dhana ya sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Karama za mashirika mbali mbali hazina budi kupyaishwa kwa kusoma alama za nyakati; watawa waendelee kujenga na kudumisha umoja na udugu, tayari kujisadaka katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia.

Kris Van Damme amewahimiza waamini walei kuchuchumilia wakfu wa maisha ya kifamilia unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha na utume wa familia; kwa kujikita katika umoja na utofauti wa karama, kwa ajili ya upendo kwa Kristo na Kanisa lake. Haya yote ni matunda ya kazi ya Roho Mtakatifu. Mama Jeanne Marie Cooper, mwamini mlei aliyejiweka wakfu kwa zaidi ya miaka kumi sasa, amemshukuru Mungu kwa kumwezesha kukutana na waamini walei, wanaojiweka wakfu kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Anawaalika watawa na waamini walei kuomba huruma ya Kristo Yesu, kwa ajili ya toba na wongofu wa watu, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.