Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Vijana jitahidini kutafuta mambo mema, mazuri na matakatifu!

Wafundeni vijana ili kufahamu na kufuata mambo mema, mazuri na matakatifu katika maisha.

08/05/2018 11:30

Vijana wa kizazi kipya wanahitaji majibu muafaka kama sehemu ya safari ya ukuaji wao kiroho na kimwili, tayari kuwajibika barabara ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo! Hii ni dhamana ambayo inapaswa kutekelezwa na wazazi, walezi na jamii katika ujumla wake, lakini Mama Kanisa anayo dhamana kubwa na wajibu wa kuwaonesha vijana dira na mwongozo wa maisha ili kuwawezesha kufanya hata maamuzi magumu! Mama Kanisa anataka kutoa majibu muafaka yatakayojibu yanayojikita katika sakafu ya maisha ya vijana wa kizazi kipya. Lengo ni kuwawezesha vijana kuchuchumia kile kilicho chema, kweli na kizuri katika maisha. Vijana wanapaswa kufundwa ili kuelewa na kufuata mambo mema, mazuri na matakatifu katika maisha yao!

Hii ndiyo changamoto ambayo imefanyiwa kazi na Monsinyo Krzysztof Jòzef Nykiel hakimu wa Idara ya Toba ya Kitume katika kongamano la vijana lililongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Sakramenti ya Upatanisho” kama sehemu muhimu sana ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayofanyika mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”. Lengo kuu ni kuwawezesha vijana kupambanua miito yao na hivyo kuwa tayari kutoa majibu magumu, tayari kumfuasa Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu. Wongofu wa ndani na upatanisho ni maneno makuu ambayo yametumiwa na Monsinyo Krzysztof Jòzef Nykiel katika hotuba yake, ili hatimaye, kuweza kufikia na kugusa udhaifu wa vijana wa kizazi kipya; watu wanaoteseka kutokana na msongo wa mawazo, hali ya kukata tamaa na hata pengine kijana kuchanganyikiwa katika maisha. Kwa njia ya toba, wongofu wa ndani na upatanisho, Kanisa linajielekeza kikamilifu katika kutekeleza dhamana na wajibu wake katika maisha ya vijana wa kizazi kipya.

Hili ni Kanisa linalotaka kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya vijana wa kizazi kipya. Vijana kwa upande wao wanapaswa pia kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili hatimaye, waweze kutubu na kumwongokea Mungu! Waguswe na Injili ya Kristo kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wawili wa Emau, walioandamana na Kristo Yesu katika hija ya maisha na mashaka kutokana na kashfa ya Msalaba, wakamtambua alipowafunulia Maandiko Matakatifu na kwa kuumega Mkate! Monsinyo Krzysztof Jòzef Nykiel amesema maisha na utume wa vijana unaweza kuangaliwa katika nyanja mbali mbali za maisha: kiutu, kisaikolojia, kisanaa, kichungaji, kitaalimungu na katika maisha ya Kisakramenti. Vijana wana kiu ya umoja, udugu na maisha ya kijumuiya yatakayowawezesha kukuza na kudumisha tunu na karama zao, ili hatimaye, kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi; upweke hasi unaowatumbukiza hata wakati mwingine katika magonjwa ya akili kama vile sonona.

Vijana katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Vijana, wameonesha kiu ya kutaka kusaidiwa kukuza na kuboresha maisha yao ya kiroho. Sakramenti ya Upatanisho ni chemchemi ya huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa waja wake. Sakramenti hii kadiri ya Mtakatifu Yohane Paulo II haina budi kusimikwa kwanza kabisa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko; Pili, Neno la Mungu na tatu, Maisha ya Kisakramenti. Vijana wanahitaji mashuhuda wa utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku; watu ambao wanajitahidi kujenga mahusiano mema na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na matendo ya huruma, kielelezo cha imani tendaji. Licha ya ushuhuda, vijana wanahitaji kusikia lugha ambayo itagusa undani wa maisha yao, ili hatimaye, kuyafahamu Mafumbo yanayoadhimishwa na Mama Kanisa. Lugha nyepesi isaidie kufafanua mambo msingi katika maisha na kwamba, mashuhuda wanapaswa kuwa ni vyombo vya huruma na upendo kwa vijana.

Kwa njia hii, vijana wanaweza kugundua ndani mwao ile njia ya maisha inayowarejesha tena na tena katika kisima cha huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko endelevu kutoka kwa Kristo Yesu, ambaye daima yuko mlangoni, akiwasubiri waja wake waweze kurejea tena nyumbani kwa Baba, kama ilivyokuwa kwenye Injili ya Baba mwenyehuruma na Mwana mpotevu! Vijana wachakarike kulisoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika maisha yao, ili hatimaye, waweze kupata maisha na uzima wa milele. Kristo Yesu ni jibu muafaka ya shida na mahangaiko ya vijana wa kizazi kipya, wakimtegemea na kumtumainia, kwa hakika ataweza kuzima kiu na matamanio yao halali ya maisha!

Sakramenti ya Upatanisho ni njia muafaka katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Hapa, vijana wanapata nafasi tena ya kusikilizwa katika undani wa maisha yao, ili kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Sakramenti ya Upatanisho ni kitalu muhimu sana cha kupambanua na kung’amua miito katika maisha ya vijana wa kizazi kipya. Vijana wakikimbilia kwenye Mahakama ya huruma katika hali ya unyenyekevu, ukweli na unyofu na hasa kwa kujenga utamaduni wa kuipokea Sakramenti hii mara kwa mara katika maisha, wanaweza kuonja: huruma, upendo na msamaha wa Mungu; mambo msingi yanayowakirimia furaha ya maisha. Katika hali na mazingira kama haya, vijana wanaweza pia kuonesha uhuru wa kuambata wito kutoka kwa Kristo kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Vijana wanapaswa kuthamini Sakramenti ya Upatanisho katika maisha yao, kama mahali pa majadiliano katika ukweli na uwazi, mbele ya Mwenyezi Mungu, ili kupata kile ambacho roho ya vijana inapenda. Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, vijana wanaweza kutekeleza matamanio yao halali katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

08/05/2018 11:30