Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa Francisko: Silaha za kupambana na shetani: Sala, toba na funga

Papa Francisko: Silaha za kupambana na shetani ni: sala, funga na toba ya kweli katika maisha ili kuambata neema na baraka za Mungu tayari kutembea katika upya wa maisha.

08/05/2018 14:49

Waamini wanahamasishwa kuwa macho dhidi ya shetani na vishawishi vyake vinavyoweza kuwavuruga katika maisha yao ya kiroho, kiasi hata cha kuvunjilia mbali mahusiano na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani! Shetani ni baba wa uwongo anayeweza kuwatumbukiza katika majanga kwa kuwapaka mafuta kwa mgongo wa chupa! Ili kuweza kupambana na shetani, Ibilisi, waamini wanapaswa kujikita katika maisha ya sala, kwa kukesha na kufunga kama njia ya kuratibu vilema vya maisha yao, tayari kuambata neema ya Mungu!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 8 Mei 2018 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawataka waamini kutothubutu hata kidogo kuhojiana na Ibilisi, kwani ni mjanja na atawabwaga chini, anafahamu kung’ata na kupulizia. Sehemu kubwa ya machimbuko ya mahubiri ya Baba Mtakatifu ni kutoka katika Injili ya Yohane 16:5-11mintarafu habari ya dhambi, haki na hukumu.

Shetani alikwishashindwa, lakini kwa bahati mbaya sana, binadamu anapenda na daima anaanguka kishawishini kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kushawishi hasa katika masuala ya madaraka, ufanisi, zawadi na mambo ambayo yamerembwa kwa nje, lakini ndani yake kuna sumu kali. Ibilisi anapenda kugusa anasa za binadamu, udadisi na hatimaye, kutoa ushauri wake ambao si rahisi sana kuukwepa. Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika maisha ya sala, kukesha na kufunga, ushauri ambayo ulitolewa na Kristo Yesu kama njia ya kumshinda Ibilisi na vishawishi vyake.

Mababa wa Kanisa wanawashauri waamini kutomkaribia kabisa Ibilisi, atawang’ata kwani hata waswahili wanasema, kamwe “Nyuki hawezi kukumbatiwa”. Waamini wamkimbie Ibilisi kutoka katika maisha yao ya kiroho. Kamwe wasithubutu kuhojiana na Ibilisi katika maisha yao. Eva alijaribu na akakiona cha mtema kuni. Ibilisi ni mjanja sana. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka waamini kusali, kufunga, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Wanapokabiliwa na kishawishi wakimbilie ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu kama wafanyavyo watoto wadogo wanapokabiliwa na matatizo pamoja na changamoto za maisha. Katika patashika nguo kuchanika za maisha ya kiroho, waamini wamkimbilie Bikira Maria ili aweze kuwafunika kwa joho lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

08/05/2018 14:49