2018-05-08 15:04:00

Miaka 70 ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Papa kushiriki, 21 Juni!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika kipindi cha Mwaka 2018 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1948, likiwa na Makanisa wanachama 147 na tangu wakati huo, zaidi ya Makanisa 200 yamejiunga na kuwa ni sehemu ya Baraza hili. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki ni mjumbe mtazamaji wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Vatican imetoa ratiba elekezi ya hija ya kiekumene ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Geneva, nchini Uswiss kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 70 tangu Baraza la Makanisa Ulimwengu lilipoanzishwa.

Hii itakuwa ni hija ya siku moja na itafanyika hapo tarehe 21 Juni 2018. Kati ya matukio makuu yanayotarajiwa kufanywa na Baba Mtakatifu ni pamoja na: Sala ya Kiekumene ambamo Baba Mtakatifu atatoa mahubiri;  kuzungumza na viongozi wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia; kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Palexpo na baadaye jioni kurejea tena mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko atakuwa ni kiongozi mkuu wa kwanza wa Kanisa Katoliki kutembelea Uswiss, tangu baada ya Mtakatifu Yohane Paulo II kutembelea nchini humo kunako mwaka 2004.

Baba Mtakatifu atakapowasili atapata fursa ya kufanya mazungumzo ya faragha na Rais wa Shirikisho la Uswiss Bwana Alain Berset. Baba Mtakatifu atapata chakula cha mchana na viongozi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwenye Taasisi ya Kiekumene ya Bossey, iliyoko kilometa 25 nje kidogo ya mji wa Geneva. Uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu katika kilele cha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni ni sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kiekumene, ili kuungana, kushirikiana na kushikamana kwa pamoja katika kukabiliana na changamoto mamboleo katika: umoja, utume, haki na amani duniani.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha umoja wa Makanisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Limeendelea kuratibu na kusimamia majadiliano ya kitaalimungu miongoni mwa Makanisa na matunda ya majadiliano haya yanaanza kuonekana. Kumekuwepo na maridhiano pamoja na matamko ya pamoja kuhusu: Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi; Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Dhamana na Utume wa Kanisa kama chombo na shuhuda wa umoja, upendo na mshikamano wa dhati, ili walimwengu waweze kumwamini Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limekuwa mstari wa mbele kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Baraza litaendelea kuwa mstari wa mbele kutetea haki msingi za binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Baraza limeendeleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini kwa kuwashirikisha viongozi wa dini na Makanisa mbali mbali duniani, lakini zaidi kwa kuwashirikisha vijana wa kizazi kipya, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na mshikamano kati ya watu wa Mataifa.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni limekuwa ni jukwaa makini la kushirikishana: utajiri, amana na tunu msingi za maisha ya Kiinjili na kiutu. Limeendelea kudumisha mapokeo ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo  sanjari na kudumisha uekumene wa maisha ya kiroho; uekumene wa damu, uekumene wa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Baraza limeendelea kujizatiti katika kukuza na kudumisha sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Tangu mwaka 1992, Baraza la Makanisa Ulimwenguni limeragibisha haki ya mazingira kwa kutambua kwamba, uchafuzi wa mazingira una maadhara makubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.