2018-05-08 14:10:00

Katiba ya Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha yapitishwa


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia Katiba Mpya ya Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kuchapishwa rasmi kwenye Gazeti la L’Osservatore Romano na kwenye Jalida Acta Apostolicae Sedis na kuanza kutumika kwa majaribio kuanzia tarehe 13 Mei 2018. Katiba hii imegawanyika katika Ibara 15. Lengo la Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha ni kujishughulisha na sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa vijana na familia mintarafu utume na mpango wa Mungu, ili kulinda na kudumisha maisha ya binadamu.

Baraza hili litatekeleza dhamana na utume wake kwa kuzingatia kanuni ya urika, sinodi pamoja na kanuni auni. Baraza litashirikiana kwa karibu na Makanisa mahalia, vyama na mashirika ya kitume ili kubalidishana uzoefu na mang’amuzi kwa lengo la kutaka kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya binadamu. Pamoja na mambo mengine, Baraza lina dhama ya kuandaa makongamano ya kimataifa mintarafu utume kwa waamini walei, vijana, taasisi za maisha ya ndoa na familia; utume wa familia na maisha pamoja na waamini walei katika ujumla wao.

Baraza lina wajibu wa kukuza na kudumisha wito, maisha na utume wa waamini walei katika Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Waamini walei ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na hivyo wanafanywa kuwa ni taifa la Mungu na hivyo kushirikishwa huduma ya kikuhani, kinabii na kifalme ya Kristo Yesu, hivyo wanatekeleza kadiri ya uwezo wao, utume wa taifa lote la Kikristo katika Kanisa na katika ulimwengu. Hawa ni waamini wanaoshiriki katika vyama na mashirika mbali mbali ya kitume ndani ya Kanisa.

Baraza litakuwa na dhamana na kuwasaidia waamini walei kuyafahamu Mafundisho tanzu ya Kanisa. Waamini walei wanao wajibu wa kuyatakatifuza malimwengu. Waamini walei wanakumbushwa kwamba, uchungu na fadhaa ya mwanadamu wa nyakati hizi, hasa ya maskini na wale wote wanaoteseka ni furaha na matumaini, machungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Kumbe, waamini walei wanapaswa kujikita katika shughuli za uinjilishaji katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu.

Baraza linawajibika pia kuwahamasisha waamini kujikita katika katekesi makini na endelevu; kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa na Maisha ya Kisakramenti; matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na kushiriki katika ustawi na maendeleo ya jamii. Baraza litakuwa linaratibu vyama na mashirika ya kitume miongoni mwa waamini walei kadiri ya mamlaka yake. Ni wajibu wa Baraza kuandaa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, Siku ya Familia Kimataifa sanjari na kukuza utu, heshima na ushirikiano kati ya wanawake na wanaume. Ni jukumu la Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha litakuwa na dhamana ya kuandaa na kusambaza mafundisho tanzu kuhusu familia kwa njia ya katekesi makini, maisha ya kiroho, tunu msingi za ndoa na familia kama sehemu ya mchakato wa majiundo endelevu. Litato adira na mwongozo ya maandalizi kwa ajili ya wanandoa watarajiwa kama kielelezo cha mshikamano wa viongozi wa Kanisa. Ni wajibu wa Baraza pia kujihusisha na majiundo endelevu kwa vijana wa kizazi kipya.

Baraza litashirikisha kwa karibu sana na Taasisi ya Kitaalimungu ya Ndoa na Familia ya Yohane Paulo II kwa ajili ya Sayansi ya Ndoa na Familia pamoja na taasisi nyingine zinazojihusisha na masuala ya ndoa, familia na maisha. Baraza litakuwa mstari wa mbele kulinda na kudumisha Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Litawajibika kuwasaidia wanawake waliojihusisha na utoaji mimba. Kwa kuzingatia kanuni maadili sheria, taratibu na Mafundisho tanzu ya Kanisa, Baraza litajihusisha na bayolojia dawa na sera zake mintarafu maisha ya binadamu na litaendelea kuwa na uhusiano wa karibu na Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya maisha. Katiba ya Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha itaanza kutumika kwa majaribio kuanzia tarehe 13 Mei 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.