2018-05-07 16:34:00

Wanajeshi 32 wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Vatican wala kiapo!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumapili, tarehe 6 Mei 2018 ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu kwa ajili ya wanajeshi 32 wa Kikosi cha Ulinzi na Usalama cha Vatican, maarufu kama “Swiss Guards”, baada ya kuhitimu mafunzo yao katika mfumo mpya na kula kiapo cha utii na uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni siku maalum kwa wanajeshi hawa ambao wanawakumbuka wanajeshi wenzao 147 waliofariki dunia kunako mwaka 1527 kwa kujitoa mhanga kumlinda Baba Mtakatifu. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amewataka wanajeshi hawa wapya kusonga mbele kwa imani, matumaini na ujasiri, daima wakitambua kwamba, kwa njia ya utume na maisha yao, ni mashuhuda pia wa imani na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake!

Kiapo cha utii na uaminifu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni changamoto katika mchakato mzima wa uwajibikaji na huduma inayotolewa katika moyo wa utii na unyenyekevu kwa wakuu wa vikosi vya ulizni na usalama, Kanisa na Khalifa Mtakatifu Petro. Ushuhuda wao unapata chimbuko lake katika imani kwa Kristo Mfufuka. Huu ni ushuhuda wa upendo kwa Mungu na jirani kiasi hata cha kujisadaka bila ya kujibakiza. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru kwa ushuhuda wa imani, ukarimu na upendo unaotolewa na wanajeshi hawa vijana kwa ajili ya ulinzi na usalama wa Vatican.

Kardinali Pietro anakaza kusema, wao ni mashuhuda wa upendo wa Kristo kiasi hata cha kujisadaka! Kanisa linawaombea ili waweze kujikita katika dhamana na wajibu wao, daima wakijiweka chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, kwani bila yeye, hawawezi kamwe kufua dafu, dhamana inayohitaji ari, sadaka na ujasiri wa pekee kabisa! Kama sehemu ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba hapa mjini Vatican, wanajeshi hawa vijana pia wanahamasishwa kupambanua wito wao na kwamba, wao watakuwa na nafasi ya pekee kufuatilia matukio haya hapa mjini Vatican.

Kiapo cha utii ni alama ya imani inayowaunganisha katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, wanapaswa kubaki wakiwa wamezama katika upendo kwani Mungu ni upendo! Huu ndio muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo kwa waja wake. Kama wanajeshi wanahimizwa kuwa watii kwa Amri Kuu ya Upendo kwa Mungu na Jirani, ili kuweza kushiriki katika furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, tayari kuambata mchakato wa utakatifu wa maisha kama anavyokaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume: “Gaudete et exsultate” yaani Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo.” Huu ni mwaliko kwa waamini wote kwa sababu kwa njia ya Ubatizo wamekuwa ni marafiki wa Kristo Yesu.

Huu ni wito na utume unaowezekana na wala hakuna sababu ya kukata wala kukatishwa tamaa. Wanajeshi hawa wamekumbushwa kwamba, wanatekeleza dhamana na utume kwa ajili ya Kanisa la Kristo na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha ushuhuda kwa ajili ya upendo wa Kristo na Kanisa lake. Mtakatifu Gregori Mkuu anasema, kuna kifodini cha upanga, lakini pia kuna kifodini uvumilivu unaooneshwa kwa namna ya pekee kabisa na kazi wanayoitekeleza kila siku kwa uaminifu, weledi na uadilifu mkubwa. Katika nyakati ngumu, matatizo, changamoto na kinzani, watambue kwamba, wamekuwa ni marafiki wa Kristo Yesu, ili waweze kuwa watakatifu. Haya ni mapambano endelevu katika maisha. Upendo kwa Mungu na jirani ni chachu ya utakatifu wa maisha unaomshuhudia Kristo Mfufuka. Mwishoni mwa mahubiri yake, Kardinali Pietro Parolin, amewaweka wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama vya Vatican nchini ya ulinzi na tunza ya watakatifu: Martini, Sebastiano na Nicola de Flue, ili waweze kuwasindikiza katika maisha ya Kanisa, Khalifa wa Mtakatifu Petro na watu wote wanaohitaji msaada na uwepo wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.