Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Sala ya Malaika wa Bwana

Upendo wa Kristo unawawajibisha waamini kulinda na kudumisha uhai!

Papa Francisko: Upendo wa Mungu unamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. - REUTERS

07/05/2018 07:53

Liturujia ya Neno la Mungu katika Kipindi cha Pasaka inaendelea kuonesha mtindo wa maisha kama shuhuda wa Jumuiya ya Kristo Mfufuka, kwa kukaa katika pendo la Kristo, linalobubujika kutoka katika upendo wa Mungu, ili kweli upendo wao, uweze kuwa na dira, mwelekeo sahihi na kung’ara katika maisha. Wakristo wanapaswa kupokea upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa moyo wa shukrani sanjari na kuhakikisha kwamba, wanadumu katika upendo huo kwa kuepuka: ubinafsi pamoja na dhambi. Hii programu nzito lakini inayowezekana kumwilishwa katika maisha ya Wakristo! Jambo la msingi ni waamini kutambua kwamba, upendo wa Kristo si jambo la mtu kujisikia tu, bali unapata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu na kuishi kadiri ya mapenzi na Amri za Mungu.

Huu ni muhtasari wa tafakari iliyotolewa na Baba Mtatakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 6 Mei 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, uliokuwa umepambwa kwa bahari ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo wa Mungu unamwilishwa katika matendo, vinginevyo yatabaki maneno matupu ambayo kimsingi hayawezi kuvunja mfupa! Ni upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa jirani, mwenye sura na historia kamili. Huyu ndiye anayemchangamotisha kutoka katika ubinafsi, mafao binafsi, usalama na hali ya kujiamini; huyu ni jirani mwenye kuhitaji kusikilizwa kwa makini na kuanza kutembea naye hatua kwa hatua katika njia ya matumaini. Ni upendo unaoshuhudiwa kwa watu wenye shida na mahangaiko mbali mbali katika maisha kwa kuanzia na wale ambao wako karibu sana katika: familia, jumuiya, eneo la kazi na shule. Kwa mwamini ambaye anaendelea kukaa katika pendo la Kristo, upendo wake unaweza kuwafikia wengine na kuwavutia kwenye urafiki wake.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kudadavua kwa kusema kwamba, upendo huu unapaswa kuwa ni endelevu katika maisha. Ndiyo maana, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaitwa kuwalinda na kuwatunza wazee ambao ni amana na utajiri wa jamii, hata kama wanaweza kusababisha matatizo na changamoto za kiuchumi, lakini, wanapaswa kulindwa na kutunzwa kwa heshima. Ni upendo wanaopaswa kuoneshwa wagonjwa hadi dakika ya mwisho wa maisha yao.

Ni upendo wanaopaswa kuoneshwa watoto tangu dakika ile wanapotungwa tumboni mwa mama zao, kwani Injili ya uhai, inapaswa kupokelewa, kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa, kadiri ya mpango wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ndio muhtasari wa upendo wa Mungu kwa binadamu. Waamini wameonja upendo wa Mungu kwa njia ya Kristo Yesu, anayewataka hata wao kupenda kama anavyopenda yeye mwenyewe. Wakristo wanaweza kutekeleza agizo hili ikiwa kama wanao Moyo kama wa Yesu.  Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ambalo kimsingi waamini wanashiriki kila Jumapili yanalenga kuunda Moyo wa Kristo, ili maisha ya waamini yaweze kuongozwa na matendo ya huruma na mapendo. Mwishoni, Baba Mtakatifu amemwomba Bikira Maria, awasaidie waamini kubaki katika pendo la Yesu ili kukua na kukomaa katika upendo kwa jirani, lakini zaidi kwa ajili ya maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa njia hii, Wakristo watakuwa wanatekeleza kikamilifu wito wao wa Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

07/05/2018 07:53