2018-05-07 14:49:00

Parokia inapaswa kuwa ni kitovu cha ushuhuda na uinjilishaji wa kina


Baba Mtakatifu Francisko akiwa kwenye Parokia ya “SS. Sacramento” iliyoko kwenye kitongoji cha Tor dè Schiavi, nje kidogo ya Jimbo kuu la Roma, Jumapili, tarehe 6 Mei 2018 amepata nafasi ya kujibu maswali manne kutoka kwa familia ya Mungu Parokiani hapo. Baba Mtakatifu amewakumbusha wazazi na walezi kwamba, wanayo dhamana nyeti ya kuwalea, kuwasindikiza pamoja na kuwafunda watoto wao tunu msingi za maisha ya Kikristo. Wajibu huu, wakati mwingine unatekelezwa na wazee katika familia. Hii inatokana na ukweli kwamba, kutokana na majukumu ya kazi, umbali na ufinyu wa muda, wazazi wanashindwa kutekeleza vyema wajibu wao.

Familia inapaswa kuwa ni mahali pa kwanza kabisa ambako watoto wanajifunza tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko unaotolewa na wazazi pamoja na walezi wao. Wazazi wahakikishe kwamba, wanatenga muda wa kuwa pamoja na watoto wao na kamwe wasiwe ni watumwa wa kazi. Shule ni mahali muhimu pa kukazia tunu msingi ambazo watoto wamejifunza kutoka kwenye familia zao. Ukuaji makini wa watoto unahitaji uwepo wa familia na wazazi watumie fursa hii kucheza na kukaa pamoja na watoto wao, kwani kwa njia hii, wanawarithisha mambo msingi katika maisha. Wazazi wasaidie kujibu maswali tete kutoka kwa watoto wao kwa hekima na busara. Wazazi wajifunze, kucheza, kuzungumza na kukaa pamoja na watoto wao kama njia ya kuwafundisha fadhila ya upendo, imani na matumaini.

Baba Mtakatifu Francisko akijibu swali la pili amekaza kusema, kimsingi Kanisa linapaswa kuwa ni shule ya utakatifu, ukarimu, upendo na mshikamano wa dhati, lakini wakati mwingine, tunu hizi zinakosekana na ushuhuda wa Kanisa unatoweka kama ndoto ya mchana! Parokia inapaswa kuwa kama familia, mahali ambapo waamini wanajifunza ukarimu na upendo kwa kusaidiana na kufarijiana kwa hali na mali. Hii inatokana na ukweli kwamba, kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu ameamua kukaa kati pamoja na watu wake, kumbe, uwepo wa Mungu unapaswa kushuhudiwa ndani ya nje ya Kanisa. Parokia zijenge na kudumisha ukarimu kama sehemu ya mchakato wa kuwaonjesha watu wa Mungu furaha ya Injili ya Kristo! Ushuhuda mkubwa uliotolewa na Kristo Yesu katika maisha yake ni ukaribu wake kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamiii. Hawa akawarejeshea utu na heshima yao; akawapatia mahitaji yao msingi; akawaponya magonja na hatimaye, akawaondolea dhambi zao. Waisraeli wakiwa jangwani walionja uwepo wa Mungu katika maisha yao, changamoto hata kwa waamini kuwa karibu na jirani zao wakati wa raha na shida.

Baba Mtakatifu akijibu swali la tatu, amewataka vijana wa kizazi kipya kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kwa vijana wenzao wanaoogelea katika upweke hasi! Wasaidiwe na ushuhuda unaobubujika kutoka katika familia ya Mungu inayoonesha ile furaha ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha yao. Waamini walei, wajitahidi kufahamu wajibu na mipaka yao katika maisha na utume wa Kanisa; wawe huru kuhudumia bila kufungwa na ubinafsi wala masilahi yao binafsi, daima wakisukumwa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili ambayo ni zawadi kutoka kwa Kristo Mfufuka. Kanisa linakuwa na kustawi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko na wala si kwa wongofu wa shuruti. Kama wafuasi wa Kristo Mfufuka washikamane, wapendane na kusaidiana kama kielelezo cha ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Waamini wa Kanisa la mwanzo waliposhukiwa na Roho Mtakatifu, waliwezesha kushuhudia furaha ya Injili na wakawavuta watu wengi katika imani.

Mwishoni, mtoto mmoja amemwomba Baba Mtakatifu kumkumbuka na kumwombea Mama yake mzazi ambaye alikuwa anasubiri kufanyiwa upasuaji mkubwa. Amewapongeza watoto wanaojisadaka kwa ajili ya kusali na kuwaombea wazazi na walezi wao, kwani huu ni wajibu wao kama watoto. Baba Mtakatifu anawataka watoto kuwa ni chachu ya maisha na utume wa familia, ili ziweze kukua na kukomaa katika fadhila mbali mbali za Kikristo. Kwa maswali na majibu haya mubashara kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, familia ya Mungu kutoka kwenye Parokia ya “SS. Sacramento” iliyoko Tor dè Schiavi imefurahia uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petrokati yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.