Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Sala ya Malaika wa Bwana

Papa Francisko asikitishwa na mauaji ya kikatili Afrika ya Kati!

Papa Francisko asikitishwa sana na mauaji ya kinyama huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati. - AFP

07/05/2018 08:17

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili iliyopita, tarehe 6 Mei 2018, aliyaelekeza mawazo yake huko Aquisgrana nchini Ujerumani ambako, Jumamosi, tarehe 5 Mei 2018 Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko amemtangaza Mtumishi wa Mungu Clara Fey, Mwanzilishi wa Shirika la Watawa Fukara wa Mtoto Yesu kuwa Mwenyeheri. Mwenyeheri Clara Fey aliishi katika kipindi cha Mapinduzi ya Viwanda Barani Ulaya yaliyosababisha mtikisiko na myumbo mkubwa wa uchumi kitaifa na kimataifa; watu wengi wakajikuta wanatumbukia katika umaskini wa hali na kipato; ukosefu wa fursa za ajira, makazi na elimu bora.

Watu wengi wakadhalilishwa utu na heshima yao na kujiona si mali kitu! Mwenyeheri Clara Fey aliyebahatika kutoka katika familia iliyokuwa inajiweza kiuchumi, akawa ni kimbilio la wakleri na watawa wengi kwa ajili ya huduma kwa watoto maskini, yatima na wale waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi.  Akawa ni jibu muafaka katika kukabiliana na changamoto za Mapinduzi ya Viwanda nchini Ujerumani, kiasi hata cha kusadaka maisha yake kwa ajili ya jirani zake.

Kunako mwaka 1837 akiwa na umri wa miaka 22 akaanzisha shule kwa ajili ya wasichana maskini na kunako mwaka 1844 akaanzisha kituo cha watoto yatima kwa kutumia utajiri wake wote kwa ajili ya kuwahudumia watoto hawa. Mwaka huo huo, akaanzisha Shirika la Watawa Fukara wa Mtoto Yesu ili kuwasaidia watoto na vijana waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Mwenyeheri Clara Fey katika maisha na utume wake, alikumbana na “mkono wa chuma” kutoka Serikalini, kiasi kwamba, akalazimishwa kuacha shughuli na utume wake na kuhamia katika nchi jirani, huku akiwa na utulivu wa ndani pamoja na kujiaminisha katika ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu katika maisha yake.

Jambo ambalo lilikuwa linampatia hofu kubwa ni usalama wa maisha ya watawa wake waliokuwa wanaendelea kuongezeka kwa kasi kubwa ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa vijana na watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Kwa bahati mbaya, shule zake nyingi alizoanzishwa zikafungwa na Serikali, hata hivyo hakukata wala kukatishwa tamaa na chuki hizi, akaendelea kujisadaka bila ya kujibakiza, hadi alipofariki dunia hapo tarehe 8 Mei 1894. Huyu ndiye Mwenyeheri Clara Fey ambaye, Baba Mtakatifu Francisko amemwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani kutokana na sadaka ya maisha yake kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa njia ya huduma ya elimu kwa vijana na watoto waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana,  ameikumbuka na kuiombea pia Familia ya Mungu, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ambayo alipata bahati ya kuitembelea na kufungua Lango la Maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu, Jimbo kuu la Bangui, matukio ambayo bado yameacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wake. Hivi karibuni, huko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, kumetokea mapigano makali yaliyosababisha watu kadhaa kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa vibaya. Katika mapigano hayo, hata Padre mmoja aliuwawa kikatili! Kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa amani, awasaidie watu wote kuondokana na chuki pamoja na hali ya kutaka kulipizana kisasi, ili wote kwa pamoja waweze kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka kwa namna ya pekee kabisa, wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliokuwa wamekusanyika mjini Roma kumzunguka Baba Mtakatifu Francisko ili kumwimbia Mwenyezi Mungu “Utenzi wa shukrani”,  yaani “Te Deum" kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewataka wanachama wa Njia ya Ukatekumeni mpya kujenga umoja na mshikamano na Kanisa, viongozi na waamini wengine, ili waweze kutembea pamoja kama sehemu ya mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, daima wakiendelea kuwa waaminifu kwa karama na utume wao katika Kanisa ambao ni kuwafundisha watu kuwa wanafunzi wa Kristo kwa kuzingatia hali na mazingira ya maisha yao. Marufuku kufanya wongofu wa shuruti, kwani hauna mvuto wala mashiko!

Wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Mfufuka kwa kutokubali kumezwa na malimwengu kwa kupenda sana fedha, utajiri na anasa za dunia. Hili ni tukio ambao limeshuhudiwa na bahari ya waamini kutoka katika nchi 134 zenye Jumuiya 21, 300 ambazo zimeundwa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Jumuiya hizi zinatekeleza dhamana na utume wake katika Parokia 6, 270 na zaidi ya familia 1, 668 ziko sehemu mbali mbali za dunia kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa “uinjilishaji wa awali”, maarufu kama “Missio ad gentes” kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wanachama wa Njia ya Ukatekumeni Mpya kwa juhudi zao katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

07/05/2018 08:17