Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Onesheni upendo wa Mungu kwa kuwajali na kuwaheshimu jirani zenu!

Papa Francisko asema, upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu unamwilishwa katika huduma makini na heshima kwa jirani.

07/05/2018 13:51

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Parokia ya “SS. Sacramento” iliyoko Tor dè Schiavi, nje kidogo ya Jimbo kuu la Roma, Jumapili, tarehe 6 Mei 2018 amekazia kwa namna ya pekee wosia ulioachwa na Kristo Yesu kabla ya kukabiliana na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake. Aliwataka Mitume wake kukaa katika pendo lake, kujifunza kutoka katika Moyo wake Mtakatifu jinsi ya kupenda bila kujibakiza, kiasi hata cha kutoa maisha yake ili yaweze kuwa ni fidia na maondoleo ya dhambi.

Huu ni upendo unaomwilishwa katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Upendo ni kazi inayowawajibisha wazazi na walezi kutoa huduma makini kwa familia zao! Ni dhamana na wajibu wa maisha ya Kikristo unaopaswa kumwilishwa katika medani mbali mbali za maisha kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji kama ilivyo Parokia hii, ambayo kwa hakika ni mfano wa bora wa kuigwa katika huduma kwa maskini kwa kuwajengea “Nyumba ya furaha” kwa kuwapatia makazi wazazi wenye watoto walemavu, watoto yatima na wote wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Waamini wanaweza kujifunza upendo huu kutoka kwa Kristo Yesu, ambaye ni ufunuo wa upendo wa Baba wa milele kwa waja wake. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye aliyeanza kuwapenda, kiasi hata cha kumtuma Mwanaye wa pekee, kuja kuwaokomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti, ili kuwashirikisha utukufu wa wana wa Mungu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuonesha upendo kwa kuwaheshimu na kuwajali jirani; kwa kuwalinda na kuwatunzia utu wao kama binadamu na kwamba, majungu si mtaji, wangetajirika wengi. Waamini wawe makini katika kutumia ndimi zao pamoja na kujenga utamaduni wa kutenda wema na kwenda zao, bila kungojea shukrani au zawadi. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuchunguza dhamiri zao ili kuangalia ikiwa kama bado wamebaki katika pendo la Kristo! Waangalie jinsi wanavyotumia ndimi zao na kwamba, changamoto kubwa kwa wakati huu ni utakatifu unaoshuhudiwa na jumuiya ya waamini. Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake kwa kusema kwamba, upendo ni huduma kwa ajili ya Mungu na jirani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

07/05/2018 13:51