2018-05-05 14:07:00

Papa Francisko: Nguzo za maisha ya kitawa: Sala, Ufukara na Uvumilivu


Maisha ya kitawa na kazi za kitume yanasimikwa kwa namna ya pekee kabisa kwenye mihimili mikuu mitatu: sala, ufukara na uvumilivu, changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 4 Mei 2018, alipokutana na kuzungumza na washiriki wa kongamano la kimataifa la maisha ya kitawa lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema hivi ni vigezo muhimu sana katika mchakato wa kupambanua wito wa maisha ya kitawa yanayokumbana na changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Baba Mtakatifu anasema, leo hii, watawa wasipokuwa makini na waangalifu wanaweza kumezwa na malimwengu; kuna mapambano na “vijembe” vinavyoendelea kati ya watawa kiasi cha kuacha kurasa ngumu na chungu katika maisha ya kijumuiya, kumbe, mwaliko ni kumwachia nafasi Roho Mtakatifu aweze kuwafunda na kuwaunda watawa kadiri ya dira na mwelekeo wa maisha na utume wa Mama Kanisa. Roho Mtakatifu ni muasisi wa karama na mapaji mbali mbali yanayoendelea kuibuka ndani ya Kanisa, katika umoja na utofauti wake, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Umoja na mshikamano anasema Baba Mtakatifu hata katika maisha ya kitawa na kazi za kitume ni changamoto pevu!

Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya watawa wamemezwa sana na ubinafsi pamoja na uchoyo, wanajiangalia wao binafsi. Watawa bila kujizatiti katika maisha ya sala, ufukara na uvumilivu endelevu, watajikuta wakiogelea katia “bahari ya matope” na huko watakiona cha mtema kuni! Baba Mtakatifu anawaalika watawa kukita maisha yao katika sala kwa Kristo Yesu, aliyewaona, akawaita, akawatuma kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Watawa wakumbuke kwamba, wameacha yote kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani katika hali ya unyenyeku na moyo mkuu, kwa kukita mizizi ya maisha na utume wao kwa Kristo Yesu na wala si vinginevyo!

Watawa wajenge moyo na utamaduni wa sala ambayo kimsingi ni chemchemi ya furaha ya Injili katika maisha na utume wao, hata pale wanapokumbana na matatizo na changamoto za maisha, daima wawe na ujasiri wa kurejea tena katika sala kwa kumkimbilia Kristo Yesu kwa faragha, ili kupyaisha tena ari na utume wao, vinginevyo, watawa watakuwa wanaishi maisha ya kughushi pasi na mvuto wala mashiko. Watawa watoe kipaumbele cha kwanza kwa maisha ya sala inayowawezesha kumwilisha hayo waliyosali katika huduma makini kwa jirani zao.

Mama Theresa wa Calcutta aliweza kupata nguvu na ujasiri wa kuwahudumia maskini kati ya maskini kutokana na utajiri wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, akamwona Kristo Yesu akiteseka kati ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii! Watawa wajibidishe kuwa na muda wa sala katika maisha yao na kamwe kazi, masomo na utume mwingine wowote ule usiwe ni kisingizio cha kutokusali! Mama Kanisa anawahitaji waamini ambao wanakita maisha yao katika sala inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha imani tendaji.

Ufukara ni nguzo msingi katika maisha na utume wa watawa katika ulimwengu mamboleo, lakini ni nguzo ambayo inaendelea kuporomoka kila kukicha kutokana na ukweli kwamba, kuna baadhi ya watawa ambao wameweka mbele mali na utajiri wa dunia hii bila kutambua kwamba, Ibilisi kwa kawaida anatumia fedha kuwavuruga watu na mtawa akishamezwa na tamaa ya fedha, huyo maisha na utume wake uko hatarini sana. Kila Shirika liwe makini kutekeleza nadhiri ya ufukara kadiri ya sheria kanuni na miongozo yake, jambo la msingi anakaza kusema Baba Mtakatifu Francisko ni kukuza na kudumisha ari na moyo wa ufukara, tayari kutumia rasilimali na utajiri wa mashirika kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kwa kushikamana na kuambata ufukara, watawa watakuwa wamejijengea ngome kubwa ya maisha na utume wao. Baba Mtakatifu anasema, si haba kuona kwamba, hata watawa wanamezwa na malimwengu kwa kupenda sana fedha eti ni sabuni ya roho! Pili kwa kupenda anasa na tafrija na tatu ni kiburi na jeuri ambayo mara nyingi inatokana na uwezo wa kiuchumi au kwa kuwa na fedha ambayo inageuka kuwa ni fedheha! Karama na mapaji yasipotumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Shirika, Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wake, yanakuwa ni hatari katika maisha na utume wa kitawa!

Baba Mtakatifu anawaalika watawa kuchunguza dhamiri zao ili kuangalia ni kwa kiasi gani wanakuza na kudumisha nadhiri ya ufukara katika maisha na utume wao! Jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba, wanatunza, wanalinda na kuendeleza rasilimali na utajiri wa mashirika yao kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wa huduma makini kwa watu wa Mungu! Uchoyo na ubinafsi wa mashirika ni sumu ya maendeleo ya uinjilishaji mpya!

Nguzo ya tatu anasema Baba Mtakatifu ni uvumilivu endelevu! Matunda ya Roho Mtakatifu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Ni katika uvumilivu, watawa wanaweza kutenda kadiri ya Roho Mtakatifu. Watawa wajenge na kudumisha uvumilivu huku wakichukuliana katika upendo na kwamba, hii ni sehemu pia ya matendo ya huruma kiroho! Lakini zaidi, uvumilivu wa imani unahitajika katika ulimwengu mamboleo, vinginevyo watawa wanaweza kupotelea “mahali pasikojulikana”.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, uvumilivu ni fadhila ya Kikristo inayowawezesha hata watawa kuchukuliana katika upendo na amani. Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume kila siku linakumbana na litania ya matatizo na changamoto kutoka kwa watawa, lakini linazifanyia kazi kwa uvumilivu. Fadhila ya uvumilivu inapaswa kumwilishwa katika maisha ya kijumuiya kama alivyofanya Kristo Yesu katika mchakato mzima wa Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Kwa njia hii, ameweza kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Fadhila ya uvumilivu iwawezeshe watawa kupambanua maisha, wito na utume wao wa kitawa.

Uhaba wa miito ya kitawa inayosikika katika akili na nyoyo za watu unapaswa kushughulikiwa kwa uvumilivu na kumwachia Roho Mtakatifu aweze kutenda kazi yake. Watawa wasiwe wachoyo kwa kufunga nyumba za kitawa ili kutoa fursa kwa watawa wazee kuzeeka na hatimaye kufa kifo chema. Huu ni uchu wa fedha na mali anasikitika kusema Baba Mtakatifu. Uvumilivu uwawezeshe watawa kukuza na kudumisha ari na moyo mkuu katika maisha na wito wao, daima wakijitahidi kuwa ni vyombo, mashuhuda na manabii wa furaha ya Injili.

Uchu wa mali ni kifo laini katika maisha ya kitawa! Watawa wawe na ujasiri tayari kupiga moyo konde na kumfuasa Kristo Yesu kwa imani, matumaini na mapendo kama ilivyokuwa kwa Ibrahimu Baba wa imani na mkewe Sara. Maisha ya kitawa yajengwe na kuboreshwa na maisha ya binafsi yanayofumbatwa katika maisha ya kijumuiya. Mwishoni wa hotuba yake elekezi, Baba Mtakatifu amekazia kwa mara nyingine tena umuhimu wa maisha ya sala, ufukara na uvumilifu, ili watawa waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.