Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Leo Mama Kanisa anawarudisha watoto wake kwenye shule ya upendo!

Leo Mama Kanisa anapenda kuwarejesha watoto wake kwenye shule ya upendo mkamilifu unaopata chimbuko lake kwa Mungu Baba ambaye ni upendo wenyewe! - AP

05/05/2018 07:30

Utangulizi: Yesu anasema “Amri yangu ni hii, Mpendane kama nilivyowapenda ninyi”. Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika tafakari ya Neno la Mungu katika dominika ya sita ya Pasaka. Furaha ya kipasaka ni furaha iliyo na msingi wake katika upendo, upendo wa Baba kumtuma mwanae aje aukomboe ulimwengu kwa kifo chake msalabani. Kuendeleza matunda ya pasaka ni kuuendeleza upendo huo wa Baba, upendo wa kujisadaka kwa ajili ya wengine. Kanisa leo linaturudisha katika shule ya upendo. Tuutafakari na kuuelewa upendo wa Baba kama kiini cha kuuishi upendo kati yetu, ushuhuda wa maisha mapya ya kipasaka.

Masomo kwa ufupi: Somo la Kwanza (Mdo. 10:25-26, 34-35, 44-48) linaeleza namna ambayo imani ya kikristo ilienea na kupokelewa na wasio wayahudi. Yesu alizaliwa katika uyahudi. Aliishi na kutekeleza utume wake katika mazingira hayo ya kiyahudi, wafuasi wake wa kwanza pamoja na mitume walikuwa wayahudi na hivi kanisa alilokuja kulianzisha lilizaliwa katika mazingira hayo hayo ya kiyahudi. Kwa jinsi hii ilionekana kuwa ili mtu awe mkristo itambidi pia kufuata na kuishi kadiri ya tamaduni za kiyahudi. Mojawapo ya tamaduni hizo ilikuwa ni kufanya tohara. Somo hili linamwonesha Mtume Petro anafika katika nyumba ya Kornelio, huyu hakuwa myahudi na hakuwa amefanya tohara ila yeye na familia yake walikuwa wanamcha Mungu. Petro akiwa nao, Mungu anawashushia Roho Mtakatifu kama alivyowashushia mitume siku ya Pentekoste. Petro anaukiri upendo wa Mungu usio wa upendeleo na moja kwa moja anaamuru wabatizwe.

Somo la Pili (1Yoh. 4:7-10) ni kifungu ambacho ni kitovu cha mafundisho ya Waraka wa Yohane na pia wa mafundisho ya Kanisa kuhusu upendo. Ni kifungu kinachokazia kusema kuwa upendo sio nadharia, sio kitu cha kufikirika wala sio mchezo wa maneno ya kufurahisha watu bali upendo ni kitu halisi na ni Mungu mwenyewe. “Mungu ni upendo”. Na hivyo kila apendaye amezaliwa na Mungu, anamjua Mungu na kwa maneno mengine, yuko na Mungu. Kinyume chake yule asiyependa hayuko na Mungu.

Ni kifungu kinachoonesha kuwa mwanadamu anaalikwa kuuishi upendo si kadiri anavyojisikia bali kama wajibu unaotoka kwa Mungu mwenyewe. Hii ni kwa sababu katika upendo aliyeanza ni Mungu. ni yeye aliyempenda kwanza mwanadamu hata katika kipindi ambacho tunaweza kusema mwanadamu alikuwa hapendeki kwa maana alikuwa ameanguka dhambini. Licha ya kutokupendeka kwa mwanadamu, Mungu alimpenda na akamtuma mwanae wa pekee ili kumpatanisha mwanadamu naye. Somo hili linatupatia motisha mpya ya kuuishi upendo katika maisha yetu.

Somo la Injili (Yoh. 15:9-17) Yesu anaendeleza mafundisho juu ya uhusiano wa ndani kabisa alionao na Baba, uhusiano wanaohitaji kuwa nao pia wafuasi wake kwanza wao na yeye halafu wao kwa wao. Mambo matatu yanajitokeza bayana. Mosi, kama alivyowaalika kama katika mfano wa Mzabibu katika mfano kukaa ndani yake kama matawi kwa mzabibu, katika injili ya leo Yesu anawaalika wanafunzi wake kukaa katika pendo lake. Yaani kuwa sehemu ya pendo hilo, kujazwa na pendo hilo ndani mwao, kufarijiwa na pendo hilo na kuongozwa na pendo hilo. Pili anaonesha kuwa asili ya pendo hilo ni Baba na pendo hilo ni zao la utii kwa amri zake. Yeye amenufaika nalo kwa sababu alitii. Hivyo wanafunzi wake pia watanufaika na pendo hilo kwa kuzitii amri zake.

Anasema “mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake”. Na Tatu anaukabidhi upendo kwa wafuasi wake kama amri. Hii huitwa pia amri mpya ya upendo. Ni amri mpya kwa sababu inajumuisha viumbe vyote. Si kama sheria ya Musa iliyoagiza kumpenda jirani. Aidha ni amri mpya pia kwa sababu kipimo cha upendo si tena nafsi ya yule apendaye kwamba “mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe” bali kipimo ni upendo wa Kristo kwa mwanadamu; “mpendane kama nilivyowapenda mimi”.

Tafakari: Masomo haya yanaturudisha kuutafakari upendo kutoka kwenye mzizi wake, Mungu ambaye ndiye upendo wenyewe. Ni kutoka hapo tunaona kuwa bila upendo wa Mungu ulimwengu na sisi sote si kitu. Tukianza na ulimwengu tunaona kuwa Mungu ameuumba kwa sababu tu ya upendo. Anafundisha Mt. Ireneo kuwa Mungu hakuumba ulimwengu kwa sababu angepungukiwa kitu bila ulimwengu kuwapo bali aliuumba ili kuushirikisha upendo wake (rej. Iraeneus, Adv.haere. IV 14,1). Na sio ulimwengu tu, hata sisi wenyewe wanadamu, tumeumbwa kwa sababu ya upendo wa Mungu (rej. Augustinus De Doctr.Christ I 32,35). Ndiyo maana hata baada ya anguko la mwanadamu, ni Mungu aliyechukua jukumu la kwanza kumtafuta mwanadamu amwokoe hadi akamtuma mwanae afe Msalabani. Bila upendo wa Mungu ulimwengu ungekuwa wapi? Bila upendo wa Mungu sisi tungekuwa wapi?

Kumbe leo Kristo anapotoa amri ya mapendo anataka tuone kuwa sisi ni zao la upendo wa Mungu na tena baada ya kukombolewa kwa upendo huo huo, ushuhuda wetu wa kipasaka unatuwajibisha kuuendeleza upendo huo kwa wenzetu. Upendo ambao si kwa faida ya anayependa bali ni kwa faida ya anayependwa. Ndiyo maana Kristo anasema kipimo cha upendo huo si kingine bali ni kujitoa sadaka kwa ajili ya mwingine; “hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake”.

Hata leo dunia imejaa upendo wa Mungu na huo tunauona katika maisha yetu lakini ushuhuda wa upendo huo kati ya mwanadamu na mwanadamu ndio unaokosekana mara nyingi. Kwa nini? Je, si kwa sababu sisi tunataka kuonesha upendo kwa faida yetu wenyewe na si kwa faida ya anayependwa? Je, si kwa sababu tumeyavika ngozi ya upendo matendo yetu kwa ajili ya manufaa binafsi? Na matokeo yake ni hoja kama hizi: nitapata nini? Kwa faida ya nani? Nahangaikia nini? N.k. Na hoja hizi zinaweka ukuta katika kutoa ushuhuda wa upendo huu wa kimungu kwa wenzetu.

Katika hili tunaweza kutumia mantiki ya nukuu maarufu ya mtawa wa kibudha, Dalai Lama, na kusema tumepewa amri ya mapendo ili tupendane, basi ukishindwa kumpenda mtu walau usimdhuru”. Kinyume chake tunachokiona ni watu kutafuta kunufaika kwa wale walio dhaifu. Uhitaji wa mtu: umasikini wake wa kipato, umasikini wake wa mawazo, ugonjwa wake, migogoro aliyonayo na shida zake nyingine badala ya kuwa fursa ya kumwonesha upendo kwa wengi imekuwa fursa ya kujinufaisha kiuchumi au kisiasa. Leo tunahimizwa kurudi kwenye mzizi wa upendo. Tupendane kama Mungu anavyotupenda, na kama ni faida basi tuitegemee si kwa tunayemwonesha upendo bali kwa aliye chanzo cha upendo.

Padre William Bahitwa.

VATICAN NEWS.

05/05/2018 07:30