Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maendeleo

Waraka wa Maaskofu Katoliki Malawi: Mwaliko wa ujenzi wa Malawi mpya

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi limeandika Waraka mpya kama mwaliko kwa familia ya Mungu nchini humo kuanza mchakato wa ujenzi wa Malawi mpya: inayosimikwa katika ukweli, usawa, utu, heshima na haki msingi za binadamu. - EPA

02/05/2018 06:57

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi katika Waraka wake wa kichungaji kwa mwaka 2018, unaoongozwa na kauli mbiu “Mwaliko wa Malawi Mpya” linaitaka familia ya Mungu nchini Malawi kujenga Malawi mpya inayosimikwa katika ukweli, usawa, utu na heshima ya binadamu. Changamoto hii inahitaji mabadiliko makubwa ya mawazo na mitazamo katika kukuza na kudumisha utawala bora. Ili kuweza kufanikisha azma hii, kuna haja kwa Serikali kuteuwa wafanyakazi ambao watakuwa ni mashujaa na vikolezo vya mageuzi chanya nchini Malawi kwa kuthubutu hata kufanya maamuzi machungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Hawa ni watu ambao wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha sheria kanuni za demokrasia na utawala bora, kwa kutoa hukumu ya haki inayofumbatwa katika hofu ya Mungu. Wafanyakazi kama hawa, watambue kwamba, wanaweza kuhatarisha hata usalama wa maisha yao, lakini wako makini kusimamia, kutangaza na kushuhudia ukweli bila kupepesa pepesa macho! Ni watu wanaopaswa kuwa na ujasiri wa kufikiri, kuamua na kutenda kwa haraka. Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini humo, kuujadili waraka huu ili hatimaye, kuweza kuumwilisha katika uhalisia wa maisha yao kama chachu ya ujenzi wa Malawi mpya!

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi katika Waraka wake huu mpya linapenda kujikita katika masuala ya: Demokrasia na ushiriki mkamilifu wa wananchi katika mchakato mzima wa demokrasia. Pili ni maboresho ya huduma za kijamii yaani: afya, elimu, kilimo, uhakika na usalama wa chakula nchini Malawi; miundo mbinu; pengo kubwa kati ya matajiri na maskini nchini Malawi; na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Sehemu ya tatu ni mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Malawi unaotarajiwa kufanyika mwaka 2019, changamoto ya ujenzi wa Malawi mpya itakayojikita katika mchakato wa kuwatafuta viongozi wenye sifa, tayari kuonesha dira na njia ya ujenzi wa Malawi mpya!

Utangulizi: Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi kwa kuongozwa na Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, tangu Malawi ijipatie uhuru wake wa bendera, bado kuna mamilioni ya watu wanaoteseka kutokana na umaskini, ujinga, maradhi, njaa na mmong’onyoko mkubwa wa maadili na utu wema. Rasilimali na utajiri wa asili, bado haujaleta ustawi na maendeleo yaliyokusudiwa kwa wananchi wengi wa Malawi. Maaskofu katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 25 tangu utawala wa vyama vingi ulipoanzishwa nchini Malawi, wanapenda kutoa mapendekezo yanayopania kuwa chachu ya ujenzi wa Malawi mpya!

Sura ya kwanza, Maaskofu wanasema, kuna haja ya kujenga Malawi mpya inayofumbatwa katika usawa na haki kwa wananchi wote, kwa kukuza na kudumisha demokrasia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kuliko mtindo wa sasa unaowanufaisha watu wachache peke yao. Malawi katika kipindi cha mwaka 1992 ilijikuta ikitumbukia katika ombwe na giza nene kwa wananchi kunyimwa haki ya kushiriki katika masuala ya kidemokrasia, wapinzani wa serikali wakachezeshwa “Sindimba bila kupenda”; utawala wa sheria ukaingia “mchanga”, haki na usawa vikatoweka kama ndoto ya mchana. Mfumo wa chama kimoja cha kisiasa ukashindwa kutekeleza matakwa ya familia ya Mungu nchini Malawi.

Tarehe 14 Juni 1993, Malawi ikaingia katika Mfumo wa Vyama vingi vya Kisiasa, huu ukawa ni mwanzo wa kupimana nguvu kati ya Chama tawala na vyama vya upinzani ili kuleta uwiano katika mchakato mzima wa uongozi nchini Malawi. Wananchi wakaanza kufurahia haki yao ya kisiasa kama inavyofafanuliwa na Katiba ya nchi ambayo kimsingi ndiyo Sheria Mama. Changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi kwa wakati huu ni kukuza na kudumisha demokrasia ya kweli ndani ya vyama vya kisiasa, ili maamuzi yanayotolewa yawe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wanachama wengi.

Huu ni udhaifu mkubwa ambao umeoneshwa na vyama vya kisiasa nchini Malawi. Matokeo yake: ukabila umeanza kuota mizizi; majadiliano katika ukweli na uwazi, yametoweka; nafasi muhimu zinatolewa kwa kuteuliwa na viongozi wakuu badala ya uchaguzi; matokeo ya chaguzi nyingi yamekuwa yakipangwa hata kabla ya wakati hali inayofifisha demokrasia na utawala wa sheria. Baadhi ya wanachama wenye mawazo na mielekeo tofauti hata ndani ya vyama vya kisiasa wameendelea kushutumiwa kuwa ni wasaliti; kumekuwepo na jitihada za makusudi kabisa za Chama tawala kuwanunua wapinzani ili kudhoofisha upinzani nchini Malawi.

Hakuna sera na mikakati ya maendeleo endelevu, kwani kila kiongozi anayeingia madarakani anaibuka na agenda na vipaumbele vyake na hivyo kukosa mwendelezo wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu. Huduma inayotolewa na serikali inaonekana kuwabagua wapinzani hata katika masuala msingi ya kitaifa. Bado kuna safari kubwa ya kuimarisha mchakato wa demokrasia ya vyama vingi nchini Malawi wanasema Maaskofu. Hapa kuna haja ya kufanya mageuzi makubwa ya kifikra ili kudumisha demokrasia ya kweli ndani ya vyama vya kisiasa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linakazia uhuru wa kuabudu, uhuru wa kidini na uhuru wa mtu kujieleza kadiri ya taratibu, sheria na kanuni za nchi. Inasikitisha kuona kwamba, wananchi wengi wa Malawi bado hawapati mwamko wa vyama vingi vya kisiasa na matokeo yake, wanaendelea kutumbukia katika ukabila. Mabadiliko ya Katiba ya Malawi ni hitaji muhimu kwa sasa ili kuwawezesha wananchi kujenga imani kwa viongozi wao wa kisiasa na kiserikali. Malawi inawahitaji viongozi wanaowajibika na kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Serikali, Bunge na Mahakama zitekeleze dhamana na wajibu wake bila kuingiliwa na mhimili mwingine, ili kudumisha demokrasia ya kweli.

Sehemu ya pili ya Waraka wa kichungaji kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi inajikita zaidi na zaidi katika huduma za kijamii kwa kusema kwamba, sekta ya afya inakabiliwa na matatizo na changamoto kubwa zinazopaswa kuvaliwa njuga na serikali pamoja na wadau mbali mbali ili kuokoa maisha ya watu. Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya wananchi wa Malawi wamejikita katika rushwa na ufisadi wa mali ya umma hasa katika manunuzi, kiasi kwamba, kwa baadhi ya wafanyabiashara hospitali zimekuwa ni machimbo ya dhahabu na utajiri wa haraka haraka. Hii ni saratani ya wananchi wa Malawi, inayopaswa kupatiwa tiba muafaka. Huduma ya afya nchini Malawi inapaswa kuboreshwa ili kukuza na kudumisha maisha, utu na heshima ya binadamu na wala isiwe ni kwa ajili ya watu wachache wenye “vijisenti vyao”.

Maaskofu wanaendelea kufafanua kwamba, sekta ya elimu inaendelea kudidimia kwa kiasi kikubwa, kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi isiyolingana na idadi ya walimu; mshahara kiduchu kwa waalimu kiasi cha kushindwa kukidhi mahitaji msingi ya waalimu na familia zao. Kuna uhaba mkubwa wa miundo mbinu ya kufundishia na vifaa vya shule. Mabadiliko ya mara kwa mara ya mitaala ya elimu yameathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya elimu nchini Malawi. Maaskofu wanasema, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu sanjari na kuwa na sera na mikakati ya elimu makini inayoendana na maboresho ya miundo mbinu ya majengo na vifaa vya kufundishia.

Hakutakuwepo na maendeleo endelevu, ikiwa kama rushwa na ufisadi vitaendelea kukumbatiwa nchini Malawi. Maboresho ya sera na mikakati ya kiuchumi hayana budi kuwajengea wananchi wa Malawi uwezo wa kupambana na umaskini, kwani hata baada ya kipindi cha miaka 54 ya uhuru, bado hali ya maisha ya wananchi wa Malawi ni duni sana wakati gharama ya maisha inaendelea kupaa kila kukicha! Pengo kati ya matajiri na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi nchini Malawi linaendelea kuongezeka kila kukicha! Hizi ni dalili za ukosefu wa haki jamii nchini Malawi. Matokeo yake, maskini wanaendelea kutumbukia katika umaskini na matajiri wanaendelea kupeta kwa kula kuku na bata kwa mrija!  Ili kupambana na baa la umaskini nchini Malawi, kuna haja pia ya kujikita katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwani waathirika wakubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi ni wananchi wa kawaida.

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi katika Waraka wake, sehemu ya tatu linajikita zaidi katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika kunako mwaka 2019 kama muda muafaka wa kuleta mageuzi kwa ajili ya ujenzi wa Malawi mpya! Wananchi wajengewe uwezo wa kufanya maamuzi magumu katika uchaguzi mkuu, kwa kutambua kwamba, hatima ya maisha yao, iko kwenye kura zao. Ili kuleta mageuzi ya kweli kuna haja ya kuwachagua viongozi wenye sifa zifuatazo: watu wakweli na waaminifu; viongozi wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya kuleta mageuzi ya kweli; watu wasiofunikwa na blanketi la ubinafsi, uchoyo, uchu wa mali na madaraka; watu wanaotambua na kuthamini kwamba, uongozi ni dhamana na huduma kwa ajili ya watu wa Mungu nchini Malawi; watu ambao wana malengo, dira na mwelekeo sahihi katika maisha; wanaoheshimu utawala wa sheria, ambao wako tayari kung’atuka madarakani muda wao unapomalizika.

Viongozi watakaochaguliwa wawe ni watu wanaosimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Malawi bila kugubikwa na ukabila, udini wala mahali anapotoka mtu! Kiongozi wa kweli ni yule mwenye hofu ya Mungu. Malawi inahitaji viongozi watakaosimama kidete kupambana na saratani ya rushwa na ufisadi kwa ari na moyo mkuu. Maaskofu wanakaza kusema, ujenzi wa Malawi mpya ni wajibu wa familia yote ya Mungu nchini humo. Malawi inahitaji viongozi wa shoka, watakaokuwa tayari kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa, utawala wa ubabe, upendeleo, vitisho na kejeli kwa vyombo vya mawasiliano ya jamii; watu wasioshaurika wala kukubali kukosolewa; wagumu kutoa maamuzi; viongozi wasioguswa wala kutikiswa na athari za umaskini, ujinga, maradhi na uharibifu wa mazingira kwa mamilioni ya wananchi wa Malawi.  Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linahitimisha waraka wake wa kichungaji kwa kusema, Malawi inahitaji viongozi watendaji, watakao kuwa tayari kukwamua uchumi pamoja na kuhakikisha kwamba, kila senti ya Malawi inatumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Malawi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

02/05/2018 06:57