2018-05-02 14:13:00

Kristo Yesu ni rafiki wa kweli na chanzo cha maisha mapya!


Watu wawili wasiofahamiana mmoja mwanamke na mwingine mwanaume walikuwa wamekaa katika benchi moja katika bustani ya mapumziko. Yule mwanamke alikuwa anasoma Biblia, habari juu ya Yona. Yule mwanaume aliona sehemu ya Maandiko Matakatifu aliyokuwa akisoma yule mwanamke. Baada ya ukimya fulani yule mwanaume akamuuliza yule mwanamke kama kweli anaamini kuwa Yona alikaa katika tumbo la samaki kwa siku tatu. Yule mwanamke akamwambia kuwa Biblia inatuambia hivyo. Yule mwanaume akamuuliza je na kama si kweli hivyo? Yule mwanamke akamwambia kuwa atamwuliza nabii Yona watakapokutana mbinguni. Yule mwanaume akamwambia na je kama nabii Yona hayuko mbinguni itakuwaje? Yule mwanamke akamjibu basi utamwuliza wewe.

Hakika katika mfano huu tunaona imani ya ajabu ya yule mama, imani kubwa na iliyo na msingi imara. Bahati mbaya sisi tunataka kujua kila kitu hasa kihusucho Mungu, na mbaya zaidi tunataka tujue tunavyotaka sisi.  Meister Eckhart anasema baadhi ya watu wanataka kumwona Mungu kwa macho kama wanavyomwona ng’ombe na kumpenda Mungu kama wanavyopenda ng’ombe wao kwa kiasi cha maziwa, jibini na faida wanayoipata toka kwa ng’ombe huyo.

Pengine namna hii ya kufikiri ndiyo inaweza kuwa sababu au kikwazo kwa imani ya wengi. Je, ufahamu wetu wa kile alichofanya Kristo ukoje? Je, mahusiano yetu na Kristo yakoje? Bwana na mtumwa au rafiki na rafiki? Wakati mwingine mtazamo uko wa bwana na mtumwa na kwa kweli katika aina hii ya urafiki, uhusiano unakita zaidi kwenye woga. Wengine ni uhusiano wa urafiki na ukaribu unakuwepo. Yesu anasema mwenyewe – Yoh. 15, 15 – siwaiti tena watumwa, kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake, lakini ninyi nimewaita rafiki, kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu, nimewaarifu.

Kwa maelezo haya yaonekana wazi jinsi Bwana Yesu anavyotaka uhusiano wetu uwe. Maisha ya ukristo yatuita katika ukuaji – tunapoanza maisha ya imani – uhusiano wa mtumwa na bwana unaonekana lakini kadiri tunavyozidi kukua na kukomaa katika imani mahusiano yetu yanabadilika – yanajengeka mahusiano ya kirafiki kwa vile tunashirikishwa pia siri za ufalme wa Mungu.  Injili ya leo yatupa changamoto kubwa – kuangalia imani yetu na ukomavu wetu kama unavyoonekana katika mapendo kati yetu, mahusiano yetu na ushirikiano wetu.

Ni kwa kiasi gani tunaifahamu hiyo siri ya Mungu ambayo Kristo ametufunulia? Kiasi kwamba tunakuwa rafiki zake Kristo? Hakika ufahamu wa kina wa Kristo ni nani na kile alichofanya kwa ajili yetu unageuza mahusiano yetu na Mungu Baba na pia maisha yetu ya ushuhuda – Yoh. 15,7 – ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo nanyi mtatendewa. Pia tunasoma katika Yoh. 15,16 – si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi, nami nikawaweka mwende mkazae matunda, na matunda yenu yapate kukaa, ili kwamba lolote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.

Hakika Mwenyezi Mungu anategemea na anatarajia makuzi toka kwetu. Kama vile mtoto azaliwavyo na kukua vivyo hivyo nasi tuna changamoto ya kukua na kuendelea mbele katika ushuhuda wa imani yetu. Hii ofa ya urafiki wa Mungu kwetu ituwajibishe na kutufikirisha sana. Eti Mwenyezi Mungu anakuwa rafiki yetu. Sote twajua sifa za urafiki. Waswahili husema - akufae kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli. Wafaransa husema – rafiki mwaminifu ni taswira ya Mungu. Waitaliano husema – ampataye rafiki wa kweli  amepata dhahabu. Hii ni baadhi tu ya mifano inayojaribu kuonesha umaana na umuhimu wa urafiki. Urafiki wa kweli hudumu, hubaki, hukua na kuzaa matunda - kama tunavyosoma kutoka Yoh. 15,7 – tunaalikwa tukae ndani yake Kristo na kuzaa matunda.

Huweza kutokea pia baadhi ya rafiki wakakosa uaminifu, wakachezea urafiki huo kwa ajili ya faida yao wenyewe. Namna kuu ya kujibu upendo huo wa Mungu kwetu ni kubaki katika pendo lake. Maana yake kutimiza mapenzi yake Baba – Yoh. 15,14 – ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Kuwa rafiki wa kweli wa Mungu ni kutimiza amri zake. Imani ya mama yule katika mfano itufikirishe sana – anaamini na hana wasiwasi juu ya ukuu wa Mungu. Ana uhakika wa kwenda mbinguni na ndiyo maana anaweza kujibu wazi – jibu kamili kama upo wasiwasi kwamba Yona alibaki katika tumbo la samaki kwa siku tatu nitakupatia nitakapokutana naye ana kwa ana. Yule mama ana uhakika wa kwenda mbinguni. Mara nyingi kuwa na wasiwasi na mashaka au kutokujiamini katika maisha kunasababisha kukosa mwelekeo mzuri katika utendaji wetu. Katika Yoh. 15,15 – Yesu anasema wazi siwaiti tena watumwa bali rafiki.

Yesu anatuambia leo kaeni katika pendo langu. Hakika ni mwaliko mtakatifu na mwaliko unaotuwajibisha sana. Katika somo II - 1Yoh. 4,8 tunasoma hivi; - yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Kwa kifupi upendo wa kweli watoka kwa Mungu. Mwenye kupenda kweli na vizuri ni lazima amjue na kumpenda Mungu kwanza. Sisi wanadamu tunashiriki utukufu na ukuu wa Mungu kwa neema. Sisi sio Mungu. Mungu ni pendo. Hali yake ni pendo. Pendo lake kwetu sisi ni zawadi. Mwanadamu anaalikwa kupokea zawadi hii na kuiweka au kuiishi katika maisha yetu na mahusiano yetu. Kwa njia yake Kristo sisi tumeshirikishwa pendo lake Mungu. Tunayo amri, wajibu na kila sababu ya kuambukizana pendo hili la Kimungu kati yetu. Huo ndiyo mwito wa Kristo leo.

Kitokacho mbinguni ni kitakatifu. Ni lazima kienezwe duniani kote. Pendo la Mungu linakuja kwetu kwa njia ya Mwanawe. Mwana naye anaeneza pendo hilo kwetu. Sisi tunalipeleka kwa wenzetu.  Haya basi nawaamuru ninyi, mpate kupendana. Ndivyo ilivyo katika Injili leo. Tendo la kupenda au kupendana kati yetu sisi wafuasi wake Kristo ni amri na si hiari. Tumesikia katika Injili mafundisho ya Yesu juu ya amri yangu. Ni ipi hiyo? Jibu lake liko wazi katika somo lenyewe la Injili ya leo. Amri yangu ndiyo hii – mpendane kama nilivyowapenda ninyi. Naye Mtume Paulo anakazia mwaliko katika Rum. 13,8 – akisema – msiwiwe na mtu cho chote isipokuwa kupendana, kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria.

Tumsifu Yesu Kristo,

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.