2018-05-01 13:36:00

Siku kuu ya Wafanyakazi Duniani na changamoto zake kwa mwaka 2018


Siku kuu ya Wafanyakazi Duniani, inayoadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo Mei Mosi, iwe ni fursa ya kukuza: uhuru na ushiriki mkamilifu wa wafanyakazi katika mchakato wa uzalishaji mali na utoaji wa huduma kwa kuhamasisha kipaji cha ugunduzi na kuimarisha sheria za kazi, utawala bora na usalama kazini pamoja na kuhakikisha kwamba, kazi inakuwa ni sehemu ya utimilifu wa ut una heshima ya binadamu. Siku kuu ya Wafanyakazi imewekwa chini ya ulinzi wa Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi. Siku kuu hii ndani ya Kanisa ilianzishwa kunako mwaka 1955 na Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili. Mababa wa Kanisa daima wamekuwa wakikazia tunu msingi za kazi, ili mtu asiwe mzigo kwa wengine, lakini afanye kazi hivyo kwamba aweze kuishi na hatimaye kujitosheleza kwa mahitaji yake msingi.

Watu wanapaswa kuepuka tabia ya kukaa vijiweni na kusogoa siku nzima hali ambayo inaunda mazingira ya dhambi. Mwili unapaswa kushikishwa adabu kwa kufanyishwa kazi, kwa kukubali ugumu na changamoto za kazi kama sehemu ya toba na wongofu wa ndani. Wafanyakazi wanapaswa kupata mshahara unaokidhi mahitaji yao msingi pamoja na familia zao, ili waweze pia kujenga umoja na mshikamano kwa kuwasaidia wengine! Ikumbukwe kwamba, kazi ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, ni utambulisho na utimilifu wa utu na heshima yake. Kazi inasaidia kuboresha ulimwengu ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi na kwa mantiki hii, kazi inakuwa ni sehemu ya Fumbo la Umwilisho! Kazi ni mkombozi na toba katika maisha ya waamini inayomwongoza na kumwelekeza mtu katika njia ya utakatifu wa maisha!

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani kwa Mwaka 2018 linakazia: utu na heshima ya wafanyakazi kwa kuhakikisha kwamba, vizingiti na vikwazo vinavyodhalilisha heshima ya binadamu vinaondolewa kwa kujikita katika uhuru, ubunifu, umoja, upendo na mshikamano mambo yanayoweza kuongeza tija katika mchakato mzima wa uzalishaji na utoaji huduma. Changamoto ya ukosefu wa fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana inapaswa kuvaliwa njuga ili kuwajengea vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi sanjari na kudumisha ulinzi na usalama katika maeneo ya kazi ili kuepukana na ajali kazini ambazo zinasababisha majonzi na mateso makubwa kwa familia na jamii katika ujumla wake.

Askofu mkuu Cesare Nosiglia wa Jimbo kuu la Torino katika mkesha wa Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, amekazia umuhimu wa uwepo wa Mungu katika hija ya maisha ya mwanadamu kama chemchemi ya matumaini hata pale matumaini yanapooneka kufifia na kutoweka kama ndoto ya mchana! Kwa ujumla, wafanyakazi wengi wametikiswa na myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa kiasi hata wanakosa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi!

Hali ngumu ya uchumi imepelekea wafanyabiashara kufunga shughuli zao na hivyo kusababisha watu wengi kukosa fursa za kazi na ajira, matokeo yake ni kushuka kwa hali na ubora wa maisha. Katika hali na mazingira kama haya, waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano kama njia ya kupambana na hali pamoja na mazingira yanayowaandama, huku wakijitahidi kuwajengea pia vijana matumaini ili wasikate tamaa na kutokomea kule kusikojulikana, kwani huko watamezwa na malimwengu na kukiona cha mtema kuni! Hapa anasema Askofu mkuu Cesare Nosiglia kila mwananchi anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jambo la pili ni kuwekeza katika vitega uchumi kwa kuzingatia kanuni maadili, utu, haki msingi za binadamu, daima binadamu na mahitaji yake msingi pamoja na familia akipewa kipaumbele cha kwanza. Wachunguzi wa mambo wanasema, mshahara ni dawa inayoratibu ugonjwa wa umaskini duniani, lakini hauponyeshi umaskini. Biashara na vitega uchumi makini ndiyo mwarobaini wa umaskini duniani.

Hapa, Askofu mkuu Cesare anakazia pia kanuni sheria, maadili na utu wema katika maeneo ya kazi, kwani vinginevyo, kazi inaweza kuwa pia ni chanzo cha nyanyaso na dhuluma kwa wafanyakazi, kiasi hata cha “kutia mchanga” utu na heshima yao kama binadamu! Ikumbukwe kwamba, binadamu daima ni kiumbe jamii, lakini kutokana na athari za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, watu wengi wamejikuta wakitumbukia katika upweke hasi na magonjwa ya afya ya akili kama vile sonona. Umoja, udugu na mshikamano ni mambo muhimu katika kupambana na changamoto mamboleo!

Umuhimu wa kazi, haki msingi, utu na heshima ya wafanyakazi ni mambo msingi katika kujenga mafungamano ya kijamii. Mshahara unaokidhi mahitaji msingi ya wafanyakazi pamoja na familia zao, ingekuwa ni ushuhuda wa haki jamii, lakini, ukweli wa mambo ni kwamba, kuna watu ambao wanalipwa mshahara usioweza kutosheleza mahitaji msingi ya familia zao. Katika kupambana na umaskini, haki jamii inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee, ili wafanyakazi waweze kufurahia jasho la kazi zao. Ukosefu wa kazi na fursa za ajira ni janga la kitaifa na kimataifa, linalohitaji wadau mbali mbali kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na vitega uchumi endelevu. Lengo kuu ni kuwawezesha wafanyakazi kutambua kwamba, kazi ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, ni utambulisho na utimilifu wa utu na heshima yake. Kazi inasaidia kuboresha ulimwengu ili uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi na kwa mantiki hii, kazi inakuwa ni sehemu ya Fumbo la Umwilisho! Kazi ni mkombozi na toba katika maisha ya waamini inayomwongoza na kumwelekeza mtu katika njia ya utakatifu wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.