2018-04-28 16:04:00

Maaskofu Katoliki Nigeria: "Kama Rais ameshindwa kazi" ang'atuke!


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria ambalo linafanya hija ya kitume mjini Vatican kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na waandamizi wake, limesikitishwa na kuhuzunishwa sana na mauaji ya mapadre wawili: Padre Joseph Gor , Padre Felix Tyolaha pamoja na waamini 15 huko kijijini Mbalom. Maaskofu Katoliki Nigeria kwa kauli moja wanasema, ikiwa kama Rais Muhmmadu Buhari hawezi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha usalama wa maisha ya raia wake, ni afadhali “kujiuzuru” kabla nchi haijatumbukia zaidi katika majanga na maafa yanayoweza kudhibitiwa.

Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, vikundi vya kigaidi nchini Nigeria, vimegeuza Ukanda wa Kati kuwa ni makaburi ya watu wasiokuwa na hatia. Kumekuwepo na kinzani na mgogoro kati ya Jamii ya wakulima na wafugaji nchini Nigeria, hali ambayo imepelekea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia pamoja na uharibifu mkubwa kwa mali ya zatu. Wananchi wengi nchini Nigeria wanaishi katika hofu na mashaka kama ilivyokuwa kwa Mapadre waliouwawa kinyama, kwani wangeweza kutafuta hifadhi ya maisha yao sehemu nyingine, lakini kama kielelezo cha wachungaji wema, waliamua kubaki na kuendelea kutoa huduma kwa waamini wao hata pale usalama wa maisha yao ulipokuwa hatarini.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria limeitupia lawama na shutuma kali sana Serikali kuu ya Nigeria pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo hadi sasa vimeshindwa kudhibiti ulinzi na usalama wa raia na mali zao na matokeo yake, mauaji ya kutisha, utekaji nyara na ubakaji wa wanawake na wasichana yamekuwa ni mambo ya kawaida nchini Nigeria. Kwa muda wa miaka miwili, Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria pamoja na wapenda amani nchini humo wamemwomba Rais Rais Muhmmadu Buhari kufumua uongozi wa vikosi vya ulinzi na usalama na kuvipanga upya kwani wengi wao wananuka harufu ya rushwa na ufisadi. Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria halina imani tena na vyombo vya ulinzi na usalama nchini humo. Ikiwa kama wananchi wanakosa imani na Rais wao, basi atambue kwamba, hapo anawajibika kimaadili kuachia ngazi haraka iwezekanavyo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.