2018-04-28 15:43:00

Askofu mkuu Protase Rugambwa anatembelea Namibia na Botswana


Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kuanzia tarehe 1-12 Mei 2018 anafanya safari ya kichungaji kwa kutembelea Namibia na Botswana, ili kujifunza zaidi maisha na utume wa Makanisa mahalia; kuangalia: matatizo, changamoto na mafanikio yaliyokwisha kupatikana katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; kuwatia shime wamisionari pamoja na mihimili yote ya uinjilishaji kuendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiini cha furaha ya Injili!

Akiwa nchini Namibia, Askofu mkuu Rugambwa, hapo tarehe 5 Mei 2018 anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu na kumweka wakfu Askofu mteule Willem Christiaans, OSFS, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Keetmanshoop, lililoko nchini Namibia. Kabla ya uteuzi huu Askofu mteule Willem Christiaans alikuwa ni Msimamizi wa kitume wa Jimbo Katoliki la Keetmanshoop. Alizaliwa tarehe 12 Februari 1961 huko Gabis, Karasburg, Jimbo Katoliki la Keetmanshoop. Baada ya masomo na majiundo yake ya kitawa akaweka nadhiri zake za daima tarehe 23 Januari 1988 na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre 10 Desemba 1988.

Katika maisha na utume wake kama Padre, Askofu mteule Willem Christiaans amewahi pia kuwa ni mkurugenzi wa wanafunzi wanaojiandaa kuingia hatua ya Unovisi Shirikani kwake; Mkurugenzi wa wasomi wa Shirika, Mkuu wa Shirika Kikanda tangu mwaka 1993 hadi mwaka 2005, kwa vipindi vitatu mfululizo. Kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2013 amekuwa Paroko, Makamu wa Askofu, Mkurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa na tarehe 26 Julai 2017 akateuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Keetmanshoop, lililoko nchini Namibia.

Ratiba elekezi ya ziara ya kikazi ya Askofu mkuu Protase Rugambwa inaonesha kwamba, Mei Mosi, 2018 atawasili mjini Pretoria, Afrika ya Kusini na kupata mapumziko mafupi kwenye Ubalozi wa Vatican kwa ajili ya Afrika ya Kusini, Namibia, Botswana, Lesotho na Swaziland. Tarehe 2 Mei 2018 Askofu mkuu Rugambwa atasafiri kutoka Pretoria kuelekea Namibia na jioni atatembelea Hospitali kuu ya Jimbo kuu la Windhoek nchini Namibia. Tarehe 3 Mei 2018 atafanya mazungumzo na Mashirika ya Kitawa nchini Namibia na baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la St. Mary.

Tarehe 5 Mei 2018 ataongoza Ibada ya Misa Takatifu na kumweka wakfu Askofu mteule Willem Christiaans kuwa Mchungaji mkuu wa Jimbo Katoliki la Keetmanshoop na jioni atakutana na kuzungumza na wakleri pamoja na kutembelea nyumba za watawa mahalia. Tarehe 7 Mei 2018, Askofu mkuu Rugambwa atatembelea Seminari kuu ya Kitaifa ya St. Charles Lwanga na hapo ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na baadaye jioni atarejea tena mjini Pretoria ili kukutana na Bodi ya Wakurugenzi Watendaji wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika. Tarehe 8 Mei 2018, Askofu mkuu Rugambwa atatembelea Jimbo Katoliki la Gaborone na kuzungumza na viongozi wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume nchini humo.

Tarehe 9 Mei 2018 atapata nafasi ya kuzungumza na Makatekista ambao kimsingi ndio watendaji wakuu katika mchakato mzima wa uinjilishaji Barani Afrika na baadaye atakutana pia na Bodi ya Washauri wa Jimbo Katoliki la Gaborone ambalo kwa sasa liko wazi. Jioni atatembelea Chuo cha St. Joseph, Kgale na baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la “Christ the King”. Tarehe 10 Mei 2018, Askofu mkuu Protase Rugambwa atasafiri kuelekea Jimboni Francistown, Kaskazini mwa Bostwana, mahali ambako bado uinjilishaji uko katika hatua za awali kabisa! Atatembelea Parokia kadhaa na baadaye kuadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni, ambayo pia ni Siku ya 52 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni inayoongozwa na kauli mbiu “... Ukweli utawaweka huru: Habari za kughushi na Uandishi wa Habari wa Amani.” Itakumbukwa kwamba, ingawa Wakristo ni sehemu ya idadi kubwa ya waamini nchini Namibia na Bostwana, lakini, waamini wa Kanisa Katoliki ni wachache sana. Askofu mkuu Protase Rugambwa, tarehe 12 Mei 2018 anatarajiwa kurejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake kwa Kanisa la Kiulimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.