2018-04-25 15:21:00

Papa Francisko aunga mkono juhudi za Korea kukutana na kujadiliana!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake, Siku ya Jumatano, tarehe 25 Aprili 2018, ameyaelekeza mawazo yake nchini Korea, ambako Ijumaa, tarehe 27 Aprili 2018 kunafanyika mkutano wa Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini huko Panmunjeon. Viongozi wakuu: Rais Moon Jae-in na Rais Kim Jong Un wanatarajiwa kushiriki kwa ukamilifu. Mkutano huu anasema Baba Mtakatifu ni fursa makini ya kuanzisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kujikita katika upatanisho na hatimaye, kujenga na kudumisha udugu na amani huko Korea na ulimwenguni kote!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wananchi wa Korea wana kiu ya kutaka kuambata amani ya kudumu na kwamba, anapenda kuchukua fursa hii, kuwahakikishi sala zake na uwepo wa Kanisa katika ujumla wake, katika mchakato huu wa majadiliano ya amani na udugu. Vatican inapenda kuunga mkono, kusindikiza na kuimarisha juhudi kama hizi, ili kujenga na kudumisha kesho iliyo bora zaidi na matumaini ya watu wanaokutana ili kudumisha urafiki kati ya watu. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime viongozi wa kisiasa wenye dhamana ya moja kwa moja kuwa na ujasiri na matumaini, daima wakijitahidi kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani, daima wakijielekeza katika njia inayopania kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.