2018-04-25 14:01:00

Mapadre wawili na waamini 16 wameuawa na kundi la kifulani Nigeria!


Watu 18 wameuawa katika  Kanisa katoliki nchini Nigeria. Moses Yamu, Msemaji wa Polisi katika jimbo la Benue amesema shambulizi hilo la kikatili lilitokea alfajiri ya Jumanne 24 Aprili 2018 katika kijiji cha Ayar Mbalom, eneo la Gwer Mashariki ambapo watu wengine kadhaa walijeruhiwa pia.

Msemaji wa Polisi huyo amethibitisha kuwa, watenda jinai hao wanao aminika kuwa wafugaji wa kabila la Fulani, walilivamia Kanisa Katoliki la Mtakatifu Ignatius huku wakiwa wamejizatiti kwa bunduki na kuwamiminia risasi watu waliokuwa kwenye Kanisa hilo, na kuua 16 miongoni mwao wakiwemo mapadri wawili. Hujuma hii inajiri chini ya wiki moja baada ya mashambulizi pacha ya mabomu kuua waumini watatu wa Kiislamu huku wengine tisa wakijeruhiwa wakiwa ndani ya msikiti katika mji wa Bama jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Aidha mapema mwaka huu, gaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram aliyejifunga bomu mwilini alijiripua na kuua watu wasiopungua 14 ndani ya msikiti mmoja katika mji wa Gamboru ulioko kwenye jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria. Kundi hilo lililoanzisha uasi mwaka 2009 kwa madai ya kupinga elimu zinazotoka Magharibi huwa kwa kawaida linawatumia watu wanaojiripua wakiwemo wanawake na wasichana kufanya mashambulio ya aina hiyo, katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama misikitini, makanisani na masokoni.

Sr Angela Rwezaula 
Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.