2018-04-23 14:32:00

Vipaumbele vya Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo!


Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, PCPM, iliyoundwa mwezi Machi 2014 na Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni imehitimisha mkutano wake wa mwaka, kwa kuendelea kujizatiti kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kumshauri Baba Mtakatifu mbinu za kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia zinazodhalilisha utu na heshima yao pamoja na kuajengea Makanisa mahalia uwezo wa kupambana na vitendo hivi katika maeneo ya Makanisa. Wajumbe wamepata fursa ya kusikiliza “Jopo la Washauri wa Waathirika wa Nyanyaso za Kijinsia” kutoka Uingereza na Wales. Wajumbe hawa wamefurahishwa kwa mwelekeo wa sasa unaotumiwa na Kanisa kwa kuwasikiliza kwa makini, ili kuwajengea uwezo wa kupambana na hali yao.

Tume pia imepongezwa kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa waathirika, hali ambayo itawasaidia kujenga na kudumisha mtandao wa waathirika wa nyanyaso za kijinsia, ili kushirikisha: uzoefu, mang’amuzi, uchungu na fadhaa wanazokabiliana nazo katika maisha. Kwa njia hii, hata sauti ya waathirika inaweza kusikika katika maisha na utume wa Kanisa. Wajumbe wa Tume wamesikiliza pia uchunguzi uliofanywa na Tume Dhidi ya Nyanyaso za Kijinsia kutoka Australia. Tume hiyo imekita upembuzi wake kutoka kwenye Itifaki ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watoto na umuhimu wa Jumuiya za Kidini katika kutibu na kuganga makovu ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo.

Wajumbe pia, walipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwa faragha. Baba Mtakatifu ameonesha nia ya kuridhia Katiba ya Tume ya Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia, PCPM. Vipambele vya Tume ambayo imegawanyika katika makundi kwa wakati huu ni: kuendelea kuwasilikiza waathirika wa nyanyaso za kijinsia; elimu na majiundo makini; sheria, kanuni na taratibu za kufuatwa. Makundi haya yanaendelea kufanya tafiti na miradi ili kulinda na kulitunza Kanisa la Kristo linalopaswa kuwa ni nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.