2018-04-17 09:03:00

Kenya: Changamoto: uchu wa madaraka, rushwa, umaskini na ajira


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika ujumbe wake wa Pasaka kwa Mwaka 2018 uliotolewa hivi karibuni, na kuongozwa na kauli mbiu “Tenda kwa haki, penda rehema na kwenda kwa unyenyekevu na Mungu wako”: unachambua kwa kina na mapana hali ya kisiasa ambayo imefungua ukurasa mpya nchini humo; hali mbaya ya kiuchumi kutokana na ongezeko la umaskini miongoni mwa wananchi wa Kenya. Maaskofu wanasema, saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma inaendelea kukua na kupanuka kila kukicha; kuna uvivu na uzembe unaowafanya baadhi ya wananchi kutafuta njia ya mkato katika maisha; pamoja na huduma hafifu inayotolewa na Jeshi la Polisi nchini Kenya. Maaskofu wamedadavua kuhusu utawala wa sheria, mambo yanayotishia elimu pamoja tunu msingi za maisha ya ndoa na familia!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika ujumbe wake wa Pasaka linaiombea Kenya baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu; ustawi, maendeleo, umoja na mshikamano. Maaskofu Katoliki Kenya wanasikitika kusema kwamba, mchakato wa uchaguzi mkuu uliohitimishwa hivi karibuni umeligawa taifa; umedumaza uchumi na baadhi ya wananchi wameathirika kutokana na machafuko na vurugu za kisiasa, changamoto kwa sasa ni kuanza kujikita katika mchakato wa uponyaji na upatanisho wa kitaifa; tiba kwa waathirika na fidia kwa watu waliopoteza mali zao, ili kupata tena ujasiri wa kuanza tena upya!

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linapongeza juhudi zilizowakutanisha Rais Uhuru Kenyatta na Bwana Raila Odinga, ingawa hawajui kwa kina yale yaliyojadiliwa na viongozi hawa wawili waliokuwa wanapingana kiasi cha kuhatarisha amani, umoja na mafungamano ya familia ya Mungu nchini Kenya, lakini kwa sasa jambo la msingi ni kuendelea kujikita katika upatanisho wa kudumu, ilikujenga umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kukuza fursa sawa kwa wananchi wote sanjari na kuendeleza mchakato wa upatanisho unaofumbatwa katika: majadiliano, haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Umefika wakati wa kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kamwe, uchaguzi mkuu usitumiwe kuwa ni “blanketi la uchu wa mali na madaraka” kama ilivyojitokeza katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 na mwaka 2017. Kanisa linapenda kuendeleza mchakato wa majadiliano ili kuwajengea wananchi uwezo wa kuwajibika kikamilifu katika kukuza na kudumisha: haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Ni wakati muafaka wa kufanya upembuzi yakinifu ili kuangalia ikiwa kama mfumo wa uchaguzi nchini Kenya unakidhi viwango vya kuwapata viongozi bora zaidi.

Kuna hitaji kubwa na la haraka la kuendelea kuwekeza zaidi katika taasisi za kidemokrasia, kwa kuendelea pia kuimarisha mchango wa upinzani kama sehemu ya utawala bora. Ni jambo la kushangaza kuona kwamba, viongozi waliochaguliwa hivi karibuni, badala ya kuchuchumilia shida, changamoto na fursa za maendeleo kwa wananchi wao wanaanza kufanya kampeni za uchaguzi mkuu kwa mwaka 2022, kielelezo cha ubinafsi wa hali ya juu kabisa. Rasilimali fedha na vitu itumike vyema kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Kenya, kwa kuepuka: ukabila na udugu katika masuala ya ajira na utumishi wa umma.

Ongezeko kubwa la umaskini wa hali na kipato nchini Kenya ni jambo ambalo kamwe haliwezi kukubalika, wakati ambapo kuna watu wachache kabisa wanaoendelea kufurahia matunda ya uhuru kwa kula “kuku na bata kwa mrija”. Maaskofu wanaitaka Serikali kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kupambana na umaskini, ili kuboresha hali na maisha ya wananchi wengi wa Kenya. Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana ni chanzo kikuu cha vijana hawa kujihusisha na biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya na utumwa mamboleo; uhuni pamoja na kujiunga na vikundi vya kigaidi ambavyo ni hatari kwa usalama, maisha na mafungamano ya kijamii. Mazao ya wakulima nchini Kenya yanapaswa kulindwa dhidi ya ushindani usiokuwa na tija wala mafao kwa wakulima wa Kenya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasikitika kusema, kwamba, saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma inaendelea kukua na kupanuka kwa haraka sana, kiasi kwamba, imekuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya wananchi wa Kenya. Kwa mtindo huu, Kenya itaendelea kutumbukia katika ombwe la umaskini mkubwa! Kenya inahitaji viongozi shupavu watakaosimama kidete kupambana na rushwa na ufisadi; kwa kukuza na kudumisha haki na usawa katika huduma bila ya kulazimika kutoa rushwa! Umefika wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa uaminifu, ukweli na uwazi katika mifumo yote ya elimu pamoja na kupambana na rushwa kwa macho makavu kabisa! Maaskofu wanalitaka Jeshi la Polisi kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuzingatia kanuni sheria na taratibu za nchi, daima utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza. Jeshi la Polisi liko kwa ajili ya kulinda usalama wa raia na mali zao na wala si kwa ajili ya kuwanyanyasa! Jeshi la Polisi, linapaswa kujisafisha kwani linatuhumiwa sana na wananchi wa kuogelea katika rushwa na ufisadi hasa katika masuala ya wizi wa mifugo.

Baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakifanya biashara ya silaha, kiasi hata cha kuhatarisha usalama wa raia na mali zao. Ajali barabarani zinapaswa pia kuangaliwa ili kuokoa maisha ya wananchi wa Kenya sanjari na kuboresha huduma katika miundo mbinu ya barabara, sekta ya afya  na elimu makini! Serikali inapaswa kuzingatia kanuni sheria za utawala bora na utawala wa sheria; kwa kuendelea kujikita katika kanuni maadili, utu wema, uadilifu na weledi. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linapongeza juhudi za Serikali kwa kuanza kuboresha miundo mbinu ya barabra, lakini linasema, rasilimali fedha ya wananchi itumike vyema.

Migomo na maandamano ya wanafunzi katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ni hatari sana kwa ukuaji wa mfumo wa elimu makini nchini Kenya. Maandamano na migomo inabomoa uchumi na kukuza umaskini, kumbe, kuna haja ya kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi kama njia ya kutafuta suluhu ya matatizo na changamoto za maisha. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasema, litaendelea kujizatiti kukuza na kudumisha tunu msingi za Injili ya familia, utu na heshima ya binadamu, kwa kuwataka wanafamilia, serikali na jamii kuwajibika kikamilifu ili kulinda na kutetea familia. Kanisa linapinga kwa nguvu zote ndoa za watu wa jinsia moja au ndoa za wake wengi, kwani mifumo kama hii ni kinyume kabisa cha mpango wa Mungu katika maisha ya familia ya binadamu. Huu ni wakati wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za familia. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linahitimisha Ujumbe wake wa Pasaka kwa mwaka 2018 kwa kuwataka wananchi wote wa Kenya kuungana, ili kujenga nchi yao, ili kwamba, utukufu wa Kenya na matunda yake yaweze kuwafikia wananchi wote wa Kenya wanaoyapokea kwa moyo wa shukrani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.