2018-04-14 16:50:00

Yaliyojiri Askofu mkuu Isaac Amani Massawe aliposimikwa Arusha


Mafundisho Jamii ya Kanisa yanakaza kusema, mtu nafsi ndiye msingi na lengo la maisha ya kisiasa. Akiwa amejaliwa hulka ya kufikiri, mtu mwenyewe anawajibika kwa maamuzi yake na ana uwezo wa kufuatilia mambo yaliyo ya maana kwa maisha yake binafsi na kwa jamii. Akiwa mrithi kwa Mwenyezi Mungu na kwa wengine katika sifa na tabia zimtambulishazo. Ni katika mahusiano tu na Mwenyezi Mungu na wengine ndipo mtu anafikia ukamilifu wake wote. Hii inamaanisha kwamba mtu aliye wa hulka yake kiumbe wa kijamii na wa kisiasa “maisha ya kisiasa sio kitu cha ziada” isipokuwa ni sehemu ya wigo muhimu na usioweza kufutika. Jumuiya ya Kisiasa asili yake ni katika maumbile ya mwanadamu ambaye dhamiri yao inawadhihirisha na kuwaunganisha kutii mpango ambao Mungu ameuandika katika viumbe wake wote. Huu ni mpango wa kimaadili na kidini. Dini na siasa vinapaswa kushirikiana ili kutetea na kuhamasisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake.

Askofu mkuu Isaac Amani Massawe katika shukrani zake kwa familia ya Mungu nchini Tanzania iliyohudhuria Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kusimikwa kwake, hapo tarehe 8 Aprili 2018 amesema bila kupepesha macho kwamba, hakuna sababu ya kuogopana, Kanisa na siasa havichangamani, lakini vinasaidiana na kukamilishana. Hata wakleri kutoka Tanzania wameshiriki katika Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, kumbe, wakleri nao ni sehemu ya wananchi na wazalendo wa Tanzania. Kama Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanavyosema: uchungu na fadhaa; furaha na matumaini ni uchungu na fadhaa ya wakleri wa Tanzania.

Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazoendeshwa na kutekelezwa na Kanisa nchini Tanzania zinawaguswa watanzania wote. Ili kufanikisha huduma makini na endelevu kwa watanzania wote anasema Askofu mkuu Isaac Amani Massawe ni katika kujenga na kukuza utamaduni wa: kushirikiana, kusikilizana, kujadiliana katika ukweli na uwazi pasi na utengano wa kidini, kiitikadi na kichama. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Tanzania inajenga mazingira ya umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa ili kukuza na kudumisha amani, ambayo inapaswa kuwa ni ushindi wa taifa la Tanzania.

Watanzania hawana budi kushikamana na kuendelea kujizatiti zaidi na zaidi katika kutafuta na kudumisha: hekima, umoja na amani kama nguzo za taifa! Hii ni sehemu muhimu sana ya Wimbo wa Taifa. Umoja na mshikamano ujengwe na kudumishwa katika vyama pamoja na kuwashirikisha raia wote wa Tanzania kwa lengo kuu ni ustawi, maendeleo na mafaniko ya watanzania wote! Tanzania ikifanikiwa kutekeleza haya, ndio ushindi mkubwa kwa wote! Tanzania inapaswa kujenga na kudumisha siasa safi inayounganisha vyama vyote na kutoa nafasi kwa kila mtanzania kuchangia ustawi na maendeleo ya wote! Ili kufikia lengo hili anasema Askofu mkuu Isaac Amani Massawe kuna haja ya kujenga utamaduni wa kuvumiliana, kusameheana, kusikilizana na kuelewana! Kwa njia hii, Tanzania itakuwa ni taifa kubwa, kwani Mwenyezi Mungu amewatajirisha sana watanzania kwa rasilimali vitu na watu!

Kwa upande wake Askofu mkuu Marek Solczyński, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, ameitaka familia ya Mungu nchini Tanzania kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa na kamwe isiruhusu kutokea kwa nyufa kwa misingi yoyote ile, iwe ni ya kidini, kisiasa au kijamii. Watanzania watafute na kuambata mambo msingi yanayowasaidia kutajirishana kama ndugu wamoja licha ya tofauti zao za kidini, kiitikadi na kisiasa. Kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi, baraka, amani na maendeleo yanaweza kupatikana. Watanzania wajitahidi kujenga na kudumisha dhamiri safi, kwa kutakiana na kutendeana mema, kwa kuweka mazingira bora zaidi, yatakayosaidia watanzania wa leo na kesho kufurahia matunda ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati!

Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu wakati wa Masifu ya Jioni kwa ajili ya kumpokea rasmi Askofu mkuu Isaac Amani Massawe baada ya kukabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Arusha, tayari kuanza dhamana na wajibu wake wa kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu Jimbo kuu la Arusha, Askofu Mkuu mstaafu Lebulu alitoa mahubiri, ambayo kweli ni muhtasari wa maisha na utume wake kama: Padre aliyelitumia Kanisa kwa muda wa miaka 50 na Uaskofu kwa takribani miaka 40. Ameikumbusha familia ya Mungu Jimbo kuu la Arusha kwamba, wao ni wa ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe!

Askofu mkuu Mstaafu Lebulu amekaza kusema, ukoo mteule ni watu ambao wamekombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu, aliyejitoa mwenyewe Msalabani, awe sadaka safi iletayo amani na kutimiza mafumbo ya ukombozi wa watu na hivyo, kuunganishwa kiasi kwamba, wanashibana na Kristo. Wao ni makuhani wa Kristo Mfalme ambaye ufalme wake ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Dhamana na utume wa makuhani ni kuwaunganisha watu wa Mungu yaani: wakleri, watawa na waamini walei, ili kuwa wamoja chini ya Kristo mchungaji mkuu. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha, kwani Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya na ukamilifu wa utakatifu wote.

Askofu mkuu mstaafu Lebulu anafafanua kwamba, utakatifu huu unapaswa kushuhudiwa na kumwilishwa katika hisia, ili kweli ziwe ni hisia za kimungu; kwa kupenda zaidi sifa na fadhila za kikristo; kwa kujisadaka na kujitosa ili kutangaza na kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika: Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; ukweli, neema, utakatifu, upendo, haki na amani. Watu wa Mungu wachukie dhana na utamaduni wa kifo; dhambi na nafasi zake. Katika fikra zao daima wajitahidi kuwaza na kutenda mema; kamwe wasitafute shari ili kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu aliyewaita kutoka gizani na kuwaingiza katika mwanga wake mkuu.

Askofu mkuu mstaafu Josephat Louis Lebulu katika Ibada ya Kumsimika Askofu mkuu Isaack Amani wa Jimbo kuu la Arusha, alitumia fursa hii kuimba utenzi juu ya ukuu wa Mwenyezi Mungu ambaye ni muumbaji, aliyemkumbuka na kumwangalia mwanadamu hata katika udogo wake, akamfanya mdogo punde kuliko Mungu; akamvika taji ya utukufu na heshima, akamtawaza juu ya kazi ya mikono yake na hatimaye, kuvitia vitu vyote chini ya miguu yake. Anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa huruma na upendo wake kwa binadamu, kiasi kwamba, amewakirimia zawadi ya Kanisa kwa njia ya Fumbo la Pasaka.

Kumbe, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu inayomwokoa mwanadamu na changamoto zote zinazodhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Changamoto hizi ni ujinga, umaskini na maradhi. Askofu mkuu mstaafu Lebulu, anamshukuru Mungu kwa zawadi ya Kanisa ambalo amelihudumia kwa miaka 50 kama Padre na takribani ya miaka 40 kama Askofu. Anamshukuru Mungu kwa uwepo na utendaji huu wa Kanisa katika mazingira ya Ukanda wa Arusha na kwa hakika matendo makuu ya Mungu yanaonekana, kwani mwenye macho haambiwi, tazama! Kanisa limeendelea kupambana na ujinga kwa njia ya elimu bora na makini; limepambana na mardhi kwa kutoa huduma bora za afya na umaskini kwa kuibua na kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za maendeleo endelevu yanayowakumbatia na kuwambata watanzania wote bila kujali: imani, dini, itikadi au kabila na mtu!

Ni matumaini ya Askofu mkuu mstaafu Lebulu kwamba, Kanisa endeleza majadiliano ya kidini na kiekumene; litaendelea kudumisha ushirikiano na mshikamano na serikali katika mchakato wa huduma ya maendeleo endelevu, kwa kupania daima: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Mwishoni, amemwombea amani, Askofu mkuu Amani ili waweze kujaliwa kudumu katika uaminifu, uchaji wa Mungu, dhamiri safi na unyofu ambayo kimsingi ni dira ya hisia, fikra, kauli na matendo. Anamwomba Mwenyezi Mungu ili awajalie kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake; kwa kutunza na kudumisha ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo, ndani yake na kwa jirani zake. Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu, alihitimisha hotuba yake wakati wa kumsimika Askofu mkuu Amani wa Jimbo kuu la Arusha kwa kutoa baraka ya kikuhani: Bwana akubarikie, na kukulinda; Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani.

Itakumbukwa kwamba mahubiri ya Misa takatifu, Jumapili ya Huruma ya Mungu, tarehe 8 Aprili 2018 ambamo alisimikwa pia Askofu mkuu Isaac Amani Massawe kuwa mchungaji mkuu wa Jimbo kuu la Arusha yalitolewa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza. Alitoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kulijalia Jimbo kuu la Arusha kupata kiongozi mkuu kwa haraka, kwani kuna majimbo ambayo yamekaa muda mrefu hayajapata kiongozi. Pili ameitaka familia ya Mungu Jimbo kuu la Arusha kuachana na dini-mkorogo zinazowafanya kutangatanga katika dini na madhehebu mbali mbali hasa zaidi kwa uchu wa mali, utajiri na madaraka. Ameitaka familia ya Mungu kuhakikisha kwamba, inakuwepo katika maisha na utume wa Kanisa kwa: kuwajali na kuwahangaikia wengine; kwa kuwapenda, kuwaheshimu na kuwahudumia kikamilifu.

Amemshukuru Askofu mkuu mstaafu Lebulu ambaye katika maisha na utume wake amepambana na mengi, akavumilia kwa hekima na busara, sasa asamehe na kusahau. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi amemtakia heri na baraka Askofu mkuu Isaac Amani Massawe na kwamba, uzoefu wa miaka 10 kama Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi sasa umsaidie na kumwezesha: kuongoza, kufundisha na kuitakatifuza familia ya Mungu Jimbo kuu la Arusha.

Naye Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania amesema shule, hospitali na vitega uchumi vingine vilivyokuwa vikimilikiwa na taasisi za dini nchini na kutaifi shwa wakati wa Azimio la Arusha mwaka 1967, havitarejeshwa kwenye taasisi hizo. Rais Magufuli alisema hayo Jumapili tarehe 8 Aprili 2018, baada ya Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kumsimika Askofu mkuu Isaac Amani Massawe aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu Katoliki la Arusha ili kuchukua nafasi ya Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu, aliyeng’atuka kutoka madarakani. Ibada hii imefanyika kwenye Parokia ya Mtakatifu Theresa, Jimbo kuu la Katoliki Arusha.

Rais alisema miradi iliyokuwa ikimilikiwa na taasisi hizo za dini, kama vile makanisa na misikiti, haitarejeshwa kwenye miliki za taasisi hizo. Alikiri kupokea maombi kadhaa ya viongozi wa dini, wakimuomba kurejeshewa vitega uchumi vyao hivyo. Alisema, hata Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam aliwahi kumwandikia barua iliyoorodhesha mali za kanisa zilizotaifishwa wakati wa Azimio la Arusha na kumwomba Rais azirejeshe mali hizo kanisani.

Awali kabla ya hotuba ya Magufuli, Padre Kitomari wa Parokia hiyo alimwomba Rais kuirejesha mikononi mwa Parokia hiyo, Shule ya Msingi Naura, iliyopo eneo la Parokia, ambayo awali ilikuwa ikimilikiwa na kanisa hilo, lakini kwa sasa ipo chini ya serikali. Katika maombi yake, alielezea sababu kadhaa za kuomba shule hiyo irejeshwe mikononi mwa kanisa na moja ya sababu hizo ni shule hiyo ipo kwenye eneo lenye hati ya Parokia, ambapo kwa sasa inaendelea na ujenzi wa majengo yake mapya. Sababu nyingine ni kuwa matumizi mabaya ya uwanja wa shule hiyo, ambao unatumiwa na askari wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki) mkoani Arusha, kama sehemu ya kuegeshea magari wanayoyakamata, kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani. Kwa upande wa hoja hiyo, Magufuli alisema kuwa inaweza kuangaliwa kwa namna ya kipekee na kuwa akirejea Ikulu, ataifanyia kazi. Shule ya Naura ilijengwa mwaka 1950 na ilikuwa ikiitwa Shule ya Msingi ya Mtakatifu Theresia. Ilitaifishwa na serikali wakati wa Azimio la Arusha mwaka 1967.

Ilipobadilishwa iliitwa kwa jina la Naura, jina la mto unaopita karibu na shule hiyo. Kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi 350. Lakini, Rais Magufuli alikataa ombi la Parokia hiyo la kutaka kupewa eneo la bustani ya Naura, kwa kuwa ni eneo la wazi. Kwamba Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004 imesema kuwa maeneo yaliyo karibu na mito au maziwa, hayatakiwi kuguswa. Siyo viongozi wa Kanisa Katoliki tu, ambao wamekuwa wakiomba kurejeshewa shule zao, zilizotaifishwa na serikali, kwani hata Kanisa Anglikana nalo limekuwa na madai kama hayo.

Mwezi uliopita Kanisa Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, nalo lilimuomba Rais Magufuli kuwarejeshea Shule ya Sekondari ya Minaki, iliyopo nje kidogo ya Dar es Salaam, katika wilaya jirani ya Kisarawe mkoani Pwani. Ombi hilo lilitolewa na Askofu mpya wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes baada ya kusimikwa na kuwekwa wakfu katika Kanisa la Mtakatifu Albano, jijini humo. Kwa mujibu wa askofu huyo, shule hiyo kongwe ya Minaki ni moja ya shule za Waanglikani, zilizotaifishwa na serikali. Askofu huyo wa Kanisa Anglikani alitoa ombi hilo kwa Rais Magufuli, aliyehudhuria ibada Kanisani hapo.

Habari hii imeandaliwa kwa ushirikiano na Sarah Pelaji, Gazeti la Kiongozi, Sr. Dr. Gisela Upendo Msuya na kuhaririwa

na Padre Richard A. Mjigwa, Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.