2018-04-14 16:31:00

Papa Francisko anaendelea kufuatilia kwa karibu hali tete nchini DRC


Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufuatilia kwa karibu sana mateso na mahangaiko ya wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa CONGO, DRC na kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kuguswa na mahangaiko ya watu hawa kwa: kuwajibika zaidi, kwa kujenga mshikamano na udugu pamoja na kuhakikisha kwamba, mchakato mzima wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo, mwezi Desemba, 2018 unaanza mara moja. Hii ni pamoja na kutekeleza Mkataba wa Makubaliano ya Amani uliotiwa sahihi kunako tarehe 31 Desemba 2016. Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuwasindikiza wananchi wa DRC katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu pamoja na kuwahamasisha wananchi wenyewe kuwa macho na kusimama kidete kutetea na kulinda mustakabali wa nchi yao! 

Kanisa nchini DRC. Linaendelea kupambana na hali ngumu katika maisha na utume wake, kutokana na maandamano ya kudai haki yaliyoandaliwa na Kamati ya Waamini Walei nchini DRC, kuleta mkitisiko mkubwa katika uwanja wa kisiasa nchini humo. Matokeo yake, Serikali ya DRC ikajibu mapigo kwa kutumia nguvu kubwa na hivyo kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha huko Kasai, Utembe-Beni na Djugu. Baadhi ya mapadre wametekwa nyara na kuuwawa na wengine wamepotea katika mazingira ya kutatanisha!

Vurugu zote hizi zimekuwa zikibandikwa majina ya choko choko za kikabila, lakini ukweli wa mambo ni kwama, hizi ni vurugu zinazofumbatwa katika masuala ya kiuchumi na kisiasa ndiyo maana Serikali inaendelea kuweka mkono wake! Haya yamesemwa na Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican wakati alipokuwa anatoa hotuba kwenye mkutano wa utu wa binadamu ulioandaliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayojihusisha na misaada ya kiutu!

Anasema, Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya wananchi wa DRC wakati wa kutoa ujumbe na salam zake za Pasaka kwa mwaka 2018 maarufu kama “Urbi et Orbi”, aligusia matatizo na changamoto zinazolikabii Bara la Afrika kutokana na ulinzi na usalama kwa kusema, kwamba, kuna watu Barani Afrika wanateseka na kufariki dunia kwa baa la njaa, vita pamoja na vitendo vya kigaidi; mambo yanayochangia kuwepo kwa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika. Baba Mtakatifu pia amekuwa akielezea mahangaiko ya watoto wadogo nchini DRC wanaotekwa kutoka kwenye familia zao na kupelekwa mstari wa mbele kama askari wa chambo katika mapigano, badala ya kuwa madarasani wakisoma. Tarehe 23 Februari 2018 Wakristo na waamini wa dini mbali mbali waliungana kusali kwa ajili ya kuombea amani ya kudumu nchini DRC na kwamba, kila mtu alipaswa kuchangia katika kukuza na kudumisha amani duniani. Vatican imekuwa pia mstari wa mbele kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa DRC hadi sasa imechangia kiasi dola za kimarekani $ 500, 000. 00 kwa ajili ya kusaidia mchakato wa kupambana na ujinga, afya na umaskini.

Juhudi hizi pia zinachangiwa na Shirikisho la Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis ambayo hadi sasa imewahudumia watu zaidi 790, 000. Zaidi ya dollar za Kimarekani milioni moja zimetengwa kwa ajili ya kugharimia miradi mbali mbali ya maendeleo endelevu hasa katika maeneo yaliyoathirika kwa vita. Watu zaidi ya milioni 13 wako katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa, kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi ili kuwasaidia watu hawa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.