2018-04-13 14:58:00

Papa Francisko: Jitahidini kuwa na uhuru wa kweli hata katika mateso!


Waamini wanapaswa kumwachia Mwenyezi Mungu uhuru kamili ili aweze kutenda ndani mwao kadiri anavyotaka kama ilivyokuwa kwa Farisayo aliyejulikana kama Gamalieli, Mwalimu wa torati, aliyekuwa anaheshimiwa sana aliyesimamia kidete ukweli kuhusu mafundisho ya mitume; wengine walioshuhudia uhuru wa kweli ni Petro mtume na Yohane, mwanafunzi aliyependwa zaidi na Kristo Yesu. Hawa wanaweza kuwa ni mashuhuda wa uhuru wa Kikristo, dhidi ya uchu wa mali na madaraka! Uhuru wa kweli unatoa nafasi ya kwanza kwa Mwenyezi Mungu, ili kumfuasa katika furaha na amani ya ndani hata katika shida na magumu ya maisha! Hii ni changamoto kwa kila mwamini kuangalia nafsini mwake, ili kuona ikiwa kweli anao uhuru unaofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 13 Aprili 2018 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu amefafanua Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Matendo ya Mitume na Sehemu ya Injili ya Yohane, kuhusu muujiza wa Yesu alipowatokea mitume wake kando ya bahari ya Tiberia na kufanya muujiza uliowapatia mitume wake samaki wengi zaidi, baada ya kukata tamaa ya kufanya kazi usiku kucha, lakini wakaambulia patupu! Yesu pia aligeuza mkate, akawapatia mitume wake. Hii ilikuwa ni mara ya tatu, Yesu kuwatokea mitume wake na kuwaimarisha katika utashi na uhuru wa kumshuhudia kati ya watu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kipindi cha Pasaka ni muda muafaka wa kufurahia uhuru wa watoto wa Mungu, unaobubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka! Huu ni uhuru unaoshuhudiwa na wadau mbali mbali katika Matendo ya Mitume; wagonjwa walionja huruma na upendo wa Mungu, kiasi cha kuwafungulia vifungo vya ulemavu wao, wakawa huru, tayari kumtangaza na kumshuhudia kati ya watu wa Mataifa. Ponsio Pilato alikuwa huru katika hukumu yake, lakini bahati mbaya, akashindwa kusimamia maamuzi yake kwani hakuwa na uhuru wa ndani. Alitambua kwamba, Kristo Yesu hakuwa na hatia, lakini kwa kutaka kuwaridhisha watu akaamuru ateswe na kuuwawa Msalabani. Hakuwa na ujasiri wala uhuru kamili, alifungwa zaidi na uchu wa madaraka, alitaka kukuza na kudumisha urafiki na Kaisari.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mtume Petro na Yohane, walikuwa ni watu huru, wakasimamia kazi na muujiza uliotendwa kwa jina la Kristo Yesu mkombozi wa dunia kwa kumponya yule kiwete aliyekuwa anaketishwa kwenye mlango wa hekalu uitwao Mzuri. Kuhani mkuu, “akawapiga mkwara wa nguvu” na hatimaye, watu wazima kuchapwa viboko, lakini bado wakaendelea kuwa watu huru na wenye furaha ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo hata katika mateso!

Huu ni mwaliko kwa waamini kumkaribisha Kristo Yesu katika: maisha, akili na nyoyo zao, ili hatimaye, kuweza kujikabidhi wazima wazima kwa Kristo Yesu, kwani wana heri wale wote wanaoteseka kwa ajili ya Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kusema, uhuru wa mitume ni ushuhuda wa upendo hata katika: mateso, nyanyaso na dhuluma mbali mbali. Uhuru wa Mitume unawapatia jeuri ya kuungama imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hata pale Yesu alipotenda miujiza, aliendelea kubaki huru na wala hakutaka watu watumie nafasi hiyo kumpaka “mafuta kwa mgongo wa chupa”. Daima Kristo Yesu alikuwa huru kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni. Hii ni changamoto kwa waamini kujiuliza ni kiasi gani wako huru katika kumfuasa Kristo Yesu katika njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, au wako huru huku wakitamani mambo ya hapa duniani? Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa na huru wa kweli unaotolewa na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.