2018-04-12 15:08:00

Furaha ya Pasaka inafumbatwa katika utii na ushuhuda unaomwilishwa!


Takwimu zinaonesha kwamba, kuna Wakristo wengi zaidi wanaoteseka na kunyanyasika sehemu mbali mbali za dunia, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo. Hawa ni watu wanateswa na kuhukumiwa kunyongwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Ukweli kuhusu: wito, maisha na utume wa Kanisa si tena Habari yenye mvuto na mashiko kwani inaleta kichefuchefu na hivyo kusababisha mateso na nyanyaso! Kuna haja kwa Wakristo kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya uvumilivu, udumifu na ushupavu wa kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake!

Daima wakumbuke kwamba, siku ile ya kwanza walipokutana na Kristo Yesu, aliwaletea mageuzi makubwa katika hija ya maisha yao hapa duniani, tukio ambalo kamwe halipaswi kusahaulika katika maisha ya waamini. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 12 Aprili 2018 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Baada ya mapumziko ya Kipindi cha Pasaka, Baba Mtakatifu amekazia zaidi: utii na ushuhuda unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini, chemchemi ya furaha katika kipindi hiki cha Pasaka, Wakristo wanapoendelea kumshangilia Kristo Mfufuka!

Mama Kanisa ametenga Siku 50 za furaha na shangwe kwa ajili ya Fumbo la Pasaka! Hii ni furaha inayofunikwa kwa sehemu kubwa la “blanketi la woga, wasi wasi na hofu” kwa kuhofia hatima ya maisha ya Wakristo kwa siku za usoni! Baada ya Roho Mtakatifu kuwashukia Mitume, wakapata ujasiri wa kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa, amefufuka kutoka kwa wafu! Roho Mtakatifu aliwaimaarisha na kuwafundisha yote yaliyosemwa na Kristo Yesu wakati wa utume wake hapa duniani!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Roho Mtakatifu aliwawezesha Mitume kusimamia kweli za Kiinjili kama sehemu ya utii kwa mapenzi ya Mungu. Mitume walifungwa jela na kufunguliwa na Malaika, wakatoka na kuanza kufundisha hekaluni. Hata pale Kuhani Mkuu alipokuwa amewakanya kwa nguvu kutofundisha juu ya Yesu, lakini Petro pamoja na mitume wengine, walisimama kidedea na kusema, imewapasa kumtii Mungu kuliko wanadamu! Utii kwa mapenzi ya Mungu ni wazo linalojitokeza hata katika Injili ya siku, ushuhuda wa maisha ya mwamini aliyempokea Roho Mtakatifu na kumwachia nafasi ili aweze kumwongoza.

Utii ni kielelezo cha maisha na utume wa Kristo Yesu, uliopata ukamilifu wake kuanzia kwenye Bustani ya Mizeituni, alipokuwa anazungumzia kuhusu Kikombe cha Mateso na Utii kwa mapenzi ya Baba yake wa mbinguni! Mkristo anapaswa kumtii Mwenyezi Mungu! Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, rushwa ilipenyeza mizizi yake hata kuingia makaburini! Yesu kwa kutambua tatizo la kumezwa na malimwengu alisema mapema kabisa kwamba, si rahisi kuwatumikia mabwana wawili, yaani Mungu na mali! Ushuhuda wa Mitume, uliwachefua sana viongozi wa wakati ule! Ikumbukwe kwamba, ushuhuda wa Kikristo unafumbatwa katika uvumilivu unaowasindikiza waamini kushirikisha imani yao kwa Kristo sanjari na kujenga msingi wa maridhiano, daima wakijitahidi kusimamia kweli za Kiinjili.

Baba Mtakatifu anasema, Utii na Ushuhuda wa maisha na utume wa Kikristo ni mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa. Hadi leo hii kuna Wakristo kutoka Afrika, Mashariki ya Kati na sehemu mbali mbali za dunia, wanaoendelea kuteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hawa ni watu wanaoshuhudia imani katika matendo, kwani wameguswa kutoka katika undani wa maisha yao na uwepo endelevu wa Kristo Yesu! Uwepo huu umeleta mabadiliko makubwa katika maisha yao, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu neema na baraka ya kumwilisha tunu hizi katika uhalisia wa maisha! Furaha ya Pasaka inafumbatwa katika utii na ushuhuda unaomwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.