2018-04-11 07:41:00

Papa Francisko: Utakatifu wa maisha ni wito kwa watu wote!


Baba Mtakatifu Francisko ametoa Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) umezinduliwa, Jumatatu, tarehe 9 Aprili 2018, Kumbu kumbu ya Bikira Maria kupashwa habari kuwa atakuwa ni Mama wa Mungu. Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha katika sehemu mbali mbali za Maandiko Matakatifu.

Baba Mtakatifu anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4). Wosia huu wa kitume umegawanyika katika sura kuu tano: Sura ya kwanza ni Wito wa utakatifu; Sura ya Pili ni Adui wa utakatifu; Sura ya tatu: Mwanga katika maisha ya Mwalimu, Sura ya nne: Alama za Utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo na Sura ya tano: Mapambano ya maisha ya kiroho; kukesha na kufanya mang’amuzi!

Sura ya kwanza: Wito wa utakatifu Baba Mtakatifu Francisko katika sura hii anasema, watakatifu ni watu wanaotia shime pamoja na kuwasindikiza waamini wenzao kama vyombo na mashuhuda wa imani na matumaini kama ilivyokuwa katika Agano la Kale; hata leo hii hawa ni watu wanaoweza kuwa ni ndugu, jamaa na marafiki; watu wanaosadaka maisha yao, mashuhuda wa upendo wa Kristo na wale wanaoendelea kujitosa kwa ajili ya umoja wa Kanisa. Hawa ni majirani wanaotangaza na kushuhudia utakatifu wa maisha katika uhalisia wa maisha ya kila siku pasi na makuu. Ni watu wanaoshuhudia unyenyekevu katika maisha, kiasi hata cha kuacha alama za mvuto na mashiko katika uekumene wa damu kama unavyofafanuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Wakristo wote wanahamasishwa kuwa watakatifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mtakatifu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata wewe unaitwa kuwa mtakatifu katika maisha yako kama mtu wa ndoa, maisha ya kuwekwa wakfu, mfanyakazi na mhudumu wa upendo kwa jirani zako!

Neema ya utakaso inaweza kuwasaidia waamini kuambata njia ya utakatifu, kwa kukumbatia Matunda ya Roho Mtakatifu. Waamini kwa njia ya maisha na ushuhuda wao, wasaidie kuyatakatifuza malimwengu kama vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu: kiroho na kimwili. Wakristo watambue kwamba, wanashiriki katika maisha na utume wa Kristo Yesu hapa duniani, kumbe, wanatumwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao kadiri ya historia na changamoto za Kiinjili; daima kwa kuungana na Kristo Yesu katika Fumbo la maisha na utume wake, kielelezo makini cha ufunuo wa huruma ya Baba kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu! Utakatifu ni mchakato unaowawezesha waamini kuishi upendo katika utimilifu wake kadiri ya nguvu na mwanga wa Roho Mtakatifu. Maisha ya kila mwamini yawe ni kielelezo cha utume kutoka kwa Kristo Yesu anayetaka kuwaletea waja wake mabadiliko katika maisha, licha ya udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, daima wakijitahidi kuambata upendo wa Kristo katika maisha yao!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna vitendo ambavyo vinatakatifuza watu, hasa pale waamini wanapojizatiti katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika misingi ya: haki, amani na upendo; maisha ya sala yanayomwilishwa katika huduma kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee anawataka waamini kujifungamanisha na tasaufi ya utume kama inavyodadavuliwa kwenye Waraka wake wa kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”; tasaufi ya ekolojia inayofumbatwa katika Waraka wake wa kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Tasaufi ya maisha ya familia imefafanuliwa kwenye Waraka wake wa kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya famili”.

Waamini wajenge utamaduni na sanaa ya kukaa kimya mbele ya Mungu, ili waweze kusikia kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka kuzungumza nao kutoka katika undani wa dhamiri zao nyofu! Moyo wa utakatifu upambe upweke wa maisha! Hakuna sababu ya kuogopa kuambata utakatifu wa maisha! Kama iliwezekana kwa Bakhita aliyetekwa nyara na hatimaye kuuzwa utumwani, lakini kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake, amekuwa mtakatifu, hii inaonesha kwamba, utakatifu ni jambo linalowezekana kabisa! Uinjilishaji mpya unafumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kuwa chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa! Maafa makubwa yanayoweza kumkumba mwanadamu ni kushindwa kuwa mtakatifu!

Sura ya Pili ni Maadui wa utakatifu: Baba Mtakatifu Francisko katika sura hii anagusia mitindo potofu ya utakatifu wa maisha unaoelea katika ombwe; akili bila ya kumtegemea Mungu wala kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Hawa ndio wale watu wanaomtafuta Mungu bila ya Kristo Yesu; wanaomtaka Kristo Yesu bila Kanisa, au kulipenda Kanisa bila watoto wake! Haya ni mawazo yanayoendelea kusumbua vichwa vya watu wa nyakati hizi. Ni watu wanaotaka mafundisho ambayo kamwe hayana Fumbo ndani mwake, kwani wanayo majibu ya maswali yote yanayomtatiza mwanadamu! Hawa ni watu wanaodhani kwamba, wanaweza kumweka Mwenyezi Mungu “mfukoni mwao” na kumtumia kama wanavyotaka!

Waamini wanapaswa kutambua kwamba, uwezo wa mwanadamu kufikiri una ukomo wake! Hawawezi kuhalalisha kweli za Kiinjili ili kukidhi matakwa yao binafsi na kwamba, Mafundisho tanzu ya Kanisa yanaendelea kufafanuliwa daima katika maisha na kwamba, taalimungu na utakatifu wa maisha ni mambo yasiyopingana wala kusigana! Hekima na busara ya Kikristo inafumbatwa pia katika huruma na upendo kwa jirani! Waamini waendelee kupambana na maadui wa utakatifu wa maisha kwa kwa kujikita katika Ibada ya kweli inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Baba Mtakatifu anasema, hata leo hii bado kuna wazushi na wakanimungu kwani wanadhani kwamba, kila jambo linategemea utashi wa binadamu na kusahau huruma na upendo wa Mungu, ambaye aliwapenda binadamu kwanza! Hawa ni watu wanaoshindwa kutambua karama, mchango na nafasi ya kila mwamini katika maisha na utume wa Kanisa. Hakuna mtu aliyebarikiwa kufanya yote kwa ukamilifu, bali watu wanategemeana na kukamilishana katika unyenyekevu! Watu wakiri na kutambua: karama, uwezo na mapungufu yao katika maisha kwani neema inajikita katika asili ya binadamu!

Mama Kanisa anaendelea kufundisha kwamba, watu wanahesabiwa haki si kwa matendo yao bali kwa njia ya neema inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu! Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena, au hapo neema isingekuwa neema. (Rej. Rum. 11:6). Wito huu wa uzima wa milele ni wa Kimungu. Wote kabisa twategemea kazi ya Mungu, kwani Yeye peke yake anajifunua na anajitoa mwenyewe; Wapita maweza ya akili na nguvu za utashi wa kibinadamu! (Rej. KKK. Namba 1999). Watakatifu walijitahidi kutenda haki mbele ya Mungu na jirani zao, wakamwilisha upendo huo katika uhalisia wa maisha yao!

Wazushi mamboleo na wakanimungu wanaendelea kujionesha kwa kujikita katika Sheria kanuni za Kanisa, Liturujia na Mafundisho Tanzu ya Kanisa kwa ajili ya kujikweza kwa kujitafutia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko! Badala ya kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu katika unyenyekevu na upendo, ili hatimaye, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa uzuri na furaha ya Injili, ili kuzima kiu na matamanio halali ya watu wa Mataifa! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna itifaki ya karama na tunu msingi zinazowaunganisha waamini ili kuambata mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Tunu hizi ni: imani na upendo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuzitafakari tunu hizi na kufanya man’amuzi mbele ya Mwenyezi Mungu.

Sura ya tatu: Mwanga katika maisha ya Mwalimu. Hapa Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuambata Heri za Mlimani kama muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu yanayoweza kuwasaidia kufikia utakatifu wa maisha. Umaskini wa roho ni kielelezo cha utakatifu; Upole ni sehemu ya Matunda ya Roho Mtakatifu. Mwamini kwa kufikiri na kutenda katika upole anaonesha cheche za utakatifu wa maisha. Waamini wajifunze kuhuzunika na kuomboleza na jirani zao; kwa kuwa na njaa na kiu ya haki; kwa kuona na  kutenda katika huruma; kwa kuwa na moyo safi; kwa kupandikiza na kukuza mbegu ya upatanishi na amani!

Baba Mtakatifu anasema, Heri za Mlimani zinawasaidia waamini kufuata nyayo za Kristo Yesu Bwana na Mwalimu wao! Waamini wakumbuke kwamba, siku ya mwisho watahukumiwa kadiri walivyowatendea kwa upendo jirani zao walio wadogo, ambao Kristo Yesu anajifafanisha nao! Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo Bwana na Mwalimu wao! Waamini waendelee kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa kutekeleza kwa dhati matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama ambavyo wamehimizwa wakati wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu. Matendo ya huruma ni kiini cha Injili ya Kristo inayolenga kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Maskini ni amana na hazina ya Kanisa, kwani wao ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu!

Baba Mtakatifu anawalika waamini kufuata nyayo za Kristo kwa njia ya sala na ibada; kwa kujikita katika misingi ya haki, amani na upendo unaomwilishwa katika huruma! Waamini wajiepushe na tamaa ya kupenda malimwengu, raha na anasa za dunia hii, waguswe na mahangaiko pamoja na mateso ya jirani zao kwa kujibu kilio chao kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama njia makini ya kuendelea kumwilisha Injili katika uhalisia wa maisha ya watu! Ushuhuda wa watakatifu umefumbatwa katika Heri za Mlimani na Matendo ya Huruma; chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha ya Kikristo!

Sura ya nne: Alama za Utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo! Baba Mtakatifu katika sura hii anapenda kukazia zaidi: udumifu, uvumilivu na unyenyekevu wa moyo kama alama za utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo dhidi ya tabia matumizi ya nguvu, ubinafsi na uchoyo pamoja na hali ya mtu kujiridhisha binafsi katika ufahari wake. Wakristo wawe wanyenyekevu kwa kujikita katika ukweli na uwazi; utu wema pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya ulimi! Waamini wafurahie pia mafanikio ya jirani zao, wawasahihishe kwa upole na udugu pale wanapolegea katika dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu. Hakuna unyenyekevu pasi na kunyenyekeshwa na huu ni ushuhuda wa utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo. Kuna waamini wanaoendelea kusimamia haki, amani na maridhiano katika jamii kiasi hata cha kuyamimina maisha yao! Hawa wanahesabika kuwa ni vyombo vya amani! Maisha ya Kikristo ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu na kwamba, furaha ya kweli inafumbatwa katika upendo!

Wakristo wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha na utulivu wa ndani, kwa kujenga na kudumisha umoja na upendo wa kidugu. Waamini waoneshe uhuru na upendo wa ndani kabisa kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya upya wa maisha yao! Familia ya Mungu ioneshe ujasiri wa kutoka kifua mbele kama ilivyokuwa kwa watakatifu wa nyakati mbali mbali ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, utakatifu ni hija inayofumbatwa pia katika maisha ya kijumuiya na Mama Kanisa anayo mifano kede kede ya Jumuiya za watakatifu. Hawa ndio akina Paul Miki na wenzake au Wamonaki waliouwawa hivi karibuni huko Algeria. Hawa ni watakatifu ambao wameishi kwa pamoja huku wakiadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na kujenga umoja na udugu. Hawa ni kama Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Jumuiya za Kikristo ziwe ni mahali pa kurutubisha upendo, umoja na udugu; kwa kusaidiana na kutakatifuzana katika maisha, ili wote waweze kuwa wamoja chini ya Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema, utakatifu unafumbatwa katika maisha ya sala kama sehemu ya mchakato wa kutaka kujenga uhusiano wa karibu na Mwenyezi Mungu, kumbe, sala endelevu ni chachu ya utakatifu wa maisha! Ukimya na tafakuri  ni nyenzo zinazojenga uhusiano mwema na Kristo! Lakini, sala ya kweli inamwilishwa katika uhalisia wa maisha yanayofumbatwa katika upendo. Waamini wajenge utamaduni na sanaa ya kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika medani mbali mbali za maisha kwani hiki ni kiini na utambulisho wa Kanisa. Waamini wajitahidi kukutana na Kristo Yesu katika Neno na Sakramenti za Kanisa, ili waweze kuwa ni chachu ya utakatifu wa maisha katika ulimwengu mamboleo!

Sura ya tano: Mapambano ya maisha ya kiroho; kukesha na kufanya mang’amuzi! Baba Mtakatifu Francisko anasema, maisha ya kikristo ni mapambano endelevu yanayohitaji nguvu na ujasiri, ili kumpatia nafasi Kristo aweze kushinda na hatimaye, waamini kufurahia maisha. Waamini watambue kwamba, shetani, Ibilisi yupo na wala si dhana ya kufikirika tu! Waamini wawe macho na waendelee kukesha na kusali kwa kutambua kwamba, ushindi wao unafumbatwa katika Msalaba wa Kristo. Utakatifu ni chemchemi ya furaha na amani ya ndani. Huu ni mwaliko wa kupambana na “giza la maisha ya kiroho” kwa kujikita katika mang’amuzi ya maisha ya kiroho kwa kutafakari kwa kina na mapana matamanio halali ya maisha, uchungu na fadhaa katika maisha yao; hofu na mashaka ili kutambua njia zinazowaelekeza katika uhuru wa kweli, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati kadiri ya mwanga wa Kristo Mfufuka. Mang’amuzi ya maisha ya kiroho, yawasaidie waamini kutambua Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Waamini wampatie nafasi Kristo Yesu ili aweze kuzungumza kutoka katika undani wa maisha yao! Furaha ya kweli anasema Mtakatifu Bonaventura, imetundikwa kwenye mti wa Msalaba. Waamini wamwombe Roho Mtakatifu ili aweze kuwaondolea woga na hofu zisizokuwa na mashiko ili kuanza mchakato wa kutoka katika ubinafsi, tayari kuliendea Fumbo la maisha ya Mungu, anayewasaidia waja wake kutekeleza utume wao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya ndugu zao katika Kristo! Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” kwa kumwangalia Bikira Maria aliyemwilisha Heri za Mlimani kuliko mtakatifu yoyote yule. Ni mwanamke aliyefurahia uwepo wa Mungu katika maisha yake na kuhifadhi yote katika sakafu ya moyo wake!Bikira Maria ni Mtakatifu kuliko watakatifu wote. Ni kimbilio la waamini katika ulinzi na tunza ya kimama. Anawafundisha na kuwasindikiza waamini katika utakatifu wa maisha; anawalinda bila kuwahukumu; anawafariji, kuwaombea na kuwatakatifuza kwa uwepo wake, changamoto na mwaliko kwa waamini kumkimbilia katika sala. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Wosia huu wa kitume utawasaidia waamini kuambata hija ya utakatifu wa maisha, ili kweli waweze kuwa ni watakatifu kwa ajili ya utukufu wa Mungu kwa kusaidiana na kuhimizana katika mchakato wa utakatifu wa maisha, ili waamini wote waweze kushiriki furaha ya uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.