2018-04-11 14:37:00

Papa Francisko kutembelea Parokia ya Mt. Paolo wa Msalaba, 15 Aprili.


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili alasiri, tarehe 15 Aprili 2018 anatarajiwa kutembelea Parokia ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba, nje kidogo ya Jimbo kuu la Roma ambako atapata nafasi ya kukutana na watoto wanaohudhuria katekesi hapo parokiani; wazee, wagonjwa pamoja na maskini! Baba Mtakatifu atapata nafasi pia kuwaungamisha waamini watakaokuwa wamejiandaa kwa ajili ya kupokea huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Baadaye, Baba Mtakatifu ataadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, huku akishirikiana na Askofu mkuu Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, Askofu msaidizi Paolo Selvadagi; Paroko Roberto Cassano na wasaidizi wake Gabriele Petreni, Eberth Antonio Carranza Segura pamoja na Padre Henrique Fragoso de Souza.

Padre Roberto Cassano anakiri kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alikwishawahi kuonesha nia ya kutembelea Parokiani hapo, miezi mitano iliyopita, ili kuwatia shime katika maisha na utume wao, kwani eneo la Parokia hii, linaangaliwa kwa “jicho la kengeza” kama eneo hatari sana kwa usalama na maisha ya watu, lakini wengi wanasahau kwamba, hata hapa kuna watu wema na watakatifu. Wakazi wa eneo hili wanaishi katika maghorofa makuu mawili yanayounganishwa na daraja moja, lakini kwa hakika maghorofa haya yanahitaji kufanyiwa ukarabati mkubwa, ili kuboresha maisha ya watu!

Katika eneo hili pia kuna Maktaba ya Serikali pamoja na vyama na mashirika ya kitume yanayojisadaka kwa ajili ya wananchi hawa! Kwa bahati mbaya, Parokia hii ina ukame mkubwa wa vijana, kwani vijana wanapohitimu masomo yao, wanakimbilia kwenda mijini ili kutafuta maisha bora zaidi, kumbe, wananchi wengi wa eneo hili ni wazee wanaopambana na hali yao ya maisha! Parokia inaendelea kuwekeza zaidi na zaidi katika maisha na utume kwa vijana wa kizazi kipya kwa kuanzisha vituo vya michezo kwa vijana na watoto. Parokia daima imeonesha upendo na mshikamano kwa wagonjwa, wazee na familia ambazo zinakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na sababu mbali mbali. Hali ya uchumi wa Parokia inasua sua kutokana na umaskini wa wanaparokia, kumbe, Parokia inapata ruzuku kutoka Jimbo kuu la Roma! Licha ya umaskini wa kipato, lakini, wanaparokia ni wakarimu sana katika kazi za kujitolea, hawana fedha, lakini wanatumia nguvu na vipaji vyao kama mtaji kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Parokia ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba, jambo la kumshukuru sana Mwenyezi Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.