2018-04-10 14:44:00

Papa Francisko: Wamisionari wa huruma ni vyombo vya upendo na faraja


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yamekuwa ni fursa kwa waamini wengi kuweza kutubu na kumwongokea tena Mwenyezi Mungu katika maisha yao kwa kukimbilia katika Mahakama ya huruma ya Mungu, yaani Sakramenti ya Upatanisho. Wamisionari wa huruma ya Mungu wamekuwa ni alama ya hamasa ya umama wa Kanisa kuingia katika utajiri wa Fumbo la imani yaani, huruma ya Mungu ambayo haina mipaka kwa waja wake. Kwa njia ya Wamisionari wa huruma ya Mungu, waamini wengi wamepata nafasi ya msamaha na maondoleo ya dhambi zao.

Ndiyo maana, Baba Mtakatifu Francisko baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu akaridhia kwamba, utume wao, uendelee ndani ya Kanisa chini ya usimamizi na uratibu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji mpya ambalo kwa sasa linaongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, kama Rais wa Baraza hili! Baba Mtakatifu analishukuru Baraza hili kwa kuwawezesha wamisionari wa huruma ya Mungu kwa njia ya sala, tafakari na maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa!

Wamissionari wa huruma ya Mungu wanayo nafasi ya pekee inayowawezesha kutekeleza mpango wa huruma ya Mungu kadiri ulivyofunuliwa na Kristo Yesu na kupata utimilifu wake katika mwanga wa Fumbo la Pasaka! Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 10 Aprili 2018 alipokutana na kuzungumza na Wamisionari wa huruma ya Mungu ambao wamekuwepo hapa mjini Vatican ili kujinoa zaidi katika maisha na utume wao maalum! Kwa njia ya Wamisionari wa huruma ya Mungu, Mwenyezi Mungu amewafariji, amewahurumia na kuwakumbuka watu wake, kiasi cha kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka!

Wamisionari wa huruma ya Mungu ni vyombo na mashuhuda wa neema ya Mungu wanaopaswa kutenda pamoja naye, kwani wakati uliokubalika anawasilikiza na siku ya wokovu anawasaidia. Wamisionari wa huruma ni mabalozi na vyombo vya amani na msamaha kutoka kwa Mungu! Huu ni mwendelezo wa amani na msamaha uliotolewa na Kristo Mfufuka kwa mitume wake, changamoto na mwaliko wa kuishi kadiri ya wito na utume huu bila ya kuwa ni sababu ya makwazo kwa watu wa Mungu. Wamisionari wa huruma ya Mungu wanapaswa kuishi na kufumbata upendo wenye huruma katika maisha yao, aliyewakirimia neema na kuwa watu wapya, ili kugundua kiini cha Injili.

Wamisionari wa huruma ya Mungu wanatambua kwamba, wao ni wadhambi na wamekuwa watu wa kwanza kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kama ilivyokuwa kwa Mtume Paulo, Mwalimu wa Mataifa. Huruma ya Mungu inajionesha katika maisha ya watu kwa kuwasaidia kutubu na kuongoka, ili hatimaye, kushirikiana na Mungu kama vyombo na mashuhuda wake. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, Mwenyezi Mungu ameweza kuupatanisha ulimwengu wote pamoja naye. Kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, Mwenyezi Mungu anachukua hatua ya kwanza ili kuonesha upendo kwa mdhambi, kama ilivyo kwa Mama Kanisa kuanza kwa ushupavu kuwaendea na kuwatafauta walioanguka, waliotengwa na kuwakaribisha ili kuwaonjesha mang’amuzi ya huruma ambayo ni matunda ya nguvu ya Baba isiyokuwa na kikomo!

Mapadre waungamishaji wawe ni vyombo vya faraja kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mungu na kwamba, mang’amuzi ya Sakramenti ya Upatanisho yawaonjeshe watu upendo wa Mungu. Wamisionari wa huruma ya Mungu wawasaidie waamini kutambua udhaifu na dhambi zao, kwa kuwapokea na kuwakumbatia kama Baba Mwenye huruma, ili mwamini aweze kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yake ambaye daima ni mwingi wa huruma na mapendo!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mwenyezi Mungu hujawa na furaha pale anapomwona mdhambi akitubu na kumwongokea. Wamisionari wa huruma ya Mungu wawaangalie watu kwa macho ya huruma na upendo; wawasikilize kwa saburi ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaosamehe, kuganga na kuwaponya. Kwa njia hii, Mwenyezi Mungu yuko tayari kuwavika pete ya uaminifu kuwaonesha kwamba, wao ni sehemu ya familia yake!

Wamisionari wa huruma ya Mungu wanaweza kuwaongoza watu kwenye chemchemi ya maisha ya uzima, ili kujipatanisha na Mungu. Msamaha ni mchakato unaomrejeshea tena mwamini furaha na maana ya maisha, kwa kuvikwa tena vazi jipya na hivyo kustahilishwa kuitwa mwana wa Mungu kwa kupewa utu na maisha mapya, imani na dhamana katika maisha. Huruma inafungua malango ya matumaini, inajenga matumaini na kurutubisha matumaini.

Mtakatifu Inyasi wa Loyola anasema, faraja ya ndani inamwezesha mwamini kufahamu siri za undani wa maisha; kuonja upendo wa Mungu na kupata pumziko, hii ndiyo njia inayopaswa kufuatwa ili kutekeleza mapenzi ya Mungu. Kwa hakika, Sakramenti ya Upatanisho inamwezesha mwamini kupata faraja ya ndani inayorutubisha hija ya maisha yake ya Kikristo! Kwa njia ya dhambi, waamini wanamwacha na kumwasi Mungu wao, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli. Kwa njia ya dhambi, waamini wanamwasi na kumgeuzia Mungu kisogo! Hiki ni kimya kikuu na utupu ambao mtu anaweza kupata mang’amuzi katika maisha yake! Kristo Yesu, alipokuwa pale Msalabani, alilia kwa sauti kuu akisema, “Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha?

Lakini, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kamwe upendo wa Mungu haukumwacha Kristo Yesu kwa sababu alikuwa mwaminifu kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu alikuwa amemchora katika viganja vya mikono yake! Hapa mkazo ni upendo usiokuwa na kikomo ndio ambao unapaswa kumwilishwa kwa waamini wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huruma ya Mungu inavunjilia mbali upweke, inamkirimia mwamini ujasiri wa kusonga mbele; inawawezesha watu kukubaliwa tena katika maisha ya kijumuiya na hivyo kujenga tena upya wa maisha. Wamisionari wa huruma ya Mungu wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wanaomwilisha huruma hii katika maisha ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.