2018-04-09 08:19:00

Bikira Maria Mama wa huruma ya Mungu ni mwalimu wa watakatifu wote!


Tunakimbilia ulinzi wako, Mama Mzazi Mtakatifu wa Mungu, usitunyime tukiomba katika shida zetu, utuopoe kila tuingiapo hatarini! Hii ni sala iliyotungwa na Mababa wa Kanisa tangu karne ya tatu, lakini Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenye heri na watakatifu katika kitabu chake kuhusu: “Watakatifu na Bikira Maria Mama wa Mungu” anasema, tafsiri sahihi inapaswa kuwa “tunakimbilia huruma yako, Mama Mzazi wa Mungu” ambayo kwa lugha ya Kilatini ingekuwa “Sub tuam misericordiam”. Hii inatokana na ukweli kwamba, Bikira Maria ni Mama wa Mungu na mwalimu wa watakatifu wote.

Bikira Maria ni Mama wa Mwana wa Mungu mwenye huruma na mapendo, kama anavyosifiwa katika Sala ya “Salve Regina” yaani “Salam Malkia” Mama mwenye huruma, ambaye waamini wa nyakati zote wamekimbilia ulinzi na tunza yake ya kimama, wakiomba msamaha wa dhambi zao kutoka kwa Kristo Yesu. Bikira Maria, amekuwa ni kielelezo makini cha Mama mwenyehuruma; Mama mwenye moyo safi, Mama wa Ibada na kimbilio la wakosefu. Ni kutokana na huruma na unyofu wa moyo anasema Mtakatifu Bernardi, waamini wengi waliweza kukimbilia ulinzi na tunza yake ya kimama! Bikira Maria amewatokea watu wengi akijionesha kuwa ni Mama mwenye huruma, chemchemi ya neema na baraka inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu! Kwa njia hii, amekuwa kweli shule ya huruma ya Yesu katika maisha ya watu!

Bikira Maria alipata upendeleo wa pekee, akatungwa mimba na kuzaliwa bila ya kupata doa la dhambi ya asili, ili aweze kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili kwa njia ya Roho Mtakatifu. Bikira Maria, aliyepalizwa mbinguni mwili na Roho, anaendelea kung’ara katika utakatifu wake mbele ya Mwenyezi Mungu. Kwa waamini wanaotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha yao, wanaonja pia huruma na upendo wa Bikira Maria, Mama mwenye huruma anayewakirimia dawa ya matumaini, wale wote wanaoteswa na kukata tamaa ya maisha! Ni Mama ambaye yuko tayari kupanguka machozi ya toba, wale wote wanaotubu na kujutia dhambi na udhaifu wao wa kibinadamu!

Ni Mama ambaye yuko tayari kuwasindikiza wakosefu mbele ya Kristo Yesu, Hakimu mwenye haki na huruma kwa wadhambi wanaotubu kutoka katika undani wa maisha yao! Mtakatifu Anthoni wa Padua anasema, huruma ya Mungu imepata maficho kwa Bikira Maria, anayewapatia maisha mapya wale wote wanaokimbilia: huruma, ulinzi na tunza yake ya kimama na kamwe hajawahi kumgeuzia mtu kisogo na kwamba, anawalisha na kuwanyonyesha kwa “maziwa ya neema ya Mungu”. Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenye heri na watakatifu katika kitabu chake kuhusu: “Watakatifu na Bikira Maria Mama wa Mungu” anahitimisha kitabu hiki kwa kusema, hata leo hii watu bado wanaokimbilia Bikira Maria Mama wa huruma, wakiomba ulinzi na tunza yake ya kimama katika shida na mahangaiko yao mbali mbali!

Itakumbukwa kwamba, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kristo Yesu ndiye chemchemi na utimilifu wa utakatifu wote! Mama Kanisa anawahimiza waamini kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu na wawe na matunda ya Roho Mtakatifu ili wafanywe watakatifu. Kutokana na udhaifu wa binadamu, waamini wanahitaji mara kwa mara kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Wakristo wote wanaitwa na kuhamasishwa kushiriki utakatifu mmoja, kwa kumtii na kumwabudu Mwenyezi Mungu katika roho na kweli; kwa kumfuasa Kristo Yesu aliyekuwa ni: mtii, fukara na mnyenyekevu wa moyo, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kwa njia hii, wastahilishwe kushiriki utukufu wa Kristo Mfufuka!

Upendo wa dhati ni njia inayoweza kuwapeleka waamini katika utakatifu! Wanapaswa pia kusikiliza, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Waamini wajitahidi kushiriki kwa ukamilifu na mara kwa mara Sakramenti za Kanisa; kwa kujitia uthabiti katika kusali, kujinyima pamoja na kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa wahitaji zaidi. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo”. Baba Mtakatifu anasema, utakatifu ni mwaliko kwa waamini wote na wala si kwa watu wachache tu ndani ya Kanisa!

Huu ni mwaliko wa kuongeza jitihada za kukutana na Kristo Yesu katika maisha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata na kukumbatia: huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Watakatifu ni watu wa kawaida kabisa, ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, leo hii wamekuwa ni marafiki zake wa karibu! Watakatifu ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya watu! Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wote wamejichukulia dhamana ya kuanza hija ya utakatifu wa maisha jambo linawezekana, ikiwa kama waamini watapania na kulivalia njuga!

Na Padre Richard. A. Mjigwa. C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.