2018-04-07 10:56:00

Mchakato wa kuendelea kupyaisha huruma ya Mungu katika maisha!


Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko aliteuwa Wamisionari wa huruma, ili waweze kuwa ni ishara ya hamasa ya kimama ya Kanisa kwa Taifa la Mungu, wakiwezeshwa kuingia kwa undani katika utajiri wa fumbo la msingi la imani. Hawa ni mapadre waliopewa dhamana na wajibu wa kuwaondolea watu hata dhambi ambazo kwa kawaida, huondolewa na Kiti cha kitume pekee, ili upana wa utume wao uonekane wazi. Hawa ni ishara ya huruma ya Baba wa milele kwa watoto wake wanaokimbilia huruma na upendo wake usiokuwa na kikomo! Hawa ni Wamisionari wa huruma kwani wanatumwa na Mama Kanisa kama vyombo vinavyotoa hamasa ya kushinda vikwazo na kuanza maisha mapya ya Ubatizo, daima wakijitahidi kuwa waaminifu, kwa kumkazia macho Yesu, Kuhani mkuu, wenye rehema na mwaminifu katika mambo ya Mungu. Wamisionari hawa wakaanza utume wao rasmi, Jumatano ya Majivu, Februari 2016.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” “Huruma na haki” akawathibitisha Wamisionari wa huruma ya Mungu kuendelea na utume wao kama kielelezo hai cha neema ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Lengo la Baba Mtakatifu ni kuwaondolea waamini vikwazo na vizingiti vilivyokuwa vinawazuia kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu kwa njia ya wongofu wa ndani, toba, msamaha na upatanisho. Mapadre kwa nguvu ya Sakramenti waliyoipokea sasa wameongezewa madaraka ya kuweza hata kusamehe dhambi ya utoaji mimba ambayo hapo awali ilikuwa imeachwa rasmi kwa Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Lengo ni kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa Katoliki.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji Mpya anasema, mkutano huu ni mwendelezo wa tasaufi ya huruma ya Mungu iliyomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu. Hadi sasa kuna Wamisionari wa huruma 897 na kati yao 550 wanahudhuria mkutano ulioandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji Mpya kuanzia tarehe 8-11 Aprili 2018. Huu utakuwa ni muda wa: Sala, Katekesi, Shuhuda, Taarifa na Maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.

Kilele cha mkutano huu ni hapo tarehe 10 Aprili 2018 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu na hatimaye, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Papa Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wawezeshaji wakuu katika mkutano wa wamisionari wa huruma ya Mungu ni viongozi wakuu kutoka katika Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na Maaskofu wakuu walioalikwa kutoa mada mbali mbali. Kati ya mada hizi ni “Upatanisho: Ni Sakramenti ya huruma ya Mungu! Dhambi na huruma ya Mungu katika maisha na utume wa Padre: Wamisionari wa huruma ya Mungu kadiri ya mtazamo wa Papa Francisko pamoja na Ushauri wa kichungaji kuhusu Sakramenti ya Upatanisho!

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anakaza kusema, huduma hii inatolewa kwa faragha kubwa sana na kwamba, Wamisionari wa huruma ya Mungu, wamekuwa ni msaada mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa kama kielelezo cha uwepo na ukaribu wa Mungu katika maisha ya waamini wake. Kama alivyosema Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa ya Krisma ya Wokovu kwa mwaka 2018. Ukweli wa Kiinjili uguse undani wa maisha ya watu, ili kwa njia ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, Yesu mwenyewe aweze kuwagusa, kuwaganga na kuwaponya waja wake, ili hatimaye, waamini waweze kumwabudu Mungu katika Roho na kweli kwa kutambua dhambi na udhaifu wao wa kibinadamu, tayari kutubu na kumwongokea Mungu. Kumbe, Wamisionari wa huruma ya Mungu ni alama ya ukaribu wa Mungu kwa waja wake.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anasema, kuna uhusiano mkubwa kati ya huruma ya Mungu na utakatifu wa maisha! Kwa maneno machache utakatifu ni hija ya ushuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Utakatifu ni dhamana, wito na wajibu katika maisha ya waamini, ili kupata utimilifu wa maisha. Hii ni changamoto kwa waamini kukimbilia katika Mahakama ya huruma ya Mungu, ili Kristo Yesu aweze kuwasafisha kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.