2018-04-06 08:50:00

Askofu mkuu mstaafu Lebulu: "Dhana ya Sinodi" & "Familia ya Mungu"


Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuendeleza safari ya Kanisa iliyoanzishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa kukazia dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, ili kweli zile “cheche za mageuzi” zilizoletwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ndani ya Kanisa, ziweze kumwilishwa katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa katika ulimwengu mamboleo! Kwa hakika Kanisa,  halina budi kufanya hija ya kumwelekea Kristo Yesu, huku likiwasaidia watu wa Mungu kukutana, kuzungumza, kujadiliana, kutafakari na kusali kwa pamoja, ili wote wakiwa wameshikamana waweze kusonga mbele kumwendea Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.

Hii ndiyo dhana ya Sinodi inayopewa msukumo wa pekee na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa. Anasema, Kanisa halina budi kuwaambata wote kwa kujiaminisha chini ya ulinzi, tunza, uongozi na karama za Roho Mtakatifu. Ni wajibu wa Maaskofu kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, ili wote kwa pamoja, waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee: “Urika wa Maaskofu” na “Dhana ya Sinodi” katika uongozi  kuanzia ndani ya Makanisa mahalia, sanjari na uwajibikaji makini wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Mambo mengine ni Uekumene na Huruma kama mihimili mikuu ya kichungaji; uhuru wa kidini wa mtu binafsi, watu wote na taasisi katika ujumla wake. Umuhimu wa ushiriki wa waamini walei walio wazi na wenye mwelekeo chanya katika maisha na utume wa Kanisa; ushirikiano kati ya Kanisa na Serikali hata katika tofauti zao ni kati ya mambo msingi yanayoweza kutekelezwa kwa dhati na Sheria za Kanisa kama chombo cha majiundo, ili kuwasaidia Wakristo kukua na kukomaa na hatimaye, kujisikia kuwa ni sehemu ya utamaduni unaojibu kwa dhati kabisa mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Askofu mkuu Mstaafu Josaphat  Louis Lebulu wa Jimbo Kuu Katoliki Arusha, Tanzania katika mahojiano na Vatican News anasema, katika maisha na utume wake kama Askofu amekazia dhana ya Sinodi na familia ya Mungu kama nguzo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; utume, ari na maisha ya kimisionari unaoliwezesha Kanisa kukita mizizi yake katika uhalisia wa maisha ya watu.

Uhai na umoja wa familia ya Mungu Jimbo kuu Katoliki la Arusha ni kati ya vipaumbele vilivyovaliwa njuga na Askofu mkuu mstaafu Lebulu. Aliwataka waamini kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa mahalia. Familia ziwe kweli ni Makanisa madogo ya nyumbani na kwamba, Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ziwe ni shule ya Injili ya huruma, upendo, imani na mshikamano. Kila mwamini alipaswa kutambua haki, wajibu na nafasi yake katika maisha na utume wa Kanisa mahalia!

Anasema, imewachukua Watu wa Mungu Jimbo kuu la Arusha takribani miaka kumi na miwili kuanza mchakato wa ujenzi wa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Arusha. Lengo kuu kwanza kabisa lilikuwa ni kujenga na kuimarisha Familia ya Mungu Jimbo kuu la Arusha, kabla ya kuanza kufikiria ujenzi wa Kanisa kama jengo, mahali pa ibada. Familia ya Mungu ilipaswa kujisikia kweli kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa kwa njia ya uhai na umoja na kwamba, Kanisa kuu la Jimbo ni kielelezo cha uhai na umoja wa Familia ya Mungu.

Askofu mkuu mstaafu Lebulu anabainisha kwamba, mkakati wa pili ulikuwa ni kukusanya rasilimali sanjari na kuunganisha nguvu kutoka kwa kila Mwana familia ya Mungu Jimbo kuu Katoliki la Arusha, kadiri ya uwezo na nafasi yake; kwa kutambua umuhimu wa kulitegemeza Kanisa mahalia, kwa njia ya sadaka, zaka na michango mbali mbali. Mkakati huu ulipania kujenga Kanisa kuu la Jimbo kuu Katoliki Arusha.

Hii ni ishala ya uhai na umoja wa Kanisa, kama Familia ya Mungu inayowajibika. Azimio la kujenga Kanisa kuu la Jimbo kuu la Arusha ni mchango wa Sinodi ya kwanza ya Jimbo  kuu Katoliki Arusha iliyoadhimishwa kunako mwaka 2000, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Jubilee ya miaka elfu mbili ya Ukristo. Hapa Familia ya Mungu ikaweka nia, ikajiangalia ilipotoka, mahali walipo na wapi wanataka kwenda kwa siku za usoni, kwa kuangalia pia vipaumbele vyao katika maisha na utume wa Kanisa mahalia.

 Mkakati wa tatu anasema, Askofu mkuu mstaafu Lebulu ni ukusanyaji wa fedha hatua kwa hatua sanjari na ukusanyaji wa vifaa vya ujenzi. Kuna kamati ya ujenzi wa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Arusha, inayowajibika kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha zinazokusanywa. Ni matumaini ya Familia ya Mungu Jimbo kuu Katoliki la Arusha kwamba, Jubilee ya miaka hamsini ya uwepo na utendaji wa Jimbo kuu Katoliki Arusha, utaweza kuona ujenzi wa Kanisa kuu ukiwa umefikia hatua inayoridhisha. Kilele cha maadhimisho ya Jubilee hii ni wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Kristo Mfalme, kunako mwaka 2013.

Askofu mkuu mstaafu Lebulu anasema dhana ya “Sinodi” na “Familia ya Mungu” ni mambo ambayo Jimbo kuu la Arusha limejitahidi kuyamwilisha katika maisha na utume wa Kanisa mahalia mintarafu shughuli za kichungaji, programu na miradi ya maendeleo endelevu ya binadamu! Mambo yote haya ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Dhana ya Familia ya Mungu ni changamoto katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo kwa kuendelea pia kusoma alama za nyakati!

Askofu mkuu mstaafu Lebulu anatambua na kuthamini uwepo na msaada wa Roho Mtakatifu anayeangaza na kuwaongoza wafuasi wa Kristo na wala hana wasi wasi kwamba, kazi ya Kristo Yesu itasonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Anatambua na kukikiri kwamba, viongozi wa Kanisa ni vyombo tu, tena ni vyombo dhaifu ambavyo vinategemea neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni vyombo vya udongo vinavyohifadhi hazina kubwa ambayo ni Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai. Huyu ndiye anayepaswa kubebwa na familia ya Mungu, Jimbo kuu Katoliki la Arusha, Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.