2018-04-01 12:30:00

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Pasaka 2018: "Urbi et Orbi"


Baba Mtakatifu Francisko katika Sherehe ya Ufufuko wa Kristo Yesu, yaani Pasaka ya Bwana, Jumapili tarehe 1 Aprili, 2018 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican na kuhudhuriwa na bahari ya watu kutoka ndani na nje ya Italia. Katika ujumbe wake wa Pasaka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” amekazia kwamba, Kristo Yesu Mfufuka ni tumaini la ulimwengu! Wakristo wanamwomba Mwenyezi Mungu ajalie amani duniani; upatanisho, matumaini, majadiliano, faraja kwa watu waliokata tamaa na wale wote wanaoteseka, kudhulumiwa na kunyanyaswa katika utu na heshima yao kama binadamu!

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake wa Pasaka amesema kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka ni sawa na chembe ya ngano ambayo imekufa ili kutoa mazao mengi. Alisulubiwa, akafa na kuzikwa kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, kielelezo cha upendo wa Mungu unaomwilishwa hadi katika hatua ya chini kabisa, ili kuweza kuupyaisha ulimwengu, ili matunda yake yaweze kuonekana hata katika historia mamboleo inayogubikwa na ukosefu mkubwa wa haki msingi za binadamu, vita, kinzani na mipasuko. Kristo Mfufuka awakirimie walimwengu matumaini, utu na heshima mahali ambapo kuna umaskini na ubaguzi; mahali pale ambapo watu wanateseka na kufa kutokana na baa la njaa na ukosefu wa fursa za ajira. Kristo Mfufuka awe kati ya wakimbizi na wahamiaji wanaonyanyaswa na kudhulumiwa kiasi hata cha kukataliwa, ili uwepo wa Kristo uwe ni faraja kwao! Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, Kristo Mfufuka awe ni faraja na nguvu kwa waathirika wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo.

Mama Kanisa katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuleta amani duniani, lakini zaidi huko Siria ambako vita imepamba moto na watu hawajui lini vita hii itakoma. Mwanga wa Kristo Mfufuka, uangaze dhamiri za wale wote wanaohusika yaani; wanasiasa na vikosi vya ulinzi na usalama kusitisha mara moja mauaji; kwa kuheshimu haki msingi za binadamu sanjari na kutoa nafasi kwa misaada ya kibinadamu ili iweze kuwafikia waathirika! Wakimbizi na wananchi wasiokuwa na makazi maalum nchini Siria wawe na uhakika wa kuweza kurejea salama salimini katika makazi yao.

Baba Mtakatifu katika Ujumbe wake wa Pasaka ameombea upatanisho katika Nchi Takatifu ambako kwa siku za hivi karibuni, kumekuwepo na machafuko makubwa yaliyopelekea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Baba Mtakatifu anayakumbuka mateso na mahangaiko ya wananchi wa Yemen na Mashariki ya Kati katika ujumla wake, ili kweli majadiliano katika ukweli, uwazi na kuheshimiana vishinde mipasuko na vita! Wakristo huko Mashariki ya Kati wanaoteseka, kunyanyaswa na kudhulumiwa, waendelee kuwa ni mashuhuda amini wa Kristo Mfufuka na ushindi wa wema dhidi ya ubaya.

Baba Mtakatifu anaombea matunda ya matumaini yaweze kuwafikia watu wote duniani, lakini zaidi Barani Afrika, ambako watu bado wanateseka kwa baa la njaa, vita, kinzani na vitendo vya kigaidi. Amani ya Kristo Mfufuka igange na kuponya majeraha ya wananchi wa Sudan ya Kusini; afungue mioyo ili kujadiliana na hatimaye kuweza kuelewana. Mama Kanisa anayakumbuka mateso na mahangaiko ya watoto wanaoteseka kutokana na vita huko Sudan ya Kusini. Watu wenye mapenzi mema, wathubutu kuonesha upendo na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji ambao wanakosa hata mahitaji yao msingi katika maisha! Baba Mtakatifu anaombea majadiliano kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini, ili majadiliano yaliko mezani yazidi kusonga mbele ili kudumisha amani na utulivu katika ukanda huu. Wahusika wakuu, wang’amue, waamue na kutenda kwa busara ili kukuza na kudumisha ustawi, mafao na maendeleo ya wananchi wote wa Korea na hatimaye, waweze kujenga mafungamano ya kuamianiana katika Jumuiya ya Kimataifa.

Baba Mtakatifu Francisko anaombea matunda ya amani kwa ajili ya Ukraine, ili mchakato unaopania kuleta maridhiano uweze kufanikiwa kwa kufumbatwa pia katika huduma za kiutu kwa wananchi ambao wanakabiliwa na mahitaji msingi kwa wakati huu. Matunda ya faraja yawafikie na kuwagusa wananchi wa Venezuela, kama walivyoandika viongozi wao wa Kanisa kwamba, “kwa sasa wanaishi katika nchi ya ugeni”. Nguvu ya Kristo Mfufuka iwasaidie kuona njia muafaka itakayodumisha amani na utu wema, ili hatimaye kuondokana na kipeo cha kisiasa na cha kiutu kinachoendelea kuwatumbukiza wananchi wengi katika maafa makubwa. Wananchi wa Venezuela wanaolazimika kuikimbia nchi yao, wapate usalama na hifadhi ya maisha yao.

Matunda ya maisha mapya ya Kristo Mfufuka yawafikie watoto ambao kutokana na vita, njaa, magonjwa na umaskini wanakosa matumaini ya maisha! Matunda haya pia yawaguse wazee wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na uchoyo na ubinafsi, kwa vile tu, “si mali kitu” kwani hawawezi kushiriki katika mchakato wa uzalishaji na utoaji wa huduma. Baba Mtakatifu anaombea matunda ya hekima na busara yawafikie na kuwaambata viongozi wa kisiasa ili waweze kuheshimu utu wa binadamu, kwa kujizatiti katika huduma, ustawi, mafao na maendeleo ya watu wao, daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa usalama wa raia na mali zao. Mwishoni Baba Mtakatifu anasema, kwa hakika Kristo Yesu amefufuka kwa wafu wala kifo na upweke havina tena neno la mwisho, kwani nguvu ya Ufufuko imeshinda yote haya! Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahi kusema kwamba, nguvu ya upendo wa Mungu inashinda ubaya, inaosha dhambi na kuwarejeshea tena wadhambi utakatifu wao; furaha kwa wanaoteseka kutokana na chuki na uhasama. Nguvu ya upendo wa Mungu inawashikisha adabu “wenye nguvu”; inakoleza maridhiano na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.