2018-03-31 09:00:00

Vijana wanahimizwa kuwa ni mashuhuda wa sadaka ya upendo!


Ibada ya Ijumaa Kuu, Mama Kanisa anapokumbuka: Mateso na Kifo cha Kristo Msalabani anawaalika watoto wake kuinua macho yao kuelekea katika Fumbo la Msalaba ambako ndiko mahali ulipotundikwa wokovu wa dunia hii, yaani Kristo Yesu. Ibada hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Sehemu ya kwanza ni Liturujia ya Neno la Mungu, ambamo masomo huweka mateso makali ya Kristo Yesu mbele ya macho yao, ili kuteseka, kufa na hatimaye kufufuka na Kristo kutoka kwa wafu! Hii ni nafasi kwa Kanisa kusali kwa ajili ya kuwaombea watu na mahitaji mbali mbali, ili hatimaye, watu wa Mungu wapate wokovu kwa njia ya Fumbo la Msalaba.

Sehemu ya Pili ni: Kuabudu Msalaba Mtakatifu, ufunuo wa: hekima, huruma, upendo, wema, na msamaha wa Mungu kwa watu wote. Waamini wanamwabudu Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani, akafa na kufufuka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mausti. Sehemu ya tatu: Waamini wanashiriki Komunyo Takatifu ili kujazwa uzima wa kimungu tayari kushiriki katika mateso, kifo na hatimaye, waweze kufufuka pamoja na Kristo, ili waendelee kuwa ni mashuhuda wake kama ilivyokuwa kwa Mwinjili Yohane!

Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa katika mahubiri yake, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Ibada ya Mateso ya Kristo Yesu, Ijumaa kuu, tarehe 30 Machi 2018 amekazia kuhusu umuhimu wa ushuhuda, ujumbe kwa vijana, Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana pamoja na changamoto katika maisha na utume wa vijana mintarafu Fumbo la Msalaba! Chini ya Msalaba kulikuwepo na Bikira Maria, Mama wa Yesu na Mwanafunzi yule aliyempenda amesimama akashuhudia mateso, kifo na hatimaye akawa pia ni shuhuda wa Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu!

Yohane Mtume ni shuhuda amini wa Mwana Kondoo wa Mungu aliyechinjwa sadaka! Kwa kuchomwa ubavuni mwake, ikatoka damu na maji, alama ya Sakramenti za Kanisa, mwanzo wa maisha mapya na utimilifu wa yote. Msalaba ni ufunuo wa ukuu wa Mungu katika unyonge wake; hekima ya Mungu dhidi ya ujinga wa binadamu na mwishoe ni ufunuo wa utajiri wa Mungu katika umaskini wake. Msalaba ni ushuhuda wa upendo mkuu wa Mungu kwa binadamu, kiasi hata akamtuma Mwanawe kuwa ni kipatanisho kwa dhambi za binadamu. Yesu aliwapenda watu wake upeo, kiasi hata cha kuteseka na hatimaye kufa Msalabani.

Padre Raniero Cantalamessa anasema, wakati huu Mama Kanisa anapoendelea na maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana, anapenda kutoa kipaumbele cha pekee katika Fumbo la Msalaba kama sehemu ya sera na mikakati ya Mama Kanisa kwa utume miongoni mwa vijana. Mwinjili Yohane ni kati ya mitume vijana waliopendwa sana na Kristo Yesu, kiasi hata cha kuwa ni shuhuda amini wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima; mwanga na mlango wa maisha ya uzima wa milele.

Mtume Yohane ni kati ya wale wafuasi wa Yohane Mbatizaji, walipokea wito na mwaliko wa kwanza kwanza wa kumfuasa Kristo, wakaamua kubaki pamoja naye na tangu wakati huo, maisha yake yakapata mwelekeo mpya! Mtume Yohane awasaidie vijana kuwa na furaha na maisha tele. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anawaalika Wakristo wote mahali popote pale walipo kujibidisha kukutana na Kristo kwa kutambua kwamba, Kristo anatoa mwaliko kwa wote kukutana naye bila ubaguzi, ili kuonja furaha inayobubujika kutoka kwa Yesu, ili kuleta mageuzi katika maisha!

Yohane katika Waraka wake wa kwanza anasema, anawaandikia Waraka huo vijana kwa sababu wana nguvu na Neno la Mungu linakaa ndani mwao na wao wamemshinda yule mwovu. Anawataka vijana wasiipende dunia na mambo yake! Wajitaabishe kuwajali, kuwapenda na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana wawe tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya watu wanaoteseka na kunyanyaswa; vijana wawe tayari kujitenga na ubinafsi na uchoyo kwani bila kufanya hivyo, watakuwa chini ya utawala wa shetani, Ibilisi. Vijana wajizatiti kusimamia na kupigania haki msingi za binadamu na kamwe wasikubali kutumiwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa ajili ya kupandikiza maovu! Vijana wawe tayari kushindana na mawimbi yanayoweza kuwatumbukiza katika ombwe la maisha kwa kumkimbia Kristo Yesu, rafiki na mkombozi wa ulimwengu.

Vijana wawe ni mashuhuda wa upendo unaoweza kujisadaka kama ule uliofunuliwa na Kristo pale juu mlimani Kalvari! Huu ni upendo unaofumbatwa katika huduma kwa Mungu na jirani; upendo unaoheshimu na kuthamini utu wa binadamu; upendo unaotakasa na kutoa mwelekeo mpya wa maisha kwani kuna furaha kubwa zaidi katika kutoa kuliko kupokea! Padre Raniero Cantalamessa anawataka vijana kujiandaa ili kuweza kujisadaka katika maisha ya ndoa na familia; katika maisha ya kipadre na kitawa; kwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, ingawa kuna umati mkubwa wa vijana wanaotekeleza yote haya bila “kujipigia debe.” Kristo Yesu pale Msalabani amewapatia waja wake mfano wa upendo usiokuwa na kifani na neema ya kuweza kuumwilisha upendo huo katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Damu na Maji yaliyotoka Ubavuni mwa Kristo Yesu ni alama za Sakramenti za Kanisa ambamo vijana wanaweza kukimbilia ili kupata faraja. Neno la Mungu liwasaidie kumwangalia kwa “jicho la imani”, Yesu Kristo Mteswa! Vijana waungane na watu wote wanamtaza yule waliyemchoma kwa uchungu, toba na imani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.