Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Ujumbe wa Pasaka 2018 kutoka kwa Askofu Mkude, Jimbo la Morogoro

Askofu Mkude: Anawataka waamini wajitahidi kumfahamu, kumwambata na kumshuhudia Kristo katika uhalisia wa maisha ya pamoja na kujitahidi kudhibiti vilema vya maisha yao!

31/03/2018 16:48

Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro katika Barua yake ya kichungaji kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kama sehemu ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka anagusia kuhusu matukio ya watu kupotea katika mazingira ya kutatanisha sanjari na Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara, mwaliko na changamoto ya kujitahidi kumjua Yesu Mfufuka, kuungana naye, kujitoa bila ya kujibakiza katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani kama kielelezo cha imani tendaji na mwishoni, anawaalika watanzania kushinda vilema vya maisha yao kwa kujikita katika tabia njema, bidii na juhudi ya kazi, maadili na utu wema, sadaka, utii wa sharia pamoja na dhamiri nyofu!

Askofu Mkude anasikitika kusema kwamba, pale ambapo mtu anapotoweka katika mazingira ya kutatanisha anaibua: simanzi, majonzi na huzuni kubwa miongoni mwa jamii, lakini zaidi sana miongoni mwa wapendwa wake! Amani na utulivu wa ndani hutoweka na matokeo yake hofu na machungu moyoni hutanda. Hivi ndivyo ilivyokuwa yapata miaka 2018 iliyopita, pale ambapo, Jumapili alfajiri na mapema wanawake walikwenda kaburini lakini hawakuuona mwili wa Yesu. Ushuhuda wa wanawake haukuaminiwa ndiyo maana Petro Mtume na Yohane wakatoka mbio kwenda kushuhudia yaliyotokea na kuona sanda,  Petro mtume akarudi nyumbani huku akiendelea kushangaa kwa yale yaliyotokea. Wanafunzi wa Emau walipata bahati ya kutokewa na Yesu, akatembea pamoja nao, wakamwona kwa macho lakini hawakumtambua! Hapa Askofu Mkude anapenda kutoa angalisho kuhusu watu waliotoweka katika mazingira ya kutatanisha kwani, Jamii inapenda kufahamu hatima ya maisha yao, ili kama wako hai wawezeshwe kurejea hima katika familia zao! Ikiwa kama wametangulia mbele za haki, basi, Mwenyezi Mungu awarehemu na kuwapatia maisha ya uzima wa milele!

Askofu Mkude anakaza kusema, Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa. Hili ni tukio la kweli ambalo limeshuhudiwa na watu na wala si hadhithi ya kubuniwa! Kwamba, Kristo Yesu aliteswa, akafa na kufufuka siku ya tatu kama yanenavyo Maandiko Matakatifu. Mitume wameshuhudia tukio hili la kihistoria, lakini hata Kristo Mfufuka aliwatokea na kuwaonesha makovu ya “Madonda yake Matakatifu”, akachukua kipande cha samaki na kula pamoja nao! Baada ya hapo, Yesu akawapatia Amri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, atakaye amini na kubatizwa ataokolewa. Asiye amini atahukumiwa.

Askofu Mkude anaendelea kudadavua kwamba, kusherehekea Fumbo la Pasaka ni kukiri katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka! Yaani, Kristo Yesu aliteswa kwa Mamlaka ya Ponsio Pilato, akasulubiwa, akafa na kuzikwa, siku ya tatu akafufuka kutoka kwa wafu. Hiki ni kilele cha ukweli wa imani ya Kanisa katika Kristo! Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumjua Yesu Mfufuka, kuungana, kujitoa na kujituma zaidi kwa huduma inayomwilishwa zaidi katika upendo kwa Mungu na jirani, kielelezo makini cha imani tendaji na wala si kufanya mambo kwa mazoea! Kama sehemu ya mchakato wa maadhimisho haya, familia ya Mungu nchini Tanzania inahamasishwa kufiriki na kuambata yale yaliyo juu, huku ikiongozwa na Roho Mtakatifu idumishe upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi, kwani haya ni matunda ya Roho Mtakatifu!

Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini Tanzania, wanapaswa kupyaisha maisha yao mintarafu Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Askofu James Spaita wa Jimbo Katoliki Mansa, nchini Zambia ameorodhesha vilema mamboleo ambavyo waamini wanapaswa kuvishinda kwa nguvu ya imani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Watanzania waepuke ujuzi bila ya kujikita katika tabia njema, utajiri wa haraka haraka bila kufanya kazi; biashara bila kuzingatia kanuni maadili; sayansi inayokinzana na utu; Ibada bila sadaka; Siasa bila kuzingatia kanuni na sheria za nchi na mwishoni ni furaha bila dhamiri nyofu. Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki Morogoro katika Barua yake ya kichungaji kama sehemu ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka anawaalika watanzania popote pale walipo kukuza na kudumisha tabia ya uchaji wa Mungu kwa kuepa vilema na kujikita katika mchakato wa kupalilia fadhila za Kristo Yesu, Mfufuka!

Ujumbe huu umehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

31/03/2018 16:48